Ibenge anavyokaribia kuipeleka azam fc nchi ya ahadi CAF

MATAJIRI wa Jiji la Dar es Salaam, Azam FC, imeanza vyema tiketi ya kuisaka hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya juzi kuibuka na ushindi wa mabao 2-0, dhidi ya Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo, Mabaharia wa KMKM kutoka Zanzibar.

Katika mechi hiyo ya kwanza iliyopigwa Kwenye Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar, mabao ya Azam yalifungwa na mshambuliaji, Jephte Kitambala Bola dakika ya 6, huku lingine likifungwa na beki wa kushoto wa kikosi hicho, Pascal Msindo kunako dakika ya 42.

Timu hizo zitarudiana Oktoba 24, 2025 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar, ingawa wakati hilo likisubiriwa, miamba hiyo inakabiliwa na rekodi chonganishi kama ambayo Mwanaspoti linaelezea.

IBE 01

IBENGE AKARIBIA REKODI MPYA

Ushindi wa Azam unamfanya kocha wa timu hiyo raia wa DR Congo, Florent Ibenge, kubakiwa na dakika 90 za kuandika rekodi mpya kwa kikosi hicho ya kufuzu katika hatua ya makundi ya Michuano ya CAF tangu kuasisiwa kwake.

Rekodi kubwa ya Azam katika Michuano ya CAF ni kutolewa raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka 2013 na FAR Rabat ya Morocco kwa mabao 2-1, iliyofungwa ugenini baada ya awali kikosi hicho kushindwa kutamba jijini Dar es Salaam na kulazimishwa suluhu (0-0).

Katika raundi ya awali mwaka huo wa 2013, Azam ilipata ushindi wa kishindo wa mabao 8-1 dhidi ya El Nasir ya Sudan Kusini kisha kuitupa nje Barrack Young Controller II ya Liberia kwa mabao 2-1 na mara zote ilizoshiriki Kombe hilo na Ligi ya Mabingwa Barani Afrika imekuwa ikiishia njiani, Ingawa safari hii kuna uwezekano mkubwa ikaandika rekodi mpya chini ya Mkongomani Florent Ibenge.

IBE 04

Azam imetwaa taji moja la Ligi Kuu Bara msimu wa 2013- 2014, mawili ya Kombe la Kagame 2015 na 2018 na matano ya Kombe la Mapinduzi ikiwa kinara ikifanya hivyo 2012, 2013, 2017, 2018 na 2019, ikibeba Kombe la Shirikisho (FA) mara moja 2019 na Ngao ya Jamii pia mara moja 2016.

Ibenge aliyetambulishwa na kikosi hicho, Julai 5, 2025, akitokea Al Hilal Omdurman ya Sudan, akirithi nafasi ya Kocha, Mmorocco Rachid Taoussi, ndiye aliyebeba matumaini makubwa ya kikosi hicho ya kusaka rekodi mpya ambayo haijawahi kuandikwa na timu hiyo tangu ilipoasisiwa mwaka 2004.

IBE 02

Wakati Azam ikisaka rekodi mpya ya kufuzu hatua ya makundi kwa mara ya kwanza katika historia kama ilivyo pia Kwa KMKM, ila Mabaharia hao wana mtihani mgumu wa kufikia malengo hayo.

Licha ya timu hiyo kuhitaji tu ushindi wa mabao 3-0, katika mechi ya marudiano Oktoba 24, ili kusonga hatua inayofuata, ila kikosi hicho kinaandamwa pia na rekodi mbovu kwenye Michuano ya CAF, jambo linaloiweka katika mtihani mgumu.

IBE 05

KMKM iliyorejea Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa mara ya kwanza msimu huu baada ya miaka 14, tangu iliposhiriki mwaka 2011, haina rekodi nzuri kwani imekuwa ikitolewa raundi ya awali kama ilivyokuwa pia katika Ligi ya Mabingwa Barani Afrika iliposhiriki Mabaharia hao kuanzia mwaka 2005, 2014, 2015, 2020 na 2022.

KMKM iliyobeba mataji tisa ya Ligi Kuu Zanzibar ikiwa kinara ikifanya hivyo mwaka 1984, 1986, 2004, 2013, 2014, 2019, 2021, 2022 na 2023, pia ikitwaa Nyerere Cup mara tatu 1977, 1982 na 1983 na Kombe la Zanzibar (FA) mara mbili 2002 na 2024, mbali na Ngao ya Jamii ikiwamo ya msimu huu, ila kwa upande wa Michuano ya CAF imekuwa changamoto zaidi kwa kikosi hicho Maalumu cha Kuzuia Magendo.

IBE 03

Akizungumza baada ya mechi hiyo, Kocha Mkuu wa KMKM, Hababuu Ali, anasema licha ya kupoteza kwa idadi kubwa ya mabao, ila bado wana nafasi nyingine ya kurekebisha makosa yaliyojitokeza katika pambano hilo.

“Siwezi kusema tunaenda kupindua meza katika mechi ya marudiano, ila tutapambana kadri ya uwezo wetu na tuone kile kitakachotokea baada ya hapo ndipo tutajua hatima yetu msimu huu.”

Kwa upande wa Kocha wa Azam FC, Florent Ibenge, anasema licha ya ushindi huo ila bado wachezaji wa kikosi hicho wanatakiwa kufanya vizuri zaidi ya kile walichokionyesha dhidi ya KMKM.

“Malengo yetu ni kuvuka hatua ijayo lakini niseme wazi bado tuna mechi nyingine ya marudiano ambayo ndiyo itakayoamua kile ambacho kwa umoja wetu tumedhamiria kukifanya msimu huu,” anasema Ibenge na kuongeza;

“Ushindi wa mabao mawili ni mkubwa na unatupa matumaini ya mechi yetu ya marudio, ila tunapaswa kutambua hizi ni dakika 45 za kwanza na tuna nyingine pia za mwisho za kufikie kile tunachokikusudia kwa umoja wetu.”