ACT Wazalendo yazitwisha ngome zake jukumu la ushindi urais Zanzibar

Unguja. Matumaini ya ushindi wa urais wa Zanzibar kwa tiketi ya ACT Wazalendo yameachwa kwenye Ngome za Vijana, Wanawake na Wazee za chama hicho, zilizopewa jukumu la kwenda nyumba kwa nyumba kusaka kura.

Majukumu mengine yanayotekelezwa na ngome hizo, ni pamoja kuelemisha Wazanzibari kuhusu sera za ACT Wazalendo, kuwahamasisha kujitokeza Oktoba 29, kukipigia kura chama hicho kuanzia udiwani, ubunge, uwakilishi hadi urais.

Hayo yamebainishwa leo Ijumaa Oktoba 17, 2025 wakati uzinduzi wa timu za ushindi wa Othman uliopewa jina la timu ‘OMO’ kupitia Ngome za Vijana, Wanawake na Wazee za ACT Wazalendo, kwa upande wa Unguja.

Septemba 29, 2025 Othman alizindua timu za ushindi za jumla zilizohusisha viongozi wa ACT Wazalendo kuanzia ngazi ya matawi, shehia, majimbo na mkoa zilizopewa pia jukumu la kutafuta kura ili ushindi kupatikana.

Katika uzinduzi huo, Katibu wa Ngome ya Wanawake ya ACT Wazalendo, Fatma Abdulhabib Ferej amesema, “Timu hizi zimeshamalizia kazi, lakini leo zinazinduliwa rasmi. Hii ni ishara ya kuonyesha matumaini ya ushindi katika chama chetu, wanawake ni ishara inayoonyesha wapo tayari.”

“Wanawake wa ACT Wazalendo wana mtandao mkubwa wa kufanya kazi kuanzia matawi, majimbo hadi Taifa.Timu hii ya wanawake imejenga hadhi ya ushindi katika kipindi,” ameeleza.
Ferej amefichua kuwa miongoni mwa majukumu waliopewa timu ya ushindi ya ngome ya wanawake ni kuhamasisha wananchi hasa wanawake kushiriki katika uchaguzi ikiwemo kugombea, kushiriki katika shughuli zote za kampeni za uchaguzi.

“Dhamira ya pili ilikuwa wanawake hawa, kuendelea kuelimisha wananchi kuhusu sera na mwelekeo wa ACT Wazalendo katika uchaguzi 2025 ili kuwavutia Wazanzibari kukipigia kura chama hiki,”

“Katika kipindi hiki wanawake wote hawa wakiwemo viongozi wapo kwenye shughuli ya Kwenda nyumba kwa nyumba, mtu kwa mtu kusaka kura za ushindi wa OMO. Si unajua wanawake hawana kipingamizi katika kuingia nyumba kwa nyumba, tofuti na wanaume, wajibu huo tunauelewa, kazi hii tunaifanya vizuri,”
Ferej amesema timu ya ushindi ya wanawake imejipanga siku ya Oktoba 29 wale wote wenye mahitaji maalumu wanafikishwa kwenye vituo vya kupiga kura ili kutumia haki ya msingi ya kuchagua viongozi wanaowahitaji.

“Tuhakikisha tunatoa mawakala wa kutosha katika kusimamia mwenendo wa kura katika vituo, tupo sambamba na timu ya ngome ya vijana, wazee,”

“Hizi timu za ushindi ni kama injini za kutafuta kura ili kuhakikisha ushindi wa kuinusuru Zanzibar. Tumejipanga vizuri kila majimbo tuna watu wasiopungua 50,” amesema Ferej ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ACT Wazalendo.

Mbali na Ferej, Katibu wa Ngome ya Wazee, Janeth Fussi amesema kundi hilo linakwenda kila eneo kusaka kura zitakazomwakikishia ushindi wa kishindo wa OMO.

“Mheshimiwa mgombea (Othman) wazee wanakuelewa, ndio maana sasa hivi wapo mguu kwa mguu, watoto wa mjini wanasema ‘battle to batlle’ hadi katika masoko kusaka kura zako,”

“Wazee hawa wanatuambia wamechoka mwili, lakini akili na mawazo yapo kwako wakimaanisha watakupigia kura Oktoba 29. Ikifika Oktoba 29, watakaoweza kupiga wataenda vituoni, watakaoshindwa wametuambia tuwafuate tuwapeleke hata kama asubuhi sana,” amesema Fussi.

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo na mgombea urais wa Zanzibar, Othman amesema hatua ya uzinduzi wa timu hizo za ushindi ni mwendelezo wa safari ya chama hicho ya kushika dola ifikapo Oktoba 29.

“Sisi tuna kiu na njaa ya mabadiliko… niwaambie njaa yetu si tumbo bali ya dhamira ya mabadiliko kwa ajili ya mustakabali wa Wazanzibari. Tulifanye hili kwa imani na dhamira ya dhati, tunajua tunachokitafuta.

“Hili jambo rahisi, ngoma imeshalala wewe umeona wapi tajiri akaomba mchuzi nyumba ya jirani? Hili la kwetu pamoja tulichokifanya tuligawanya kwa ngome, yapo mazuri kwa vijana yaonekane, yapo mazuri kwa wanawake yaonekane, yapo mazuri kwa wazee yaonekane,” amesema Othman.

Othman ambaye ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, amesisitiza umoja kwa ngome hizo, katika utekelezaji wa majukumu ya kuhakikisha ushindi wa ACT Wazalendo ifikapo Oktoba 29.

“Nguvu yetu ndio umoja wetu, nguvu yetu ndio nidhamu yetu,” amesema Othman.
Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Zanzibar Ismail Jussa amesema hamasa na vuguvugu walizozionyesha wakati wa uzinduzi ziendeleee katika mitaa ili kuhakikisha ushindi wa Othman.

“Hizi hamasa na vuguvugu zisimame kuanzia leo, kuanzia dakika hii.Katika hili hakuna mashindano, bali tunakwenda kushirikiana vijana, wanawake na wazee kila mmoja ajifunze kwa mwenzake, si kulaumiana maana safari yetu ni moja,” amesema Jussa.