Wanawake aina hii doa kwa jamii

Katika muktadha wa kijamii unaozidi kushuhudia mabadiliko ya maadili na mitazamo ya uhusiano, kundi la wanawake linaibuka na kuacha doa kwa wenzao na jamii kwa jumla.

Hawa si wanawake wa kawaida wanaotafuta wapenzi au wenza wa maisha, bali ni wale wanaopatikana katika mazingira ya kila siku kama mikutano, hafla za kijamii, au hata kwenye usafiri wa umma, ambapo hukutana na wanaume kwa bahati tu, kisha kutumia fursa hiyo kama njia ya kujinufaisha kifedha.

Kwa kawaida, mkutano wa kwanza huwa wa kawaida kabisa. Salamu, tabasamu, na hatimaye kubadilishana namba huonekana kama ishara ya urafiki au mwanzo wa uhusiano.

Lakini kabla hata mawasiliano hayajakomaa, wanawake hawa huanza kuomba msaada wa kifedha. Wengine huanza kwa ujumbe kama vile: “Ningependa unisaidie tu kidogo, nimekwama.”

Maombi haya huongezeka kwa kasi; kutoka vocha hadi ada, kutoka nauli hadi gharama za saluni. Kwao, pesa ni msingi wa kila mawasiliano.

Ni tatizo ambalo linazidi kushamiri, likiwaathiri hasa vijana wa kiume wanaojaribu kujenga maisha na uhusiano wa maana.

Kwa kutumia lugha ya kiungwana na sura zenye mvuto, wanawake hawa hujifanya wa heshima na wa maadili, lakini nia yao halisi ni kutumia huruma na hila kupata pesa kwa njia isiyo ya halali.

Wataalamu wa masuala ya kijamii wanatambua tabia hii kama ishara ya uharibifu wa maadili miongoni mwa wanawake.

Mtaalamu wa saikolojia ya jamii, Fatuma Ndete, anasema: “Mtazamo wa kutegemea wanaume kiholela kwa masuala ya kifedha mara tu baada ya mawasiliano ya awali si tu unadhalilisha jinsi ya kike, bali pia unadumaza maendeleo ya kijamii kwa kuendeleza utegemezi usio wa lazima.”

Kwa mujibu wa baadhi ya vijana waliohojiwa, wanawake wa aina hii huleta mchanganyiko wa maumivu ya kihisia na hasara za kifedha.

 “Unakutana naye mkutanoni, mnaongea siku moja tu, kesho anakuambia hana nauli, anataka elfu tano. Ukimpa, kesho atakuambia mtoto wake ni mgonjwa,” anasema Brian Kejo, kijana mkazi wa Arusha. Anoangeza: “Ukikataa, anakuita mchoyo au anakutukana. Wanatumia huruma kama silaha.”

Hali hii pia inachangia kuporomoka kwa imani kati ya wanaume na wanawake. Wanaume wengi, baada ya kupitia visa vya namna hii, hujenga mitazamo hasi kuhusu wanawake kwa ujumla.

Hata wanawake wa kweli, waadilifu na wanaojituma, hujikuta wakipata lawama zisizo zao.

“Mara nyingi tunakosa hata kusaidiwa kwa sababu mtu mwingine alimvunja moyo kwa kumwibia pesa,” anasema Mary Fuko, mwanafunzi wa chuo kikuu jijini Dar es Salaam.

Tabia hii pia ina athari kubwa kwa maendeleo ya wanawake. Badala ya kuwahamasisha kuwa na juhudi, kujituma na kujitegemea, baadhi ya wanawake wanaamini kuwa wanaume ni suluhisho la kila changamoto ya maisha.

Hii ni dhana potofu inayodhoofisha juhudi za uwezeshaji wa wanawake na maendeleo ya kiuchumi kwa ujumla.

Jamii inapaswa kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na tabia hii. Kwanza, ni muhimu kwa vijana wa kiume kuelewa kuwa kutoa pesa si msingi wa uhusiano. Uhusiano wa kweli hujengwa kwa kuheshimiana, kuelewana, na kushirikiana.

Ikiwa mwanamke anaanza uhusiano kwa kuomba pesa, hiyo ni dalili ya kukosa uaminifu wa kiuhusiano. Pili, ni jukumu la wazazi, walimu na viongozi wa dini kutoa elimu ya maadili kwa watoto wa kike mapema, ili kuondoa dhana kwamba mwanamume ni chombo cha mapato.

Serikali na mashirika ya kijamii pia yanahimizwa kuanzisha kampeni za mafunzo ya kujitegemea kwa wanawake, pamoja na kuwapa fursa za kiuchumi zitakazowawezesha kujikimu bila kutegemea misaada ya wanaume wanaokutana nao kwa bahati tu. “Tunahitaji kuwajengea wanawake uwezo wa kifedha na kiakili. Kujitegemea kunaleta heshima ya kweli,” anasema Grace Mwikati, mwanaharakati wa haki za wanawake.

Kwa upande mwingine, kuna haja ya kuweka wazi kwamba wanawake wengi ni waadilifu, wachapa kazi, na wanaojituma kila siku kujenga maisha bora.

Hawa wanawake wachache wanaotumia ujanja wa kihisia kwa manufaa yao ya kifedha hawapaswi kuwa kigezo cha kuhukumu jinsia nzima. Hata hivyo, kukaa kimya kuhusu tabia zao ni kuruhusu doa hili kuenea zaidi.

Wanaume wanapaswa kujifunza kusema “hapana” kwa heshima na uthabiti. Ukarimu ni jambo jema, lakini unapotumiwa vibaya, hugeuka kuwa sumu ya maendeleo.

Mwanamke anayekupenda kweli hatakudharau kwa sababu hujampa pesa, bali atakujali kwa hali yako halisi na kushirikiana nawe katika changamoto na mafanikio.

Katika jamii yenye matumaini ya maendeleo na usawa wa kijinsia, ni muhimu kuwatambua wanawake wa aina hii kwa uhalisia wao.

Si kwa kuwachukia, bali kwa kuwaepuka na kuwaelimisha wengine. Maendeleo ya jamii hayawezi kujengwa juu ya msingi wa ujanja wa mawasiliano ya muda mfupi na tamaa ya fedha.

Ni wakati wa kusema wazi kuwa wanawake wa aina hii ni doa; na ni jukumu la kila mmoja wetu kulisafisha.