Ukarabati huu, uliofanywa chini ya mpango wa uwekezaji wa kijamii wa benki, ‘Exim Cares,’ ni sehemu ya maono makubwa ya Benki ya kuimarisha mifumo ya afya nchini Tanzania kwa kuunda mazingira salama, jumuishi, na ya heshima kwa makundi yaliyo hatarini, hasa watoto na vijana wanaokabiliana na changamoto za afya ya akili.
Akizungumza wakati wa hafla ya makabidhiano, Afisa Mtendaji Mkuu wa Fedha wa Benki ya Exim, Bw. Shani Kinswaga, alisema mradi huu ni sehemu ya jitihada za muda mrefu za benki kuleta mabadiliko chanya ya jamii kupitia uwekezaji endelevu katika afya na ustawi wa jamii.
“Benki ya Exim siyo tu benki inayotoa huduma za fedha, bali pia ni sehemu ya mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii, na tumeelekeza hatua zetu za kwanza katika afya ya akili. Tunaamini kuwa afya ya akili si tu suala la matibabu, bali ni kipaumbele cha jamii na uchumi. Kitengo hiki kilichokarabatiwa hakionyeshi tu miundombinu, bali pia ni mwakilishi wa dhamira yetu ya pamoja ya kujenga matumaini na heshima kwa kizazi kijacho,” alisema Bw. Kinswaga.
“Kupitia Exim Cares, tumeahidi kukusanya jumla ya shilingi milioni 300 katika kipindi cha miaka mitatu ijayo kwa ajili ya kuboresha miundombinu na kampeni za uhamasishaji wa afya ya akili kote nchini. Ushirikiano wetu na Hospitali ya Taifa Muhimbili ni sehemu ya maono haya mapana kuhakikisha huduma za afya ya akili zinapatikana kwa urahisi, zinatolewa kwa ufanisi na kwa ukarimu,” aliongeza.
Bw. Kinswaga pia alitaja mchango wa washirika wa sekta ya bima kama vile Alliance General, Strategis General, Heritage Insurance Co., Alliance Life, na MUA, ambao wameungana na Benki ya Exim kupitia Tamasha la Bima – Amsha Matumaini. Kampeni hii inalenga kuhamasisha jamii, kupambana na unyanyapaa, na kukusanya rasilimali kwa ajili ya msaada na huduma za afya ya akili.
“Ushirikiano wetu na washirika kutoka sekta ya bima, ni kielelezo thabiti cha kile kinachoweza kufanikishwa kupitia ushirikiano wa sekta binafsi na umma pale wanapounga mkono na kua na nia njema. Pamoja, hatuboreshi tu miundombinu, bali pia tunaongeza uelewa wa taifa kuhusu afya ya akili,” alisema.
Akikabidhiwa jengo lililokarabatiwa, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dkt. Delillah Charles Kimambo, alieleza shukrani zake kwa Benki ya Exim kwa kushirikiana na kuunga mkono jitihada za kuimarisha mifumo ya afya.
“Kitengo hiki kilichokarabatiwa cha Afya ya Akili kwa Watoto na Vijana kimekuja wakati muafaka, wakati changamoto za afya ya akili miongoni mwa vijana zinaongezeka nchini,” alisema Dkt. Kimambo.
“Maboresho haya yatawezesha kutoa huduma bora zaidi, kwa ukarimu na heshima, kwa wagonjwa wetu. Kwa niaba ya Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ningependa kupongeza Benki ya Exim kwa uthabiti wake katika kusaidia taasisi za umma za afya na kutambua afya ya akili kama sehemu muhimu ya ustawi wa taifa,” aliongeza.
Jengo lililokarabatiwa lina vyumba vya wagonjwa vilivyoimarishwa, vyumba vya ushauri na tiba, maeneo ya mafunzo na ofisi za wahudumu wa afya, vyote vikiwa na vifaa vya kisasa na mpangilio mpya unaounda mazingira tulivu, salama, na rafiki kwa watoto. Mazingira haya yameundwa ili kuhamasisha uponyaji na kurejesha matumaini kwa watoto na vijana wenye changamoto za afya ya akili.
Uingiliaji wa Benki ya Exim unafuata takwimu zinazoongezeka kuhusu idadi ya wagonjwa wa afya ya akili nchini. Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, idadi ya wagonjwa wa afya ya akili imeongezeka kutoka 386,000 mwaka 2012 hadi zaidi ya milioni 2 mwaka 2021, jambo linalosisitiza hitaji la haraka la kuboresha miundombinu na kampeni za uhamasishaji.
Kupitia Exim Cares, Benki imekuwa ikitekeleza miradi yenye athari kubwa kitaifa, ikiwa ni pamoja na kampeni za kuchangia damu, kusaidia elimu, mafunzo ya fedha kwa wanawake na vijana kupitia Women Empowerment Programme (WEP), na kampeni za kuhifadhi mazingira. Afya ni mojawapo ya nguzo tano za mpango huu, kando na Elimu, Mazingira, Uwekezaji wa Kijamii, na Ubunifu.
Benki imehakikisha kuwa ukarabati huu wa Muhimbili si mradi wa pekee, bali ni sehemu ya safari endelevu ya kuimarisha mifumo ya afya nchini kupitia uwekezaji endelevu na ushirikiano wa pamoja.
“Tunajivunia kuwa sehemu ya hadithi hii ya matumaini,” alimalizia Bw. Kinswaga. “Wakati sekta binafsi na taasisi za umma zinaposhirikiana kwa manufaa ya jamii, matokeo ni Tanzania yenye nguvu zaidi, yenye afya bora, na yenye ustawi wa kweli.”