Dodoma. Je, Watanzania wanarudi tena katika zama za matumizi ya mizizi, majani na magome ya miti kwa ajili ya tiba?
Ni swali linalochochea mjadala mkubwa katika jamii, hasa wakati huu ambapo huduma za kisasa za afya zimeenea kila kona ya nchi.
Tanzania imepiga hatua kubwa katika ujenzi wa zahanati, vituo vya afya, hospitali na hospitali za rufaa.
Hali hiyo imesababisha watu wengi kukimbilia tiba za kisayansi kila wanapopata changamoto za kiafya. Asante kwa Serikali ya awamu ya sita kwa jitihada zake za kuhakikisha huduma za afya zikipatika Karibu kila eneo nchini.
Hata hivyo, utafiti unaonyesha kuwa licha ya uwepo wa huduma hizo, bado kuna idadi kubwa tu ya Watanzania wanaotafuta tiba asili.
Asilimia 60 hutumia tiba asili
Mkurugenzi wa Huduma za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dk Ahmad Makuwani, anasema takribani asilimia 60 ya Watanzania hutafuta huduma za kiafya kwa kutumia tiba asili.
Hata hivyo, hakuna utafiti wa kina unaoonyesha kama watumiaji hao ni wakazi wa vijijini au mijini.
Akizungumza kwenye kongamano la nne la kisayansi la tiba asili lililofanyika jijini Dodoma, Dk Makuwani alisema kuna maeneo ambayo dawa za asili hufanya vizuri zaidi kuliko tiba za kisasa.
Alitoa mfano wa kipindi cha janga la Uviko-19 ambapo tiba hizo zilitumika kwa wingi.
“Katika kipindi cha Uviko-19 tiba asili zilionekana kutusaidia zaidi. Changamoto iliyopo ni ukosefu wa mifumo thabiti ya kirufaa ambayo ingeweza kutuokoa zaidi,” alisema na kusisitiza wanaojua tiba za asili kurithisha ujuzi wao kwa wengine hasa vijana, akisema ulinzi wa misitu ni sawa na uchumi kwa Taifa.
Joel Mangula (Mzigula), mganga wa tiba asili kutoka Dodoma, anasema idadi ya Watanzania wanaotumia dawa za asili imeongezeka kwa kasi, ingawa changamoto kubwa ni upatikanaji wa miti kutokana na uharibifu wa mazingira.
“Faida ya tiba hii ni uhakika wa matibabu na gharama nafuu ikilinganishwa na tiba za hospitali. Lakini miti mingi imepotea, na hivyo dawa hupatikana mbali na kwa gharama kubwa,” alisema Mangula aliyerithi elimu ya tiba kutoka Kwa babu yake.
Mwajuma Mnghunungu, mganga mwingine wa tiba asili, anasema tiba hizo zimewasaidia watu wengi kupona hata magonjwa makubwa. Hata hivyo, anataja tatizo la baadhi ya waganga wasio na uwezo wanaotapeli wagonjwa kwa matangazo ya kishirikina.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Profesa Said Aboud, anasema hivi sasa Serikali inaboresha huduma za tiba asili kwa kuanzisha hospitali 14 za rufaa zinazotoa tiba jumuishi.
Anasema dawa 26 za asili zimeidhinishwa kutolewa hospitalini na wagonjwa wanaruhusiwa kuchagua huduma.
“Kwa sasa Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili na Ocean Road zinafanya utafiti wa tiba asili kwa saratani ya matiti na tezi dume, na matokeo yanaendelea vizuri,” alisema Profesa Aboud.
Hata hivyo, alionya kuhusu baadhi ya waganga wasioidhinishwa wanaotumia mwanya huo kutapeli wananchi.
Kwa mujibu wa Sheria ya NIMR ya mwaka 1979, tiba zote za asili lazima zipitiwe na taasisi hiyo ili kuhakikisha hazina madhara kwa afya ya binadamu. Lakini changamoto kubwa, anasema Profesa Aboud, ni waganga wengi kukataa kupeleka sampuli zao maabara kwa hofu ya kupokonywa umiliki.
Mwenyekiti wa Baraza la Tiba Asili, Profesa Joseph Otieno, alisema taratibu za kuwatambua watoa huduma zipo wazi na hakuna urasimu katika kupata vibali na leseni.
“Watu hawatafuti tiba asili kwa sababu ya gharama nafuu pekee, bali kwa sababu wanataka kupona na mara nyingi matokeo huonekana haraka,” alisema Profesa Otieno.
Joseph Luwoneko, mkazi wa Godegode, Wilaya ya Mpwapwa, anasema:
“Mimi nimekuwa nikitumia dawa asili muda mrefu na siwezi kukimbilia hospitali isipokuwa daktari akinishauri. Kwa kweli tiba za asili zinabeba suluhisho la magonjwa mengi.”
Hata hivyo, alikiri kuwa magonjwa kama kifafa, kichaa na baadhi ya maradhi ya kurithi bado hutibiwa zaidi kwa tiba za kisayansi.
Kwa upande wake. Mchungaji Laurent Masanyika anakiri huduma za tiba asili ni salama zaidi wakati mwingine kuliko matibabu ya kisasa.
Mchungaji Masanyika anasema tangu zamani Wafrika waliishi kwa kutumia tiba asili na hakukuwa na magonjwa mengi ya ajabu lakini kila walipougua walitumia dawa hizo na kupona.
“Tatizo ni watu wanaoibuka na kujiita waganga wa tiba asili, lakini kama wangefuatiliwa hawa waache kufanya hivyo wabaki wale wenye kujua miti ya asili, wangetusaidia na kuisaidia Serikali yetu,” anasema.
Hata hivyo, mchungaji anasisitiza utafiti ufanyike ili kuthibitisha ubora wa dawa kutokana na kuibuka kwa wimbi la watoa huduma hiyo ambao baadhi wanakosa cha kufanya hivyo wanaibuka kupitia matatizo ya watu.
Naye Melea Nhonya anakiri hata sasa hapendi kutumia dawa za hospitali katika magonjwa ambayo anaamini yanaweza kutibika kwa dawa za asili.
Hata hivyo, anasema baadhi ya magongwa yanakosa dawa katika miaka ya hivi karibuni kwa sababu ya uharibifu wa mazingira uliokithiri ambao unafanya miti isipatikane kwa urahisi.
Kuhusu kupanda miti kwa ajili ya dawa, anasema haiwezi kuwa na uhalisia kama ilivyokuwa kwa miti ya zamani.