KUANZIA ndani ya Tanzania, Afrika hadi Ulaya, hii ni wikiendi ya shoo shoo.
Kuna shoo za kibabe zinapigwa kwenye viwanja tofauti kwa wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya kimataifa yanayosimamiwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) na Ulaya kuna shoo za maana kwenye EPL na Bundesliga.
Kwanza kuna vita ya ndugu wawili wa Tanzania, hii ni KMKM kutoka Zanzibar dhidi ya Azam ya Tanzania Bara ikiwa ni mechi ya Kombe la Shirikisho Afrika itakayochezwa kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuanzia saa 10:15 jioni.
Nyingine itakuwa Malawi ambako Yanga inashuka dimbani kuwania nafasi ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika ikikabiliana na Silver Strikers, kwenye Uwanja wa Bingu jijini Lilongwe kuanzia saa 10:00 jioni.
Na kule Ulaya, mabingwa wa Ujerumani, Bayern Munich watakuwa na mtihani wa kuwakabili wapinzani wao wa jadi, Borussia Dortmund kwenye Uwanja wa Allianz Arena kuanzia saa 1:30 usiku, wakati Jumapili hii mabingwa wa Ligi Kuu England, Liverpool watawaalika mahasimu wao wa kihistoria, Manchester United kwenye Uwanja wa Anfield kuanzia saa 12:30 jioni.
Wikiendi ya ‘Shoo Shoo’ itafungwa na mechi nyingine za kibabe, ambapa Simba ya Tanzania itakuwa ugenini eSwatini kuivaa Nsingizini Hotspurs katika Ligi ya Mabingwa Afrika kuanzia saa 10:00 jioni, muda ambao pia Singida Black Stars ya Tanzania itakuwa ugenini Burundi kuikabili Flambeu du Centre katika Kombe ka Shirikisho Afrika.
Ni mechi zenye mvuto mkubwa, kila timu ikiwa na malengo ya kuandika historia mpya kwenye soka la Afrika.
Azam na KMKM zote hazijawahi kucheza hatua ya makundi CAF licha ya ushiriki wao mara kadhaa, Yanga inaisaka hatua hiyo kwa msimu wa tatu mfululizo upande wa Ligi ya Mabingwa, lakini Silver Strikers, kufika hapa ni mafanikio makubwa, inahitaji kwenda mbali zaidi.

SILVER STRIKERS VS YANGA VITA IPO HAPA
Yanga ipo katika kiwango bora tangu kuanza kwa msimu huu. Haijapoteza mechi yoyote kwenye mashindano yote, imeshinda nne na sare moja. Safu yao ya ulinzi, ikiongozwa na Djigui Diarra golini na mabeki wa kati Ibrahim Bacca na Dickson Job ambao wamekuwa wakicheza sana, haijaruhusu bao hata moja. Katika suala la kucheka na nyavu, imefanya hivyo mara tisa.
Katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga iliiondoa Wiliete SC ya Angola kwa jumla ya mabao 5–0, ikishinda 3–0 ugenini na 2–0 nyumbani. Matokeo hayo yanaonyesha uhatari wa Yanga ulivyo.
Silver Strikers iliitoa Elgeco PLUS ya Madagascar kwa faida ya bao la ugenini. Hiyo ilitokana na ugenini kupata matokeo ya 1-1, nyumbani ikawa 0-0.
Ndani ya uwanja, tunaweza kushuhudia burudani kubwa eneo la katikati kutokana na Silver Strikers kutajwa kuwa imara hapo ikiwatumia zaidi nyota wake, Uchizi Vunga na Levison Maganizo.
Yanga nayo ipo vizuri hapo kati, Aziz Andabwile amewaka tangu kocha Romain Folz atue kikosini hapo. Pia kuna mtu kama Mohamed Doumbia, Balla Moussa Conte, Duke Abuya na Mudathir Yahya. Pia Pacome Zouzoua mwenye uwezo wa kutokea pembeni, kucheza nyuma ya mshambuliaji na kusaidia eneo la kati kwenye kiungo.
Kocha msaidizi wa Yanga, Patrick Mabedi, raia wa Malawi, anasema mechi dhidi ya Silver Strikers ni ya kipekee kwake kwani anarejea nchini humo akiwa anakwenda kupambana na timu na nyumbani kwao.
“Mechi hii ni muhimu sana, ninarudi nyumbani tunakwenda kucheza na Silver Strikers ambayo ni timu ya nyumbani. Tutafanya kile tunachoweza ili kufanya vizuri na kwenda hatua inayofuata,” alisema Mabedi.
Mabedi, ambaye kabla ya kujiunga na Yanga alikuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Malawi, alisema anawafahamu vizuri baadhi ya wachezaji wa Silver Strikers. Wengine aliwahi kuwafundisha katika timu ya taifa ya Malawi, wakiwamo vijana waliopandishwa kutoka kikosi cha chini ya miaka 20.
“Kucheza na timu yenye wachezaji unaowafahamu ni faida kubwa. Ninajua udhaifu na nguvu zao, lakini mwisho wa yote tunapaswa kupambana ili kupata matokeo mazuri,” aliongeza.
Kocha huyo mwenye leseni A ya CAF amesema licha ya Silver Strikers kuwa na matokeo yasiyoridhisha katika mechi tatu zilizopita ikiambulia sare mbili na kipigo kimoja, hawatakiwi kuidharau.
“Katika soka unaweza kuona timu inashindwa kupata matokeo mazuri, lakini inakuja kufanya vizuri dhidi ya timu kubwa. Yanga ni timu kubwa, hivyo wapinzani wetu watacheza kwa nguvu zaidi,” alisema Mabedi.
“Tunaamini tutapata matokeo mazuri. Wachezaji wako kwenye hali nzuri na morali ipo juu,” aliongeza.

Silver Strikers si wageni kwa Yanga. Rekodi zinaonyesha timu hizo zilikutana mwaka 1986 kwenye michuano ya Kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kagame Cup), ambapo Yanga ilishinda kwa mabao 3–1 jijini Dar es Salaam.
Silver Strikers inayofundishwa na Peter Mgangira, wachezaji wanaotegemewa ni Uchizi Vunga, Levison Maganizo, George Chikooka, Maxwell Paipi, Dan Sandukira, Nickson Mwase, Stanie Davie na Chinsisi Maonga.

Wakati Yanga ikiwa nchini Malawi, hapo Zanzibar Azam FC na KMKM wanakutana katika mechi inayobeba matumaini na rekodi mpya kila upande, ambayo pia inaihakikishia Tanzania mwakilishi mmoja kwenye hatua ya makundi ya michuano inayosimamiwa na CAF msimu huu.
Timu hizi zinafahamiana kwa karibu, kwani zimewahi kukutana mara kadhaa katika mechi za kirafiki na mashindano ya Kagame Cup. Mara ya mwisho zilikutana mwaka 2021, ambapo KMKM ilishinda mara mbili, 3–2 katika hatua ya makundi na 1–0 kwenye mechi ya kuwania nafasi ya tatu.

Tangu Azam kuanzishwa kwake mwaka 2004, haijawahi kufika hatua ya makundi ya michuano ya CAF licha ya kushiriki mara 10 katika mashindano hayo. Huu ni msimu wake wa 11 kushiriki, na ndoto yao ni kufanya kile ambacho hawajawahi kukifanya nayo ni kufuzu hatua ya makundi.
Katika raundi ya awali msimu huu, Azam iliitoa Al Merreikh Bentiu ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 4–0, ikishinda mechi zote mbili 2–0.
Wachezaji wanaobeba matumaini ya timu hiyo ni pamoja na Feisal Salum ‘Fei Toto’, Jephte Kitambala, Issa Fofana, Baraket Hmidi, na Lusajo Mwaikenda.
Kwa upande wa KMKM, inaingia ikiwa na hamasa kubwa baada ya kuiondoa AS Ports ya Djibouti kwa jumla ya mabao 4–2. Inaongozwa na kocha Hababuu Ali Omar na nyota wao Nassor ‘Cholo’ Abdullah, Ahmed Is-haka, Mohammed Hassan, na Jumah Khalfan.
“Tunaiheshimu Azam, lakini hatuiogopi. Tutapambana kuhakikisha tunapata matokeo mazuri nyumbani kabla ya kurudi Dar es Salaam kwa marudiano,” alisema Hababuu.
Kocha wa Azam, Florent Ibenge, anasema kikosi chake kipo tayari kupambana.
“Nimewaambia wachezaji wangu hakuna mchezo rahisi katika CAF. Kila timu iliyo hapa ina ubora. Tusipokuwa makini, tutajikuta tukipoteza nafasi,” alisema Ibengé.
Kocha huyo kutoka DR Congo ni mmoja wa makocha wenye mafanikio makubwa barani Afrika, akiwa amewahi kubeba taji la michuano hii akiwa na RS Berkane.

Kwa miaka yote ya ushiriki wake katika mashindano ya CAF, Azam imekuwa na safari yenye milima na mabonde. Ilianza kushiriki mwaka 2013, ikaishia hatua ya awali.
Timu hiyo imeshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika mara mbili, 2015 na 2024-2025. Mara zote imeishia hatua ya awali.
Kwa upande wa Kombe la Shirikisho Afrika, angalau imewahi kufika hatua ya pili, lakini makundi, imekuwa hadithi isiyoisha simulizi kutokana na kutofika huko.
Kombe la Shirikisho Afrika
Matokeo: Azam 8–1 El Nasir (hatua ya awali)
Barrack Young Controllers 1–2 Azam (hatua ya kwanza)
Matokeo: Azam 1–2 Ferroviário da Beira (hatua ya awali)
Matokeo: Bidvest Wits 3–7 Azam (hatua ya kwanza)
Azam 2–4 Espérance (hatua ya pili)
Matokeo: Azam 1–3 Mbabane Swallows (hatua ya kwanza)
Matokeo: Fasil Kenema 2–3 Azam (hatua ya awali)
Azam 0–2 Triangle United (hatua ya kwanza)
Matokeo: Azam 4–1 Horseed (hatua ya kwanza)
Azam 0–1 Pyramids (hatua ya pili)
Matokeo: Al Akhdar 3–2 Azam (hatua ya pili)
Matokeo: Bahir Dar Kenema 3–3 Azam (penalti 4–3) hatua ya kwanza
Matokeo: Azam 2–3 Al-Merrikh (hatua ya awali)
Matokeo: Azam 1–2 APR (hatua ya kwanza)
Silver Strikers vs Yanga Saa 10:00 jioni, Uwanja wa Bingu, Lilongwe
KMKM vs Azam Saa 10:15 jioni, Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar