Dar/Kibaha. Ulikuwa usiku wa kawaida kwa vijana wanne marafiki walioishi nyumba moja, wakiwa katika chumba cha mmoja wao wakipiga soga.
Madereva hawa watatu wa pikipiki maarufu bodaboda na mwezao anayeendesha bajaji, baada ya kazi ya kutwa nzima, walikuwa wakisubiri mke wa mwenzao awaandalie chakula.
Ghafla lilitokea jambo lililobadili furaha ya usiku huo, pale mlango ulipogongwa na ulipofunguliwa mwanaume mwenye silaha aliyeficha uso aliingia ndani akifuatiwa na wengine wawili walioficha nyuso kwa kofia, mmoja akiwa na pingu mkononi, kisha vijana hao kuchukuliwa.

Tukio hili liliishia kwa kutolewa taarifa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani, Oktoba 16, 2025 kuwa miili ya vijana wanne imeokotwa pembeni mwa barabara mkoani Pwani.
Taarifa hiyo imesema Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa serikali ya Mtaa wa Kidimu kwamba, maeneo ya Kidimu- Vingunguti, wilayani Kibaha, mkoani humo imeonekana miili ya watu wanne wasiojulikana, ikiwa pembezoni mwa barabara inayotoka Mapinga kuelekea Kibaha.
Taarifa hiyo imesema wataalamu wa uchunguzi wa matukio makubwa walifika eneo la tukio na kukuta miili hiyo ya wanaume wanaokadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 19 hadi 22, ambao hawakufahamika majina wala makazi yao wakiwa na majeraha usoni na miguuni.
Miili hiyo ilipelekwa katika Hospitali ya Rufaa ya Tumbi kwa uchunguzi zaidi. Ikiwa huko na uchunguzi ukiendelea kubaini nini kilichowatokea, ndipo wakajitokeza wazazi na baadhi ya ndugu wakaitambua miili ya watu hao.
Waliotambuliwa ni Mikidadi Abbas Mikidadi (21) na Hassan Juma Jumanne (21), waliotajwa kuwa ni madereva wa bodaboda (deiwaka), wakazi wa Tabata Chang’ombe, Dar es Salaam.
Wengine ni Fadhili Patrick Hiyola (19), dereva wa bodaboda (deiwaka), mkazi wa Vingunguti Miembeni, Dar es Salaam na Abdalla Fadhil Nyanga (21), ambaye ni dereva wa bajaji, mkazi wa Kisukuru Tabata, Dar es Salaam.
Jeshi la Polisi lilieleza kuwa miili yote ilishakabidhiwa kwa wazazi na ndugu kwa ajili ya mazishi, baada ya taratibu za uchunguzi wa daktari kukamilika, huku ukiendelea uchunguzi wa kina kubaini wahusika wa mauaji hayo na yalitokea wapi.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limetoa wito liwataka wananchi kama kuna mwenye taarifa yoyote ya kuwezesha kupata ukweli wa vifo hivyo aziwasilishe ili zifanyiwe kazi.
Kufuatiwa tukio hilo, kwa nyakati tofauti jana Oktoba 16, 2025, Mwananchi limezungumza na wazazi wa Hassan Jumanne na Abdalla Nyanga maarufu Dulla ambao wameeleza wanayoyajua kuhusu tukio hilo.
Dulla alizikwa jana Oktoba 16 saa 10:00 jioni wakati Mikidadi Mikidadi na Fadhili Hiyola walizikwa Oktoba 15, 2025.
Mwili wa Hassan umeagwa leo Oktoba 17, 2025 katika Hospitali ya Amana na maziko yanatarajiwa kufanyika kesho Jumamosi Oktoba 18, Same, mkoani Kilimanjaro.
Hadija Mmbaga, mama wa Hassan Jumanne, anasimulia kuwa asubuhi ya Oktoba 14, mmoja wa waendesha bodaboda alimuliza iwapo ana taarifa ya kuchukuliwa kwa mwanaye.
“Nilipokea simu na kuulizwa kama nina taarifa za Hassan kuchukuliwa, nilijibu hapana. Ndipo nilipoelezewa kuwa yeye na wenzake watatu wamechukuliwa usiku wa kuamkia siku hiyo,” amesema.
Amesema baada ya taarifa hiyo aliwasiliana na wazazi wengine kuhusu tukio hilo, wakakubaliana kwenda vituo vya polisi na hospitalini lakini hawakuwapata chochote.
Hadija amesema jioni ya siku hiyo alipokea simu kutoka kwa mzazi mwingine akamuarifu kuwa amepigiwa simu na namba ngeni, akaelezwa kuna miili imeokotwa Kibaha na imepelekwa Hospitali ya Tumbi.
“Ikabidi wanaume waende hospitali, walipofika walionyeshwa miili iliyookotwa na waliitambua kuwa ni ya watoto wetu. Walikuwa wameumizwa na ni wazi walipigwa,” amesema.
Hadija anasema vijana hao wamekuwa wakiishi nyumba moja kwa kuwa ni marafiki.
Akinukuu maelezo ya mke wa marehemu Abdallah, amesema tukio hilo lilitokea saa saba usiku na kwamba, vijana hao wakitoka kwenye shughuli zao walikuwa na kawaida ya kukaa pamoja chumbani kwa Dulla na kupiga stori, kwani wanaedesha vyombo vyao vya moto maeneo tofauti.
“Yule binti (mke wa Dulla) anasema kwa kuwa wana kawaida ya kukaa pamoja, hata kula wamekuwa wanakula wote, hivyo walimwambia awawekee chakula, huku kijana mwingine nje ya wale wanne akienda kufuata chakula kingine,” ameeleza Hadija.
Anaeleza baada ya muda walisikia mlango ukigongwa wakaamini aliyetoka amerudi, hivyo mwanamke (mkewe Dulla) alikwenda kufungua mlango, lakini haikuwa matarajio ya macho yake, alikutana na mwanamume aliyeshika silaha akiwa ameficha uso, akamwamuru arudi nyuma bila kupiga kelele.
Alitii na hapo hapo akashuhudia wengine wawili wakiingia ndani wakiwa wamefunika nyuso zao kwa kofia nyeusi, mmoja akiwa ameshika pingu. Idadi ya watu hao ikawa watatu.
Hadija anasema mmoja alirudi nje, ndani wakabaki wawili, mwenye silaha na aliye na pingu. Anaeleza vijana hao wanne walikusanywa pamoja wakafungwa pingu na macho kwa kutumia nguo zao. Waliamuru wanawake waliokuwapo kujifunika kwa shuka hadi walipoondoka.
“Alieleza jambo hilo lilikuwa la muda mfupi, kwani kijana aliyekwenda kufuata chakula aliporudi na kuuliza walipo wenzake, aliambiwa wamechukuliwa na watu wakiwa na silaha na kuondoka nao bila kueleza wanakwenda nao wapi,” anasema na kuongeza:
“Kutokana na maelezo ya mashuhuda ya uwepo wa silaha na pingu, tukaamua kwenda polisi lakini hatukuambulia kitu na matokeo yake tunapewa maiti.”
Hadija anasema kabla ya tukio hilo, walielezwa na mtu mmoja kuwa siku moja kabla ya tukio (Oktoba 13) kulikuwa na mzozo kati ya vijana hao na mwenzao mmoja, uliosababisha kurushiana chupa iliyomjeruhi huyo mwenzao.
“Wanasema baada ya mzozo, mzazi wa huyo kijana alikwenda kwenye nyumba wanayoishi vijana hao na kuwatishia kuwa atawapoteza na wazazi wao wakose dhamana ya kuwatoa kutokana na majeraha waliyosababisha kwa kijana wake. Cha ajabu siku iliyofuata vijana wetu wamepotea kweli na tumepata maiti,” anasema.
Anaeleza mzazi huyo alipoulizwa kijana wake ameumia kwa ukubwa gani na ametumia fedha kiasi gani kwa matibabu ili alipwe, alitaja Sh25, 000 kisha akalipwa.
Said Mikidadi, kaka wa marehemu Mikidadi akizungumzia tukio linalohusishwa na mauaji ya vijana hao amesema ulikuwa ugomvi wa vijana ambao ulimuhusisha Dulla na kijana wa mtaani kwao Kisukuru.
“Tunaweza kusema ni ugomvi wa vijana, ulisababisha mzazi wa yule kijana kwenda kwa kina Dulla kwa kueleza kumfanyia kitu kibaya kijana wao kwa kumjeruhi mtoto wake,” amesema.
Amesema baada ya malalamiko hayo wazazi walimwomba radhi na kutaka kujua nini tatizo na hata kumlipa ili kuepukana na jambo hilo alilosema angempoteza na wazazi wangeenda popote kulalamikia dhamana.
Said amesema waliona jambo hilo limemalizika, lakini baada ya siku chache wakaelezwa vijana wamechukuliwa na watu wasiojulikana.

“Wakati wanahangaika polisi ndugu yake Dulla aliwakumbusha tukio la mzazi aliyekuja kutoa onyo kwao, hivyo wazazi walikusanyana na kwenda kwa yule mzazi ambaye kijana wake alipigwa na kumuomba awaeleze watoto wao wapo kituo gani, ili wakahangaikie dhamana lakini jibu la yule mzazi alisema ahusiki na chochote,” amesema na kuongeza:
“Hata kama hakufanya yeye kauli yake ya awali inatuambia anahusika ndiyo maana wazazi wetu walimfuata kumuomba aonyeshe walipo watoto wao lakini alisema hajui na kusababisha mzozo hadi pale ilipotoka taarifa ya kupatikana kwa miili yao.”
Kwa upande wake, Mohamed Abdallah baba mkubwa wa marehemu Abdallah Nyanga, ambaye ndiye msemaji wa familia, amesema taarifa za kuchukuliwa kwa kijana wao walielezwa na mkewe, aliyewasimulia tukio zima lilivyotokea.
“Kijana wetu tunavyomfahamu hakuwa na makuu, siyo mwizi na wala si mkorofi. Hadi muda huu hatujui tuseme nini, tulijua amechukuliwa na polisi lakini tulizunguka vituo vyote tukaambiwa hawapo, mwishowe tunapata taarifa za kifo chake,” amesema.
Anasema miili ya vijana hao ilikuwa na majeraha ya kupigwa, alama za kamba shingoni na ni kama waliwekwa matambara mdomoni ili wasipige kelele.
Anasimulia kuwa, kijana wao aliondoka nyumbani kwao Tabata Chang’ombe na kwenda kupanga Kisukuru ambako marafiki zake waliungana naye huko.
Abdallah anasema vijana hao waliishi kama ndugu wa karibu, huku rafiki yao Fadhili Hiyola akiwatembelea mara kwa mara.
Amesema Dulla ameacha mke na mtoto mmoja wa mwaka mmoja na miezi minane.
Dereva wa bodaboda, Abdul Twaha, amesema tukio la kuchukuliwa vijana hao na kuuawa limewaogopesha.
“Kwa sasa tunaishi kwa mashaka kwa sababu hatujui nani anafuata kesho, tunawafahamu hawa vijana hawana vitu vya ajabu,” amesema.
Dionis Charwa, Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kidimu, Kibaha mkoani Pwani, ameeleza kuwa alfajiri ya Oktoba 14, 2025 alipokea simu kutoka kwa mwananchi akamjulisha kuhusu kupatikana miili ya vijana wanne, pembezoni mwa mtaro wa barabara kuu ya kutoka Bagamoyo kuelekea Kibaha.
Akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa, Oktoba 17, 2025, Charwa amesema alipofika eneo la tukio alikuta umati wa wananchi wenye taharuki. Miili mitatu ilikuwa pamoja na mmoja ukiwa pembeni.
Anasema miili hiyo ilikuwa na nguo na eneo la tukio hapakuwa na dalili za kuonyesha dalili za mapambano wala damu, jambo linaloashiria kwamba huenda waliuawa kwingine kisha wakatupwa hapo.
“Ni wazi kabisa hawa vijana waliuawa sehemu nyingine. Hakukuwa na dalili za vurugu eneo lile, jambo linalotia hofu kubwa kwa wakazi wa Kidimu,” amesema.
Charwa amesema baada ya tukio hilo, hofu imetanda kwa wananchi kutokana na mauaji hayo ambayo yameibua kumbukumbu za matukio kama hayo yaliyowahi kuripotiwa miaka iliyopita katika eneo hilohilo.
Mkazi wa mtaa huo, James Mgaya, amesema alishuhudia miili hiyo alipokuwa akielekea kazini alfajiri ya siku ya tukio.
“Nilikuwa naenda kazini, kufika eneo hilo nikaona miili ya vijana pembezoni mwa barabara. Kwa kweli nilishtuka na nikapata hofu sana,” amesema.
Amesema miaka ya nyuma eneo hilo lilikuwa likishuhudia matukio ya aina hiyo, kabla ya hali kutulia kwa muda mrefu.

“Hapo zamani kulikuwa na nyumba za wananchi ambazo zilivunjwa na Serikali kwa kuwa zilikuwa kwenye eneo la hifadhi ya barabara. Baada ya hapo eneo likabaki pori, na sasa matukio kama haya yameanza kurudi,” amesema.
Mkazi mwingine wa Kibaha, Christina Mwaluko, ameiomba Serikali kuweka mikakati ya kuyatumia mapori yaliyopo jirani na makazi ya watu ili kuzuia wahalifu kujificha humo.
“Ni muhimu Serikali ikayatumia maeneo hayo kwa shughuli za maendeleo ili kuondoa mazingira hatarishi kama haya,” amesema.