Nairobi. Shirika la kimataifa la Article 19, Afrika ya Mashariki, limeahidi kushirikiana na Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Tanzania (Jowuta) katika kuwajengea uwezo wanahabari kwenye masuala ya utetezi wa sheria za habari, haki za wanahabari na ukatili dhidi ya wanahabari wanawake.
Makubaliano ya ushirikiano huo yamefanyika leo Oktoba 18, 2025 jijini Nairobi, Kenya baina ya Jowuta na Article 19, mara baada ya mkutano wa taasisi za vyombo vya habari katika nchi za Afrika ya Mashariki, kujadili masuala ya uhuru wa vyombo vya habari, ushirikiano na utetezi wa wanahabari.
Akizungumza na Mwenyekiti wa Jowuta, Mussa Juma, Naibu Mkurugenzi wa Article 19, Patrick Mutahi amesema taasisi hiyo inatambua changamato za sekta ya habari katika nchi za Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania na itafanya kazi na Jowuta.
Mutahi amesema kutokana na changamoto hizo, Article 19 kwa kushirikiana na wahisani wake ikiwepo Jumuiya ya Madola (Commonwealth), itakuwa na mradi wa kusaidia sekta ya habari katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda.
“Tumepata faraja kukutana katika mkutano huu kujadili changamoto za masuala ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa vyombo vya habari katika nchi za Afrika Mashariki na kuona ni jinsi gani tunaweza kushirikiana kukabiliana na changamoto hizi,” amesema.
Mutahi amesema Article 19 itatoa usaidizi kwa Jowuta katika uketelezaji wa miradi ya kusaidia wanahabari ili kuhakikisha wanahabari wanafanya kazi katika mazingira ya uhuru na kutokuwa na changamoto nyingi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jowuta, Juma, amemhakikishia m,kurugenzi huyo kuwa Jowuta ni chombo cha wanataaluma wa habari ambacho kina uwezo wa kutekeleza miradi ya ushirikiano na Article 19 na taasisi nyingine.
Amesema Jowuta ambayo ina wanachama zaidi ya 400 katika mikoa yote nchini Tanzania, inahitaji ushirikiano kuwasaidia wanahabari kufanya kazi katika mazingira bora, kuwajengea uwezo wa kiuchumi na kushiriki katika majadiliano na waajiri katika kupata hali bora kazini.
“Tuna imani ushirikiano baina ya Article 19 na Jowuta utakuwa na manufaa makubwa kwa wanahabari nchini, ikiwemo kubadilishana uzoefu na wanahabari katika nchi nyingine ili kuhakikisha wanafanyakazi katika mazingira mazuri,” amesema.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Programu na Mafunzo wa Chama cha Waandishi wa Kujitegemea nchini Kenya (KCA), Willian Oloo-Janak amesema changamoto za sekta ya habari katika nchi za Afrika Mashariki kwa kiasi kikubwa zinafanana.
Amesema ili kukabiliana na changamoto hizo, ni muhimu kushirikiana ikiwemo kufanya kazi pamoja na taasisi za kikanda ikiwepo Jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC) na nyinginezo.
Katika mkutano huo, vyama vya wanahabari Afrika Mashariki, vilikubaliana kufanya kazi kwa ushirikiano, kubadilishana uzoefu, kuwa na mkakati wa pamoja kufanya utetezi wa kupata sheria nzuri za habari, kuwa na sera rafiki ikiwepo ya hali bora za wanahabari na masuala ya kupinga ukatili dhidi ya wanahabari wanawake .
Vyama vingine vilivyoshiriki mkutano huo ni Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Chama cha Waandishi wa Habari nchini Rwanda na Chama cha Waandishi wa Habari wa Kujitegemea Kenya.
Vingine ni Chama cha Wafanyakazi katika Vyombo vya Habari Kenya, Taasisi ya Wanahabari wa Mashinani Kenya, Wanahabari Uganda na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Uganda.