Yanga waishi kibosi Malawi, wafikia kwenye hoteli hii

Msafara wa Yanga umetua ndani ya ardhi ya Malawi ukiwa na zaidi ya watu 50 ambao unajumuisha wachezaji, maofisa wa benchi la ufundi, viongozi, maofisa, waandishi wa habari pamoja na mashabiki wa timu hiyo.

Safari ya Yanga ilianza jijini Dar es Salaam mnamo saa 1:00 na kabla ya saa 3 asubuhi ikawa imeshakamilika kwa jopo hilo kutua ndani ya ardhi ya Malawi.

Jijini Lilongwe, Malawi ndiko ambako Yanga imefikia na mchezo wake dhidi ya Silver Strikers utachezwa hapo keshokutwa Jumamosi katika Uwanja wa Taifa wa Bingu uliopo jijini hapo.

Sasa baada ya kufika Malawi, Yanga imeonyesha jeuri ya fedha iliyonayo kwa kufikia katika Hoteli ya Kifahari zaidi jijini Lilongwe ambaye timu nyingi kubwa ndio huwa zinafikia hapo zikienda kucheza nchini humo.

Hoteli hiyo ya hadhi ya Nyota tano ni President iliyopo katikati ya jiji la Lilongwe ambayo gharama ya chini ya Chumba kimoja ni Shilingi 500,000.

Baadhi ya timu ambazo zimewahi kufikia hoteli hiyo ni Simba pamoja na timu za taifa za Senegal na Tunisia ambazo zimewahi kwenda nchini Malawi kucheza na timu ya taifa ya nchi hiyo.

Hoteli hiyo ndani yake ina Kituo kikubwa zaidi cha mikutano nchini Malawi cha Mikutano cha Kimataifa cha Bingu Wa Mutharika.

Baadhi ya huduma nyingine muhimu zilizopo katika hoteli hiyo ya kisasa ni bwawa la kisasa la kuogelea la nje, spa na kituo cha ustawi na sauna.  Wageni wanaweza kufurahia mchezo wa tenisi au mazoezi katika kituo cha mazoezi ya mwili.

Hoteli hiyo ambayo Yanga wamefikia, iko umbali wa Kilomita 27 kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Lilongwe.

Mchezo baina ya Silver Strikers umepangwa kuchezwa Jumamosi kuanzia saa 10:00 jioni kwa muda wa Afrika Mashariki.