NAIBU KATIBU MKUU UVCCM AWATAKA VIJANA WA CCM CHATO KUSINI KUTOBWETEKA

Mgombea Ubunge wa Jimbo la Chato Kusini,Paschal Lutandula,akizungumza na wana CCM.

Naibu Katibu mkuu wa UVCCM Tanzania Bara,Mussa Mwakitinya akizungumza na wajumbe wa CCM Jimbo la Chato Kusini.

…………….

CHATO

ZIKIWA zimesalia siku 10 kufanyika Uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani nchini, Naibu Katibu mkuu wa Jumuia ya Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) Tanzania Bara, Mussa Mwakitinya, amewataka vijana wa Chama hicho kutobweteka na idadi kubwa ya wagombea wake kupita bila kupingwa kwenye baadhi ya majimbo na kata na kwamba jukumu la kuzitafuta kura ni muhimu zaidi.

Amesema Chama hicho hakihitaji kupata ushindi mwembamba badala yake anawataka wananchi kukichagua Chama hicho kwa kura nyingi na kuvunja rekodi ya chaguzi zingine zilizopita.

Alikuwa kwenye mkutano wa ndani wa CCM uliofanyika kwenye Kata ya Bwanga Jimbo la Chato Kusini, wilayani Chato mkoani Geita kwa lengo la kuwahamasisha kutafuta kura za Chama hicho.

Aesema ili kufikia azma hiyo vijana wa Chama Cha Mapinduzi, wanalo jukumu kubwa la kuwahamasisha wananchi kumpigia kura nyingi mgombea Urais wa CCM,Dkt. Samia Suluhu Hassan,Mbunge wa Jimbo la Chato Kusini, Paschal Lutandula na Madiwani wote wa kata 9 katika Jimbo hilo.

Mwakitinya ameendelea kuwahamasisha vijana kuzisaka kura za Chama hicho katika maeneo yote yanayoruhusiwa ikiwa ni pamoja na kwenye masoko, minada, nje ya nyumba za ibada na ikiwezekana hata kwenye nyumba za kulala wageni.

Hata hivyo amewasisitiza vijana kuwa ni nguzo ya ulinzi wa amani ya Tanzania, na kwamba wasikubali kurubuniwa na baadhi ya watu wasiopenda amani na utulivu uliopo nchini.

Kwa upande wake Mgombea wa Jimbo la Chato Kusini kwa tiketi ya CCM,Paschal Lutandula, amesema Chama Cha Mapinduzi kipo katika mikono salama na kwamba wananchi wapo tayali kwa kukichagua Chama hicho kwa kura nyingi.

Amesema mgombea wa Urais wa CCM, amefanya kazi kubwa sana katika makundi yote ya kijamii wakiwemo, wakulima wadogo na wakubwa, Wavuvi, Wachimbaji Madini, Mawakala wa usafirishaji, Waganga wa Jadi pamoja na wananchi wa kawaida.

Amemhakikishia Naibu Katibu mkuu wa UVCCM Tanzania Bara, kuwa CCM Jimbo la Chato Kusini lina uhakika mkubwa wa kukipatia Chama hicho ushindi wa kishindo ifikapo Oktoba 29 mwaka huu.

         Mwisho.