.,……………
Mgombea ubunge wa Jimbo la Kawe kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Glory Tausi Shayo, ameahidi kushughulikia changamoto sugu zinazowakabili wananchi wa jimbo hilo, zikiwemo miundombinu mibovu, elimu yenye michango mingi na kero kwa wavuvi.
Katika ziara yake kwenye kata za Msasani na Mikocheni, Glory amezungumza na wavuvi na kueleza kuwa wengi wao wameamua kujiajiri kupitia sekta ya uvuvi, lakini wanakumbana na kero nyingi ikiwemo maafisa uvuvi kudai faini kubwa na kutokutoa risiti. Amesema pia wavuvi wanataka leseni za uvuvi zitolewe kwa muda wa miaka mitano badala ya mwaka mmoja ili kupunguza usumbufu.
Glory amesema ameamua kugombea ubunge wa Kawe kwa lengo la kulifanya kuwa jimbo bora lenye huduma bora kwa wananchi. Ameeleza kuwa Kawe ni miongoni mwa majimbo yenye miundombinu mibovu – hakuna barabara nzuri na kwa urahisi, hakuna mitaro, na huduma za afya zimekuwa “mwiba mchungu”.
Aidha, ameahidi kupambana na changamoto ya elimu kwa kuhakikisha elimu inakuwa bure kwa vitendo na si kwa kauli tu. “Sasa hivi elimu inaitwa bure lakini ina michango mingi mno. Nitahakikisha elimu inakuwa bure kweli na vijana wanapata ajira,” alisema.
Glory ametoa wito kwa wananchi wa Kawe kujitokeza kwa wingi tarehe 29 Oktoba 2025 na kumpigia kura ili aweze kuwatumikia na kutatua kero zao kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Dorothy Semu, amewahimiza wananchi wa Kawe kumpigia kura Glory Tausi Shayo, akimwelezea kuwa ni kiongozi jasiri, anayejiamini na mwenye nia ya dhati ya kuleta mabadiliko.