Serikali yaagiza wananchi kuwajibika kulinda misitu Makete

Iringa. Kutokana na ongezeko la matukio ya moto wa misitu na uharibifu wa rasilimali za asili nchini, Serikali imeelekeza kuimarishwa kwa elimu na uhamasishaji wa wananchi ili kuongeza ushiriki katika kulinda misitu, kudhibiti majanga ya moto na kuhamasisha uwekezaji endelevu katika sekta hiyo muhimu ya uchumi.

‎Akizungumza na Mwananchi Digital Oktoba 16, 2025, katika ukumbi wa mikutano wa Sunset, Manispaa ya Iringa, Mkuu wa Wilaya ya Makete mkoani Njombe, Kissa Gwakissa amesema wananchi wanapaswa kubadilika na kuchukua hatua za makusudi kulinda misitu dhidi ya moto na uharibifu unaotokana na shughuli za kibinadamu.

‎Amesema Serikali imeweka mikakati na sheria madhubuti katika ngazi za vijiji kuhakikisha kila mwananchi anawajibika katika kulinda misitu, ikiwa ni pamoja na kuweka adhabu kwa vitendo vinavyochochea moto kama uchomaji mashamba ovyo na uvutaji sigara misituni.

‎“Tunataka jamii iwe mstari wa mbele kulinda mazingira yao na hii ni mali yao, chanzo cha kipato na uhai wa vizazi vijavyo hivyo Serikali peke yake haiwezi kufanikiwa bila ushirikiano wa wananchi,” amesema Gwakissa.

‎Kupitia hilo DC Kissa amesema serikali imeweka sheria kali katika vijiji vya wilaya hiyo kudhibiti wachoma misitu, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kitaifa kuimarisha usimamizi endelevu wa misitu kupitia programu ya FORLAND Talk Show.

‎“Mfano katika kijiji cha Ibaga, mtu akikutwa na kipisi cha sigara hupewa adhabu ya kulipa shilingi 50,000 na hii imepunguza kwa kiasi kikubwa visa vya moto,” amesema DC Kissa  huku akisisitiza kuwa

‎”Elimu na ushirikiano kati ya serikali na wananchi ni silaha kuu ya kupambana na uharibifu wa misitu,”.

‎Ili kuweka mkazo katika suala hilo umefanyika uzinduzi wa mfululizo wa vipindi vya majadiliano ya kitaifa vilivyozinduliwa mkoani Iringa na Mradi wa Forestry, Land Use and Value Chains Development in Tanzania (FORLAND) , vinavyolenga kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kulinda misitu na kuhamasisha uwekezaji endelevu katika sekta hiyo.

‎Uzinduzi huo ni sehemu ya kampeni ya mawasiliano na mabadiliko ya kitabia (SBCC) inayolenga kuhimiza jamii kushiriki kikamilifu katika kulinda misitu, kuhimiza uwekezaji, na kuimarisha uthabiti wa mazingira dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

‎Mradi wa FORLAND unafadhiliwa kwa pamoja na Serikali ya Finland na Serikali ya Tanzania chini ya usimamizi wa Wizara ya Maliasili na Utalii (MNRT), ukiwa na lengo la kukuza sekta ya misitu endelevu na jumuishi, kuchochea uchumi wa taifa, kupunguza umaskini, na kulinda rasilimali za asili kwa manufaa ya vizazi vijavyo.

‎Akizungumza na Mwananchi Digital katika ukumbi wa Mtaalamu wa Mawasiliano wa Mradi wa FORLAND, Sheila Chatto amesema kupitia kipindi hicho wanataka jamii iwe sehemu ya suluhisho la uharibifu wa misitu.

‎“Kupitia mijadala hii tunalenga kuongeza uelewa, kubadili mitazamo, na kuvutia wawekezaji wapya katika mnyororo wa thamani wa sekta ya misitu,” amesema Sheila.

‎ Mshauri Mkuu wa Mradi wa FORLAND, Michael Hawkes amesisitiza kuwa jamii zenye uelewa na ushiriki mkubwa ndizo nguzo kuu za uendelevu wa mazingira.

‎“Tunataka kila mwananchi atambue kuwa misitu ni injini ya uchumi wa kijani na maisha bora,” amesema.

‎Aidha, FORLAND Talk Show imebeba mada isemayo “Kuzuia Moto, Kulinda Maisha ya Baadaye, Hatua za Jamii na Sera kwa Misitu Salama na Uwekezaji Endelevu,” amesema.

‎Mada hiyo imechaguliwa kutokana na changamoto kubwa ya moto wa misitu nchini, unaosababisha madhara makubwa kiuchumi na kimazingira.

‎Moto wa misitu umekuwa tishio linaloongezeka kila mwaka kutokana na shughuli za kibinadamu kama uchomaji mashamba, utayarishaji wa malisho, uchomaji mkaa na hata uvutaji sigara ovyo.

‎Imeelezwa kuwa athari zake ni kubwa  misitu kuungua, bayoanuai kupotea, mmomonyoko wa udongo, na upotevu wa mapato kwa jamii na serikali.

‎Katika mjadala huo, wataalamu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Ofisi ya Waziri Mkuu (Idara ya Usimamizi wa Maafa), Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Taasisi ya Utafiti wa Misitu (TAFORI), serikali za mitaa, wawekezaji na wakulima wadogo walishiriki kutoa uzoefu na mapendekezo.

‎Mjadala uliangazia umuhimu wa uratibu kati ya taasisi za serikali, sekta binafsi na jamii ili kupunguza matukio ya moto na kuongeza tija katika usimamizi wa misitu.

‎Mwenyekiti wa Kijiji cha Kidete wilayani Mufindi, Jestina Gidion amesema jamii yao imeunda kamati maalumu za kukabiliana na moto na kuweka sheria ndogo za kudhibiti uchomaji holela.

‎“Tulichambua maeneo yenye hatari, tukatunga sheria na tukaweka adhabu kali, na hivi sasa hatupati tena moto kama zamani,” amesema Jestina.

‎Afisa Misitu na Mkufunzi kutoka Chuo cha Mafunzo ya Misitu (FWITC), Chamba Pamba amesema elimu ya uzuiaji moto inapaswa kutolewa mara kwa mara kwa wananchi, hasa vijijini ambako moto mingi huanzia.

‎Mtaalamu wa Ufuatiliaji wa Moto wa Misitu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kekilia Kabalimu amesisitiza umuhimu wa kutumia teknolojia kama sensa za moto na ramani za anga kusaidia utambuzi wa mapema wa matukio ya moto kabla hayajaleta madhara makubwa.

Naye Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Iringa, Jacline Mtei ameeleza kuwa jeshi hilo limekuwa likishirikiana na jamii katika kutoa mafunzo ya kuzima moto na kuanzisha vikosi kazi vya dharura vijijini.

‎Aidha, Kamanda wa Kikosi cha Uzuiaji Moto kutoka Iboya, Ananias Lyanzile, amewataka wawekezaji katika sekta ya misitu kukatia bima mali zao na mashamba ya miti kama njia ya kujikinga na hasara zitokanazo na majanga ya moto.

‎Kwa upande wa serikali ya mkoa, Ofisa Misitu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Goliam Bahati amesema ipo haja ya viongozi wa vijiji na kata kutembelea maeneo yenye misitu mara kwa mara kujionea hali halisi na kusimamia sheria za mazingira.

‎Mtaalamu wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kutoka FORLAND, Andrew Ferdinands, alisema mpango huo wa majadiliano umelenga kuunganisha maarifa ya kitaalamu na uzoefu wa jamii ili kuunda sera bora na vitendo vya ulinzi wa misitu.

‎Kupitia majukwaa kama haya, mradi wa FORLAND unalenga pia kuhamasisha uwekezaji katika sekta ya misitu, ukitambua kuwa ni chanzo cha ajira, kipato, na nyenzo ya kupambana na mabadiliko ya tabianchi.

‎Mradi huo unahimiza ushiriki wa vijana, wanawake, na wajasiriamali wadogo na wa kati (MSMEs) katika shughuli za misitu kuanzia upandaji miti, uchakataji wa mazao ya misitu, hadi bidhaa za mbao zenye thamani kubwa.

‎Kwa mujibu wa maelezo ya mradi, FORLAND unatekelezwa katika mikoa minne ya kusini mwa Tanzania Iringa, Njombe, Ruvuma na Lindi, ambayo ina utajiri mkubwa wa misitu ya asili na mashamba ya miti.

‎Kupitia utekelezaji huo, FORLAND inapanua mafanikio ya miradi iliyotangulia ya Private Forestry Programme (PFP) na Forestry and Value Chains Development Programme (FORVAC), ikilenga kuhakikisha matokeo yake yanaendelea kudumu kwa muda mrefu.

‎Mradi huu unatoa mafunzo, msaada wa kitaalamu na kiufundi kwa wadau wa sekta ya misitu, wakiwemo wakulima wadogo, jamii zilizo na haki za kisheria za kutumia misitu, pamoja na taasisi za serikali za mitaa.

‎Mada kuu katika mijadala hii ni kuhakikisha misitu inakuwa sehemu ya ajenda ya maendeleo ya uchumi wa kijani na si suala la mazingira pekee.

‎Aidha, imeelezwa kuwa mijadala hiyo itaendelea kufanyika katika kanda zote nne za utekelezaji, ili kuhakikisha kila jamii inapata nafasi ya kujifunza, kutoa maoni, na kushiriki katika hatua za kulinda misitu.

‎FORLAND pia imeweka mkazo katika kuimarisha mnyororo wa thamani wa sekta ya misitu, kuanzia kwenye uzalishaji wa miche, upandaji miti, uchakataji wa mazao, hadi uuzaji wa bidhaa za mbao na zisizo za mbao (non-timber products).

‎Kupitia mafunzo na mijadala kama hii, mradi unalenga kujenga jamii zenye maarifa, zenye kujitegemea na zinazoheshimu mazingira, ili kuhakikisha rasilimali za misitu zinadumu kwa manufaa ya wote.

‎Viongozi wa serikali, wataalamu, na wadau wote walioshiriki mjadala wa Iringa wamepongeza jitihada za FORLAND, wakisema ni mfano wa ushirikiano wa kimataifa unaochochea mageuzi chanya katika sekta ya misitu Tanzania.

‎Kwa ujumla, mjadala huu umeonesha kuwa tatizo la moto wa misitu linaweza kudhibitiwa endapo jamii itashirikishwa ipasavyo, sheria zitazingatiwa, na teknolojia itatumika kikamilifu.

‎FORLAND, kupitia FORLAND Talk Show imedhihirisha kuwa elimu, ushirikiano, na ubunifu ni silaha muhimu katika kulinda misitu, kulinda maisha, na kujenga uchumi wa kijani unaostawi.