Ibada ya kitaifa ya kumuaga Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, marehemu Raila Amolo Odinga, imefanyika leo jijini Nairobi, ikiunganisha maelfu ya waombolezaji, viongozi wa kitaifa na wageni wa kimataifa waliokuja kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo mkongwe wa siasa.
Ibada hiyo imehudhuriwa na Rais wa Kenya William Ruto, Rais wa zamani Uhuru Kenyatta, Makamu wa Rais wa Tanzania Dkt. Philip Mpango aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, pamoja na viongozi wengine kutoka nchi mbalimbali za Afrika.
Katika hotuba yake ya kugusa moyo, Mjane wa marehemu, Mama Ida Odinga, alizungumzia safari yao ya ndoa ya zaidi ya miaka 50, akimkumbuka Raila kama mume, baba na kiongozi aliyejitoa kwa taifa lake.
“Safari yetu haikuwa rahisi, tulipitia mengi, lakini tulijifunza kuvumilia na kusamehe. Raila alikuwa mtu wa watu, mwenye moyo wa upendo na aliyepigania haki bila woga,” alisema Mama Ida kwa hisia.
Viongozi waliozungumza katika ibada hiyo walimtaja Raila kama nguzo ya demokrasia ya Kenya, mtu aliyetoa maisha yake kwa ajili ya kupigania uhuru, usawa na haki kwa wananchi wote.
Rais William Ruto alimuelezea Raila kama “mpinzani mwenye heshima na mzalendo wa kweli”, akiahidi kuwa serikali itahakikisha urithi wake wa kisiasa unaenziwa.
Mwili wa marehemu Raila utaendelea kuagwa kesho kabla ya kusafirishwa Bondo, Kaunti ya Siaya, ambako atazikwa nyumbani kwake siku ya Jumapili.