Moshi. Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha Sauti ya Umma (SAU), Majalio Kyara ameishutumu Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa kile alichokiita changamoto za uratibu wa ratiba za kampeni, hali ambayo amesema imekuwa ikisababisha mkanganyiko na migongano katika maeneo ya mikutano.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa, Oktoba 17, 2025, mjini Moshi, Kyara amesema katika kipindi hiki cha kuelekea ukomo wa kampeni, inahitajika umakini mkubwa zaidi ili kulinda amani na utulivu wa taifa.
“Tumeanza kampeni zetu jana mkoani Kilimanjaro, ambapo ratiba inaonyesha tulikuwa na mikutano Siha na Machame. Kwa hali ya kawaida, Siha ni wilaya tofauti na Machame ambayo ipo Wilaya ya Hai. Hata hivyo, kwa busara za viongozi wetu tuliweza kulitatua na kufanya mikutano yote kwa amani,” amesema Kyara.
Amesema hali ilikuwa mbaya zaidi leo baada ya kufika katika eneo la Kisomachi, Jimbo la Vunjo, Wilaya ya Moshi, ambapo walikuta chama kingine kikiwa na mkutano wa ubunge katika eneo hilo hilo.
“Tulizungumza nao kwa busara, wakaeleza hawakuwa wamepokea taarifa. Tuliwaomba tuwasalimie wananchi kisha tuendelee na ratiba yetu. Walikubali, lakini tulipoanza kuzungumza walikuja watu kutushambulia na kufungua muziki kwa sauti kubwa, hali iliyosababisha taharuki,” amesema Kyara.
Amesema kwa msaada wa vyombo vya usalama waliweza kuondoka salama, lakini akaomba INEC kuwa makini zaidi katika uratibu wa kampeni hasa kipindi hiki cha kuelekea ukomo wake.
“Niwaombe sana wenzetu wa Tume ya Uchaguzi, hususani kamati ya ratiba. Tunapoelekea mwisho wa kampeni, ni kipindi muhimu kuliko tulikotoka. Changamoto tunazokutana nazo ni kubwa, tunavumilia, lakini wakati mwingine tunashindwa, ndiyo maana tumewaomba waandishi wa habari mtufikishie ujumbe huu kwa Tume,” amesema.
Kyara ameiomba INEC pia kuweka wazi namba za mawasiliano zinazofanya kazi vizuri, ili kurahisisha mawasiliano pindi changamoto kama hizo zinapojitokeza.
Aidha, alitumia nafasi hiyo kumshukuru Mungu kwa kampeni zao kuendelea kwa amani na utulivu, akiahidi kwamba chama chake kitaendelea kuhubiri amani kama nguzo kuu ya uongozi wake endapo watapewa ridhaa ya kuunda Serikali.
“Tunaamini kupitia amani, sisi Sauti ya Umma tutakaposhika dola, tutaijenga Tanzania bora yenye umoja na maendeleo,” amesema Kyara.
Akijibu malalamiko hayo, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Vunjo na Moshi Vijijini, Lucas Msele, amethibitisha kupokea taarifa hizo, lakini akasema kwa mujibu wa ratiba rasmi ya INEC, mgombea huyo hakuwa na mkutano wa kampeni katika Jimbo la Vunjo siku ya leo.
“Ni kweli nimepokea malalamiko ya mgombea urais kupitia chama cha SAU, lakini kwa mujibu wa ratiba, leo Oktoba 17 alikuwa na mikutano katika Jimbo la Moshi Mjini, siyo Vunjo,” amesema Msele.
Amefafanua kuwa Wilaya ya Moshi ina majimbo matatu ya uchaguzi Moshi Mjini, Moshi Vijijini na Vunjo na kwamba kwa ratiba ya Tume, mgombea huyo anatarajiwa kuwa na mkutano Vunjo kesho, Oktoba 18, katika eneo la Marangu.
“Huenda kulikuwa na mkanganyiko katika usomaji wa ratiba. Ni vyema wagombea na viongozi wa vyama kuhakikisha wanaisoma na kuielewa vizuri kabla ya kuelekea kwenye mikutano,” amesema Msele.
Ametoa wito kwa vyama vya siasa kuwasiliana na Tume mapema endapo kutakuwa na changamoto yoyote ya ratiba, ili kudumisha amani katika maeneo ya mikutano.
“Niendelee kutoa wito kwa viongozi wa vyama na wagombea kuisoma ratiba vizuri, na kama kuna tatizo, tuwasiliane kabla ya kwenda eneo la mkutano ili kuepusha migongano na vurugu,” amesema.