Mtaalamu asimulia alivyochunguza video ya Lissu kesi ya uhaini

Dar es Salaam. Shahidi wa tatu wa Jamhuri katika kesi ya uhaini  inayomkabili mwenyekiti wa Chama  cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amesimulia mahakamani namna alivyofanya uchunguzi wa picha mjongeo (video clip) inayomuonesha Lissu akitamka maneno yanayodaiwa kuwa ya uhaini.

Shahidi huyo ni Mkaguzi wa Jeshi Polisi, Samweli Eribariki Kaaya miaka (39), Mtaalamu wa Picha, kutoka kitengo cha Picha Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai. Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam.

Kitengo hicho kinajishughulisha na kupinga na kurekodi picha za mnato na za mjongeo za matukio ya uhalifu, watuhumiwa wa uhalifu na  kunafanya uchunguzi wa picha mjongeo, picha mnato, ambayo ndio majukumu yake.

Katika kesi hiyo Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini akidaiwa kutoa maneno ya kuitishia Serikali  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Anadaiwa kuwa  Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akitoa maneno ya kuitishia Serikali na kuonesha nia hiyo kwa kuchapisha maneno hayo katika mitandao ya kijamii kuwa:

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”.

Kesi hiyo inayosikilizwa na Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, mbele ya jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi  wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Katika ushahidi wake wa msingi (examination in chief) akiongozwa na mwendesha mashtaka Wakili wa Serikali Mwandamizi, Tawab Issa  shahidi huyo amesema  ndiye alipokea na kufanyia uchunguzi wa kisayansi video ya Lissu pamoja na mambo mengine ili kujiridhisha kama ni halisi au la.

Kwa mujibu wa maelezo yake katika ushahidi huo, Aprili 8, 2025 alipokea flash disk pamoja na kadi ya data (memory card) kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalumu, Dar es Salaam.

Pamoja na vihifadhi data hivyo pia alipokea barua mbili za maelekezo ya kazi ya kufanya, barua  moja ilikuwa inahusu kuchapisha taarifa za uwongo mtandaoni na ya pili ilikuwa inahusu uhaini, iliyokuwa na kumbukumbu namba DA.223/476/06B/169.

Barua hiyo ya uhaini  ilimhitaji kufanya mambo yafuatayo:

Mosi, chanzo cha picha mjongeo zinazopatikana kwenye flash dick hiyo,

Mbili, uthibitisho wa uhalisia wa maudhui kwenye  picha mjongeo iliyomo katika flash disk.

Tatu, chanzo cha picha iliyopo kwenye memory card.

Nne, uhalisi wa maudhui kwenye  picha mjongeo uliyopo katika memory Card.

Tano, ulinganisho wa maudhui wa picha mjongeo  iliyopo kwenye flash Disk na iliyopo katika memory Card.

Sita, kuchunguza maudhui yafuatayo (maneno  yanayodaiwa kuwa ya uhaini yaliyotajwa kwenye hati ya mashtaka kama yalivyonukuliwa hapo juu,   kama yanapatikana katika disk na hizo.

Uchunguzi wa awali na malengo yake

“Katika hatua hii tunafanya uchunguzi wa kutazama (physical examination). Hapa tunaangalia necessary or unnecessary movement of the things (vitu vinavyopita) kwa mfano nzi au mtu anapeleka MIC kwenye podium”, amesema shahidi Mkauzi Kaaya.

Pia,  wanatazama mwendelezo wa matukio lakini, uwepo wa kukatika kwa picha kwa maana ya Jumpshort, ambayo inanisaidia kung’ amua kama kuna kipande kilichokatwa au hakuna.

Pia, wanaangalia kama kuna mstari mshazari unanisaidia kutambua uhalisia wa picha uliopo kati ya object na lenzi ya kamera pamoja na  Continuity ambayo (mwendelezo wa maudhui/picha.

Kwa mujibu wake mambo hayo yote yanawezesha kujua kama picha husika ni hali au si halisi na kwamba nyumbuliko wa midomo (lips movement) zinaweza kuwa uhaini ikiwa mazungumzo anayozungumza mtu ni halisi au si halisi.

Uchunguzi na matokeo yake

Baada ya kufika maabara aliandaa vifaa vya kufanya uchunguzi, ambavyo ni pamoja na kompyuta kwa ajili ya kufungua na kuangalia data alizotakiwa kuzifanyia uchuguzi, printa kwa ajili ya kuprinti taarifa chunguzi na kuvifanyia uhakiki.

Kisha alihakiki programu endeshi (software) kwa kuwa ndizo zinazofanya  compyuta (hardware) kufanya kazi.

Amezitaja programu hizo kuwa ni window 11,  programu ya chunguzi ya  Foresic Software hizi zipo mbili ambazo ni  Amped Program inaongeza ubora wa kile kitu kinachofanyiwa uchunguzi na ya pili. inafanya utambuzi wa sura.

Programu nyingine aliyoihakiki ni programu ya ulinzi au usalama wa kompyuta iitwayo kaspesky Ant Virus.

Caspeskya ni Software ambayo kazi yake ni kulinda programu endeshi pamoja na programu zote zilizopo katika kompyuta na inalinda vielelezo ninavyoviweka visiliwe na virusi.

Kisha alisoma tena zile barua alizokabidhiwa ili kujua maelekezo ya kile alichotakiwa na mamlaka iliyoombwa uchunguzi kuifanya.

Baada ya kumaliza hatua hizo akianza rasmi kufanya uchunguzi huo wa awali, ambapo aliifungua video zote kwenye flashi baada ya kupata nywila kutoka mamlaka iliyoombwa uchunguzi na kwenye memory card moja baada ya nyingine baada ya kuiunganisha kwenye kompyuta yake  maalumu.

Kwenye flash disk alikuita picha mjongeo moja yenye kichwa cha habari ‘Tundu Lissu uso kwa uso na watia nia majambo, ni no reforms, no election njia panda’.

Video hiyo ilikuwa urefu wa saa 3:38 na ilikuwa katika mfumo wa MP4.

Ndani yake aliona maudhui kuwa: “

“Wanasema msimamo huu unaashiria uasi ni kweli kabisa maana tutazuia uchaguzi, hivyo tutazuia watu, hiyo ndio namna ya kupata mabadiliko, tunaenda kukinukisha sana uchaguzi huu tutauvuruga maana tunaenda kukinukisha vibaya sana.”

Hayo ndio maneno anayoshtakiwa nayo Lissu kuwa ni ya uhaini, shahidi huyo amesema  yalipatikana kwenye saa ya pili na dakika 58, kwenye flash.

Kwa upande wa memory card amesema kuwa alipoifungua alikuita kuna vipande 25 vya picha za video ilivyopekuliwa kwenye folder lililoandikwa stream imepewa namna kuanzia namba 6 mpaka 30 .

Kipande cha 28 ndicho lilikuwa na maudhui yaliyoko kwenye hati ya mashtaka na lilikuwa na urefu w dakika 8 sekunde 27.

Endelea kufuatilia sehemu ijayo kujua matokeo ya uchunguzi huo kujua kile shahidi huyo alichokibaini baada ya ripoti yake ya uchunguzi kupokewa.

Kesi hiyo imeahirishwa mpaka saa 9:30 kumwezesha shahidi kufuata kompyuta yake kwa ajili kuonesha na kutambua vielelezo hivyo alivyofanyia uchunguzi kabla ya kupokewa ripoti yake mahakamani kuwa kielelezo.