Dar es Salaam. Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, imetangaza kima cha chini cha mshahara wa sekta binafsi ambao utakuwa Sh358,322 kutoka Sh275,060, likiwa ongezeko la asilimia 33.4.
Kima hicho kitaanza kutumika rasmi Januari mosi, 2026. Ongezeko hilo limegusa sekta za kilimo, afya, mawasiliano, usafirishaji, hoteli, madini, biashara na viwanda.
Nyingine ni shule binafsi, huduma za ulinzi binafsi, nishati, uvuvi na huduma ya baharini, michezo na utamaduni pamoja na huduma nyingine.
Serikali ilipandisha kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1 (kutoka Sh370,000 hadi Sh500,000), lengo likielezwa ni kuimarisha ustawi kwa wafanyakazi.
Rais Samia Suluhu Hassan, alitangaza ongezeko hilo wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi), iliyoadhimishwa kitaifa mkoani Singida, Mei mwaka huu.
Akitangaza ongezeko la kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi leo Ijumaa Oktoba 17, 2025, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Ridhiwani Kikwete amesema ongezeko hilo ni takwa la kisheria.
Amesema tangazo la mara ya mwisho lilikuwa mwaka 2022, hivyo la leo mwaka 2025 ni baada ya miaka mitatu, ambayo inatakiwa kisheria kufanyika mapitio ya kima hicho.
“Nitoe rai kwa waajiri wote wa sekta binafsi kuzingatia na kutekeleza kima hiki kipya cha mshahara kwa kuwa ni takwa la kisheria. Ofisi yangu haitasita kuchukua hatua kwa waajiri watakaokaidi au kushindwa kitekeleza amri hii kwa makusudi,” amesema na kuongeza:
“Ofisi yangu itaendelea kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa amri hii, kutoa elimu kwa waajiri na wafanyakazi pamoja na kufanya tathmini ya mara kwa mara ili kuhakikisha utekelezaji wake unafanyika kikamilifu.”
Chama cha Waajiri Tanzania (ATE), kimesema amri hiyo ya kima cha chini cha mshahara inaendana na mchakato wa tathmini iliyofanyika ikihusisha Serikali, vyama vya wafanyakazi na waajiri.
Akizungumza kwenye mkutano wa Ridhiwani, Mtendaji Mkuu wa ATE, Suzanne Ndomba, amesema katika kipindi cha miezi iliyobakia kabla ya kuanza utekelezaji, waajiri waendelee kufanya mazungumzo katika kampuni zao kwa kuwa inaenda kubadilisha ulipaji mshahara.
“Sisi (ATE) tutaendelea kuzungumza na waajiri jinsi gani wanaweza kutekeleza amri hii ili wasije wakajikuta wanakumbwa na mkono wa sheria,” amesema.
Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Rehema Ludanga amesema:
“Kama mnakumbuka sekta ya umma kima chao kilishatangazwa, wafanyakazi sekta binafsi wao walikuwa wanatumia kima cha chini cha mwaka 2022,” amesema.
Amesema kima hicho kipya ni faraja na hatua kubwa, akiwaomba waajiri wote kuendana na kima hicho.
“Haimaanishi waajiri wanaolipa zaidi ya hivyo kwamba wapunguze, hapana bali tunaangalia uzalishaji wa eneo husika. Hiki ni kima cha chini, yaani cha kuanzia lakini mwajiri asilipe chini ya hapo, anaweza akaongeza kulingana na eneo lake la uzalishaji,” amesema.
Mwenyekiti wa Bodi ya kima cha chini cha mshahara sekta binafsi, Suleiman Rashid amesema umefanyika utafiti ndipo matokeo yake hayo yametangazwa.
“Ilifanyika utafiti kwa kuzingatia hali ya uchumi na uwezo wa kulipa huo mshahara, uwezekano wa kuajiri, uchumi wa nchi pamoja na mfumuko wa bei,” amesema.
Amesema zipo njia zinazotumiwa duniani kote ambazo zinaangaliwa kulingana na Shirika la Kazi Duniani (ILO), ambapo kima hicho kimeangaliwa kama kinaweza kulipwa bila kuathiri hali yoyote.
Christopher Makombe, mchambuzi wa uchumi amesema kuongezeka kwa kima cha chini cha mshahara kunatoa fursa ya kuboresha hali ya maisha ya wafanyakazi na kuongeza mzunguko wa fedha katika uchumi.
Amesema wafanyakazi wataongeza matumizi yao kutokana na nyongeza hiyo, jambo linalochochea ukuaji wa biashara na mapato ya Serikali kupitia kodi.
“Ongezeko hili linaweza kuongeza morali na tija kazini, kupunguza tofauti za kipato na kuimarisha ustawi wa maisha kwa ujumla. Ikiwa litasimamiwa vizuri, ongezeko hili linaweza kuwa kichocheo cha maendeleo endelevu na ustawi wa uchumi wa nchi,” amesema.
Amesema pamoja na nia njema ya kulinda masilahi ya wafanyakazi, ongezeko la kima cha chini cha mshahara linaweza kuleta changamoto kwa sekta binafsi, hasa biashara ndogo na za kati.
“Gharama kubwa za uendeshaji katika mishahara zinaweza kusababisha kupungua kwa ajira, kupandishwa kwa bei za bidhaa ili kufidia nyongeza,” amesema.
Mbali ya kima cha chini, mchumi Oscar Mkude, amesema jambo la muhimu ni ni wafanyakazi kupitia vyama vyao kufanya majadiliano ya mikataba ya hali bora ambayo ndiyo inaweza kuwalinda dhidi ya mishahara isiyokidhi maisha ya staha.
Akizungumza na Mwananchi mfanyakazi kutoka sekta binafsi, Kenneth Michael amesema ni habari njema ikilinganishwa na gharama ya maisha ya sasa.
“Natamani utekelezaji uanze hata kesho, nimefurahi. Nashukuru Serikali na wote waliohusika. Kwa fedha hiyo maana yake kwa siku mtu unalipwa zaidi ya Sh10,000 hivyo ni jambo jema,” amesema.