Siri usizopaswa kumueleza mwenza wako

Mwanza. Katika maisha ya ndoa, ukweli na uwazi ni nguzo muhimu za kudumisha uhusiano wenye afya na mafanikio.

Hata hivyo, kuna baadhi ya mambo ambayo kwa busara na hekima mtu hafai kumwambia mwenza wake.

Hii haimaanishi kusema uongo, bali ni kuchagua kwa tahadhari kile kinachosemwa ili kulinda amani, heshima, na uhusiano mzima wa kindoa.

Makala haya yanajadili baadhi ya siri ambazo si busara kumweleza mwenza wako, hasa kwa wale walio tayari katika ndoa, na kueleza athari ambazo siri hizo zinaweza kuwa nazo katika maisha ya ndoa.

Ingawa ni muhimu kumjulisha mwenza kuwa uliwahi kuwa kwenye uhusiano mwingine, si lazima kueleza kwa kina kuhusu kila kitu kilichotokea.

Mambo kama idadi ya wapenzi wa zamani, makosa yao, au hata mafanikio ya uhusiano huo, yanaweza kusababisha wivu, mashaka au hata hali ya kujilinganisha.

Mainda Japhet anaeleza kilichomkuta baada ya kumsimulia mumewe kuhusu sababu zilizomfanya aachane na mwenza wake wa zamani.

Anasema japo lengo la kumueleza lilikuwa kumtahadharisha mumewe vitu asivyovipenda katika uhusiano wao wa ndoa, mume wake alichukulia tofauti na kuanza kushuku uhusiano wa mke na mwenza huyo wa zamani.

“Nilimwambia sababu kubwa iliyofanya niachane na X wangu ambaye ndiye alikuwa mwanaume wangu wa kwanza ni tabia yake ya kuwa na mazoea ya kupitiliza na wanawake wengine. Inafikia hatua hata wakipigiana simu namna wanavyoongea ni kama uhusiano wao wa kazini umevuka mipaka,”anasema Mainda.

Anasema mumewe aliona sababu hiyo ya kawaida, hasa alivyomwambia yule mwanaume aliyeachana naye alikuwa mwanaume wake wa kwanza, hivyo alianza kuwa na wasiwasi kwakuwa aliamini mwanamke humpenda mwanaume wake wa kwanza kuliko wengine.

“Mara kwa mara alikuwa ananiuliza, fulani huwasiliani naye…hamjakutana, yaani maswali ambayo yalinionesha kuwa yupo insecurity (hana imani nami),”anaeleza.

 Maoni hasi kutoka kwa familia au marafiki

Wakati mwingine, familia au marafiki huweza kutoa maoni mabaya kuhusu mwenza wako. Maoni haya yakifikishwa kwake, huweza kuharibu uhusiano kati ya mwenza na familia au marafiki zako.

Mwanasaikolojia anayefanya shughuli zake mkoani Simiyu, Maduhu Nyadwera anasema kuwa kumweleza mwenza maoni hasi kutoka kwa familia au marafiki, kunaweza kuathiri vibaya uhusiano kwa njia kadhaa ikiwemo kumpunguzia mwenza kujiamini na kuhisi hana thamani machoni pa familia, marafiki jambo linalomfanya ajione duni.

“Kujenga chuki na umbali wa kihisia..anaweza kuanza kuona familia au marafiki zako kama wapinzani, hivyo kuleta mgawanyiko kati yenu..kuchochea migogoro isiyo na msingi kwakuwa maneno hayo yakirudiwa mara kwa mara, yanaweza kuzua mashaka na mabishano yasiyoisha,”anasema.

Anasema athari nyingine ni kupoteza uaminifu kwakuwa mwenza anaweza kuanza kuhisi kuwa mwenzake anashirikiana zaidi na watu wa nje kuliko yeye katika mambo ya uhusiano.

“Kwa ufupi, maoni hasi kutoka nje yanapopelekwa moja kwa moja kwa mwenza bila kuchujwa, huua amani, heshima, na kuaminiana katika ndoa,”anaongeza.

Siri zako binafsi ambazo hazina madhara katika ndoa

Kila mtu ana maisha ya ndani, ndoto, mawazo au hofu.Si kila jambo la ndani linapaswa kusemwa, hata kama halina athari yoyote katika ndoa. Hii ni pamoja na mawazo ya muda mfupi kama kuwahi kuvutiwa na fulani.

Mzee maarufu jijini Mwanza, Salim Boba anasema ni muhimu wana ndoa kuepuka kusema hata vitu vidogo vidogo mbele ya wenza wao, kwakuwa wakati mwingine hawajui namna ambavyo vitapokelewa.

Anasema kama binadamu hisia tofauti hazikosekani, lakini ni vizuri kuchunga ndimi kuropoka yale anayofikiria ili kuepusha migongano na migogoro kwenye ndoa.

“Mfano rafiki wa mke wako amekuja kumtembelea nyumbani kwenu. Na alivyovaa kapendeza kweli lakini mke wako yupo ovyo..usimwambie mkeo kwamba mbona mwenzako anapendeza lakini wewe upo upo tu. Hiyo italeta tafsiri mbaya kwake atahisi unamtamani rafiki yake hivyo kusababisha ugomvi. Wew mnunulie vipodozi na nguo nzuri mwambie vaa mke wangu upendeze,”anasema.

Siri za kifamilia ambazo si zako binafsi

Kama ndugu au jamaa amekuamini na kukupa siri, si busara kumwambia mwenza wako bila ruhusa. Hata kama uko karibu naye, bado unapaswa kuheshimu mipaka ya wengine.

“Kuna wanandoa wengine wanapendana sana kiasi kwamba kwao kufanya umbea ni kawaida tu, wanaambizana hata mambo ambayo yalipaswa kuwa siri kati ya waliowapa siri hizo. Hiyo haifai…wakati mwingine ukimwambia mwenza siri za kifamilia au hata za rafiki zako unasababisha mwenza wako kumchukulia tofauti..anaweza kumuheshimu au kumshusha kulingana na siri yenyewe,”anasema Suleyman Mohamed, mkazi mkoani Mwanza.

Ulinganisho wa mwenza wako na watu wengine

Kumwambia mwenza wako kuwa mtu fulani ni bora kwake kwa kipengele fulani kama urembo, kipato au tabia, ni jambo la kuumiza. Hii ni aina ya siri inayoweza kuwa ni mawazo ya ndani, lakini kuyatamka kunaweza kuwa na madhara makubwa.

Mwanasaikolojia na mshauri wa uhusiano, Dk Jerry Nyabululu anasema kumlinganisha mwenza wako na mtu mwingine ni kosa la kisaikolojia linaloweza kuathiri uhusiano kwa njia nyingi.

Anasema moja ya njia hizo ni kudhoofisha utu wa mwenza wake kutokana na mtu anayelinganishwa mara kwa mara, kuhisi hatoshi na anapoteza thamani binafsi.

“Pia kujenga uhasama na migogoro kwani ulinganisho huleta hisia za hasira, wivu, au visasi…athari nyingine ni pamoja na kushusha motisha ya kuboresha uhusiano, mwenza anaweza kukata tamaa kwa kuona juhudi zake hazithaminiwi,”anasema Dk Jerry.

Anasema pia inaweza kuvuruga msingi wa upendo kwakuwa ulinganisho huondoa heshima na kuibua mashaka, hivyo kuharibu uhusiano wa kimapenzi.

“Kwa hiyo, badala ya kulinganisha ni vyema kushirikiana kuboresha yale yanayokosekana bila kutumia watu wa nje kama kipimo,”anasema.

Matamanio ya muda mfupi yasiyo na msingi

Watu hufikiria mambo mbalimbali, na si kila wazo linapaswa kusemwa. Ikiwa una hisia au ndoto ya muda mfupi ambayo haina maana wala hatari yoyote, ifanye kuwa siri yako.

Athari ni kumfanya mwenza wako ajisikie hawezi kukufikisha unapotaka, kuamsha hofu ya kukataliwa au kutotosheleza, kuvuruga mwelekeo wa malengo ya pamoja katika ndoa.

Kwa nini siri hizi zisitamkwe?

Kuepusha maumivu yasiyo na sababu; si kila ukweli unafaa kusemwa kwa sababu unaweza kuumiza bila kujenga.

Maduhu anasema siri hufaa kubaki moyoni kwa sababu zinalinda amani ya uhusiano kwani  kusema maneno yasiyopaswa kusemwa,  huongeza majeraha ya kihisia badala ya kutatua matatizo.

“Hazijengi bali zinabomoa..hazitoi suluhisho la kiuhusiano, bali huongeza maumivu na mashaka,” anasema.

Ndoa ni safari ya pamoja inayohitaji hekima, busara, na ustaarabu katika mawasiliano. Ingawa uwazi ni muhimu, si kila siri inapaswa kuwekwa mezani.

Baadhi ya mambo bora kubaki kuwa ya mtu binafsi, hasa kama kuyafichua kutaleta maumivu au matatizo yasiyo ya lazima. Hii haimaanishi kuwa na maisha ya siri ya hatari, bali ni kuheshimu mipaka ya hisia, utu, na historia ya kila mmoja.

Kwa kutumia busara katika kushiriki habari, wanandoa wanaweza kuimarisha uhusiano wao na kujenga mazingira ya kuaminiana, kuheshimiana na kudumu katika upendo wa kweli.

Mafundisho ya dini nayo…

Mchungaji Damiano Makala wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) usharika wa Amani mjini Bariadi anasema kuwa ndoa ni agano takatifu mbele za Mungu, hivyo siri za ndani ya wanandoa zinapaswa kulindwa kwa kuwa kuzifichua ni kuvunja uaminifu ambao Mungu mwenyewe ameuweka kati yao.

 “Biblia inasema ‘Mtu mwaminifu huficha jambo’ (Methali 11:13). Ikiwa kila jambo la faragha litatamkwa hadharani, upendo na heshima huanza kufifia, na shetani hupata nafasi ya kuleta migogoro na mafarakano. Siri ni sehemu ya uaminifu katika upendo wa kweli.”anasema.

Naye Sheikh wa Wilaya ya Maswa, Isa Eliasa anasema kuwa katika Uislamu, mtu anayefunua siri za mwenza wake anachukuliwa kama amevunja amana.

“Mtume Muhammad (Rehema na amani ziwe juu yake) alisema: ‘Watu wabaya zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu ni wale wanaofunua siri za wake zao baada ya kuwa nao karibu.’ Siri za kifamilia ni amana, na kuzificha ni sehemu ya kumcha Mungu (taqwa) na kulinda heshima ya ndoa,”anaeleza   na kuongeza: “Mwenye kuzitangaza hadharani, huleta fitina na mafarakano yasiyo na mwisho.”