Shahidi Kaaya amedai hayo leo Oktoba 17, 2025 wakati akitoa ushahidi wake mbele ya jopo la majaji watatu, wakiongozwa na Jaji Dustan Ndunguru akisaidiana na Jaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.
Akiongozwa na wakili wa Serikali Mwandamizi Tawabu Issa kutoa ushahidi wake Kaaya amedai kuwa, alianza kazi baada ya kuandaa vifaa vyake maalum ikiwemo kompyuta ya uchunguzi, printer maalum na programu za Forensky Software na Linzi, ambapo baada ya kuhakikisha vifaa vyote viko katika hali nzuri na vimehuishwa, alianza kufanya kazi kwa mujibu wa maombi ya mamlaka husika.
Amedai kuwa, Mamlaka hiyo ilitoa barua mbili za maombi ya uchunguzi, moja ikihusu kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni na nyingine ikihusu tuhuma za uhaini.
Amedai barua hiyo ilimwelekeza kuchunguza chanzo cha picha mjongeo iliyoko kwenye Flash Disk na Memory Card, kubaini uhalisia wa maudhui na kulinganisha kama taarifa zilizomo katika vifaa hivyo zinafanana.
Katika uchunguzi wa awali, mtaalam huyo alibaini kuwa Flash Disk aliyoletewa ilikuwa imelindwa kwa nywila. Baada ya kuwasiliana na mamlaka iliyoleta vielelezo hivyo, alipatiwa nywila na kufanikiwa kuifungua, ambapo alikuta video moja yenye kichwa “Tundu Lissu uso kwa uso na Watia Nia majimboni – No Reforms No Election Njia Panda” yenye urefu wa saa tatu na dakika 38.
Alitazama video hiyo na kubaini maudhui yenye maneno “Msimamo huu unaashiria uasi ni kweli kabisa maana tutazuia uchaguzi hivyo tutahamasisha uasi, hiyo ndiyo njia pekee ya kupata mabadiliko, tunaenda kukinukisha sana sana uchaguzi huu tutauvuruga, maana tunakwenda kukinukisha vibaya sana.”
Baada ya hatua hiyo, alifanya uchunguzi wa kisayansi kwa kutumia teknolojia ya Clone Analysis kubaini kama video imepandikizwa sura au sauti na kubaini kuwa hakuna pandikizi lolote. Vilevile, kupitia Noise Analysis alibaini kuwa video hiyo ilirekodiwa mchana na mwanga pamoja na rangi zilikuwa halisi.
Uchunguzi zaidi ulibaini kuwa kamera iliyotumika kurekodi ni aina ya Sony HXR-NX100, jambo lililothibitisha kuwa video hiyo ni halisi na haijafanyiwa marekebisho.
Katika uchunguzi wa Memory Card yenye alama ya Aldeepo, ukubwa wa GB 32, rangi nyeupe na nyeusi, alibaini vipande 25 vya video vilivyohifadhiwa kwenye folda ya Stream, kuanzia kipande namba sita hadi 30, ambapo kipande namba 28 kilikuwa na maudhui yale yale kuhusu uasi wa kisiasa.
Aidha, mtaalam huyo alibaini kuwa video hiyo ilipakiwa pia kwenye mtandao wa YouTube kupitia akaunti ya Jambo TV ambayo ilionekana kuwa na watazamaji 52,406 na wafuasi milioni moja na elfu kumi, huku watu 578 wakionekana kuipenda.
Baada ya kukamilisha uchunguzi, mtaalam huyo aliandaa ripoti rasmi iliyosainiwa na Mnadhimu wa Maabara ya Uchunguzi, kugongwa mhuri wa Kamisheni na vielelezo vyote kuingizwa kwenye bahasha tofauti, zikapigwa mihuri na kutiwa sahihi. Vielelezo hivyo vilikabidhiwa kwa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ambapo Assistant Inspector Michael Gyumi ndiye aliyepokea rasmi Aprili 8.
Flash Disk hiyo ilikuwa aina ya Kioshia yenye ukubwa wa GB 8 na stika ya kijani iliyoandikwa DM, ikiwa imeambatanishwa na lebo PF 145, huku Memory Card ikiwa na alama X na video 25 zilizotumika kama ushahidi katika uchunguzi hu… kesi hiyo inaendelea Mahakama Kuu Masijala ndogo Dar-es-Salaam.