Hatari iliyopo balehe za mapema, kuchelewa kukoma hedhi

Dar es Salaam. Wataalamu bingwa wa magonjwa ya saratani nchini, wamesema wasichana wanaobalehe mapema (kabla ya miaka 12) wapo hatarini kupata saratani ya matiti, huku wakishauri hatua za kuchukua.

Vilevile, wameeleza na kuonya kuhusu tiba za urembo unaosaidia mwonekano mzuri wa ngozi au ujana kuwa huchochea saratani ya matiti.

Wameeleza hayo leo Ijumaa, Oktoba 17, 2025 kwa nyakati tofauti ikiwa ni mwendelezo wa uelimishaji wa jamii, katika mwezi wa uelewa juu ya saratani ya matiti.

Daktari bingwa mbobevu wa magonjwa ya saratani, Dominista Kombe amesema: “Kuzaliwa mwanamke, ni changamoto ya kwanza na kadri umri unavyoenda ndivyo hatari huongezeka. Lakini wale wanaobalehe kabla ya kutimiza umri wa miaka 12 wanakua hatarini zaidi.”

“Kuwalisha watoto vyakula vilivyokuzwa kwa dawa zenye vichocheo kwa mfano wanapika maini ya kuku broiler watoto wanakula, matokeo yake wanakuwa na estrogen nyingi wanabalehe kabla ya miaka 12,” amesema.

Ametaja kundi jingine ni wanawake waliochelewa kukoma hedhi mpaka kufikia umri wa miaka 52.

“Mwenye umri huu maana yake bado ana uzalishwaji wa estrogen (homoni ya kike), inachangia mama kuwa katika hatari ya kupata magonjwa, kichochezi hiki cha kike kikitumika muda mrefu si salama. Ili kuwa salama tunawashauri wanawake walioangukia katika changamoto hii kuhakikisha wanachunguza afya yao ya matiti mara kwa mara na uchunguzi wa kina hospitali kila mwaka,” amesema.

Akizungumzia tiba za urembo, amesema huchangia uzalishwaji mwingi wa vichocheo ambavyo husababisha saratani ya matiti.

“Hata kwa wataalamu wa afya ile tiba ya kubadilisha homoni jaribuni kutumia dozi ndogo na muda mfupi kadri iwezekanavyo. Kunapokuwa na tiba hii dozi yake ni ndogo na risk (hatari) yake ni ndogo pia, hii tiba therapia inachochea uwezekano wa kupata saratani ya matiti,” amesema alipokuwa akitoa mafunzo kwa wafanyakazi wa shirika lisilo la kiserikali la JHPIEGO Tanzania.

Dk Kombe (70) ambaye anashikilia rekodi ya kuwa daktari bingwa wa saratani wa kwanza mwanamke, amesema tafiti mbalimbali zimeonyesha kichocheo cha homoni za kike ndicho kinachosababisha saratani hiyo kwa kiasi kikubwa.

Akifafanua zaidi, Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Ocean Road, Caroline Swai amesema tiba nyingi za urembo si salama, akitoa angalizo kuwepo kwa kemikali hasi.

“Hatuna ushahidi bado ni kwa namna gani, lakini zipo za aina nyingi na zingine zimewekwa kemikali ambazo hata Shirika la Viwango Tanzania (TBS) walithibitisha si salama,” amesema.

Meneja huduma za uchunguzi katika Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dk Maghuwa Stephano amesema uwepo wa homoni ya kike kwa kiwango kikubwa kwa mwanamke kwenye maisha yake, ambayo inaendelea tu inaweza kusababisha saratani ya matiti.

Amesema ni muhimu wananchi kufika hospitali kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa saratani mara kwa mara kwani dalili ni uvimbe ambao unaweza kuwa kwenye titi au kwapa.

Pia, mwonekano wa titi kuwa na ukubwa au ngozi kuwa kama ganda la chungwa.

“Uvimbe usiouma, ziwa kuleta mabadiliko waweza kuona limepinda na ndivyo inavyoanza, ngozi ikawa kama ganda la chungwa, chuchu inatoka vitu, inaanza kama jipu,” amesema.