Makocha KMKM, Azam FC watambiana

WAKATI presha ya mechi ya kwanza ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika kati ya KMKM na Azam FC ikipanda, makocha wa timu zote wametambiana kabla ya pambano hilo.

Mechi hiyo itakayopigwa kesho Jumamosi Oktoba 18, 2025 saa 10:15, kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, inavuta hisia kubwa kutokana na timu hizo mbili kujuana vizuri, huku zikisaka rekodi mpya katika michuano ya kimataifa kwa kufuzu hatua ya makundi.

Akizungumza na Waandishi wa Habari, Kocha wa KMKM, Hababuu Ali, amesema licha ya ubora wa wapinzani wao, lakini wamejipanga kuhakikisha wanaandika rekodi mpya katika soka la Zanzibar.

“Tuna wachezaji wawili ambao ni majeruhi lakini hilo kwetu sio kigezo cha kufanya vibaya, licha ya ukweli kwamba wenzetu ni wazoefu, hatua hii tuliyofika ni kubwa ingawa tunahitaji zaidi ya hiki tulichokifanya,” amesema Hababuu.

Hababuu amesema licha ya kuikabili Azam kwa mara ya kwanza akiwa kocha mkuu wa KMKM, lakini hilo kwake analichukulia kama changamoto ya kawaida katika kazi, hivyo maandalizi waliyofanya ndiyo yatakayodhihirisha.

Kwa upande wa Kocha wa Azam FC, Florent Ibenge, amesema licha ya kiu kubwa ya timu hiyo kutaka kuandika rekodi mpya ya kufuzu hatua ya makundi kwa mara ya kwanza michuano ya kimataifa, lakini hahitaji kuwapa presha zaidi nyota wa kikosi hicho.

“Kuna faida na hasara kucheza na timu zinazotoka ukanda mmoja, lakini kwetu ni changamoto mpya na tunahitaji kuitumia ili kufikia malengo ambayo tumedhamiria msimu huu.

“Tumefanya maandalizi ya kutosha lakini hii ni mechi ya kwanza ambayo tunahitaji kuitumia vizuri kabla ya marudiano pale jijini Dar es Salaam,” amesema Ibenge.

KMKM imefika raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuitoa AS Port ya Djibouti kwa jumla ya mabao 4-2, huku Azam ikiitoa EL Merriekh Bentiu ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 4-0.

KMKM na Azam ni timu zinazofahamiana na mara kadhaa zimeshakutana katika mechi tofauti za kimashindano na hata kirafiki na hakuna anayeweza kumcheka mwenzake.

Mabaharia wa majini wa visiwani ambao kirefu cha jina lao la KMKM ni Kikosi Maalum cha Kuzuia Magendo, katika mechi mbili za mwisho za kimashindano imewanyanyasa Azam.

Ukiachana na mechi za kirafiki za hivi karibuni, rekodi zinaonyesha timu hizo zilikutana mara ya mwisho katika michuano ya Kagame 2021 na zote Azam ilipasuka.

Ilianza kukutana zikiwa Kundi A mechi iliyopigwa Agosti 11, 2021 na Azam kuduwazwa kwa kunyukwa mabao 3-2, licha ya kumaliza kama kinara wa kundi mbele ya KMKM iliyokuwa ya pili.

Azam iliyomaliza mechi hizo za makundi ikiwa na pointi sita, ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia Idd Kipagwile anayecheza Dodoma Jiji kwa sasa dakika ya 41.

Hata hivyo, KMKM ilirudi kipindi cha pili kibabe kwa kupindua meza kwa kusawazisha bao hilo kupitia Haji Simba Salim dakika ya 54, kisha Hasim Ali kuongeza la pili dakika ya 67 na Adam Ibrahim Abdalla akapigilia msumari wa tatu dakika ya 73.

Azam ilipata bao la pili la kufutia machozi dakika ya 83 kupitia Paul Peter, aliyepo kwa sasa kwa maafande wa JKT Tanzania akitokea Dodoma Jiji.

Siku chache baadae timu hizo zilikutana katika mechi ya kusaka mshindi wa tatu, katika mechi hiyo iliyopigwa Agosti 14, 2021, Azam ilichapwa tena bao 1-0, lililowekwa kimiani dakika ya 77 kupitia kwa Iliyas Mohammed na kuifanya KMKM kulipa kisasi cha kulala mabao 4-0 katika mechi ya makundi ya Kombe la Kagame 2014.