Dk Nchimbi alivyopokewa kwao, akabidhiwa serikalini

Nyasa. Mwamba amefika nyumbani na tunatamba naye. Huyu ni mgombea mwenza, mtoto wetu, akafanye kazi kwa weledi na kuwatumikia Watanzania wote bila ubaguzi.

Hizi ni hisia tofauti za wananchi wa Nyasa, Mkoa wa Ruvuma, wakimwelezea na kumtakia heri Dk Emmanuel Nchimbi kwenda kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan akiwa Makamu wa Rais.

Dk Nchimbi ni mgombea mwenza wa urais kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), ambaye leo Jumapili, Oktoba 19, 2025 amerejea tena Ruvuma hususan Nyasa kusaka ushindi wa CCM katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Jumatano ya Oktoba 29, 2025.

Septemba 20, 2025 alikuwa Ruvuma na alifanya mikutano na mgombea urais, Samia maeneo mbalimbali isipokuwa Nyasa.

Wakati wananchi wakimpongeza na kumkabidhi serikalini baada ya kuwa ‘mfalme wa Nyasa’ yeye amejiapiza mbele yao kwenda kufanya kazi kwa weledi kwa kumsaidia Rais Samia ili atimize malengo ya kuwatumikia wananchi.

Tofauti na mikutano mingine zaidi ya 95 aliyoifanya kwenye mikoa 25 ya Tanzania ikiwemo miwili ya Zanzibar tangu kuanza kwa kampeni, huu wa leo kwao umekuwa wa kipekee, ukitawaliwa na hamasa.

Mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Shule ya Msingi Lituhi, amepokewa na umati wa watu, ngoma za kitamaduni za ukanda huo zikipamba kwa burudani hali iliyochagiza shangwe mara kwa mara.

Baada ya kupanda tu jukwaa kuu, wazee wa Ruvuma wakiongozwa na Saad Wabu Musa, Chifu wa Nyasa na Katibu wa Machifu wa Mkoa wa Ruvuma, walimpa baraka na kumkabidhi serikalini.

“Mwamba amefika nyumbani, tunatamba naye, kila mtu ana kwake na kwa kuwa ulikuwa mfalme huku kwetu, sasa tunakutoa na kuikabidhi Serikali ili ikutumie,” amesema Chifu Musa.

Sauti ya maelezo hayo, ameyatoa wakati Dk Nchimbi akiwa amekaa kwenye kigoda, amekabidhiwa vifaa vya jadi, kufungwa kitambaa chekundu kichwani na kufungwa cheupe.

Umati wa watu uwanjani hapo ulikuwa ukishangilia huku sauti zikitoka,”Baba, Baba, Baba, Baba.”

“Kwa heshima kubwa, Rais Samia alikupa mtoto wetu wa Nyasa, ulimsaidia ukiwa katibu mkuu na sasa amekuteua kuwa msaidizi wake.Tunamwambia Chifu Hangaya kwamba hatumdai na sisi ndio anatudai,” amesema Chifu Musa.

Mwananchi limepata wasaa wa kuzungumza na baadhi ya wananchi juu ya tukio hilo lakini ndugu yao kupata nafasi hiyo nyeti.

Rikopo Chale, Mkazi wa Ndumbi amesema, anachopaswa kwenda kukifanya Dk Nchimbi, asiwasahau, akawapambanie ikiwemo kupata vifaa vya matibabu.

“Sisi tumempa vifaa vile ili kutupambania na kama tuna hali mbaya atatusaidia na tunamwomba Rais Samia aendelee kumwamini na kumfundisha mambo mengi,” amesema Chale.

Mkazi wa Mbaha, John Komba amesema: “Sisi tunafurahi sana kumpata kiongozi, hatujawahi kupata kiongozi mkubwa anayetokana na kanda hii hasa Nyasa. “Asimamie maendeleo ambayo ndiyo msingi wa wote na asiwe mbaguzi, si wa Nyasa tu bali Watanzania wote na ndiyo maana tumemtoa serikalini lakini nyumbani ni nyumbani, hakuna anayesahau kwao,” amesema Komba.

Andrew Ndeji, Mkazi wa Lituhi yeye amesema: “Huyu ni mgombea mwenza, mtoto wetu, kwa nafasi yake inatuheshimisha. “Sisi hatuna lami, maji ya kutosha na tuna uhakika atatusaidia. Na huu umati unauona hapa tumekuja kumwona na kusikia atatuambia nini lakini sisi tunamwona anafaa, yuko safi basi akamsaidie mama,” amesema Ndeji.

‘Ala kiapo mbele ya nduguze’

Katika hotuba yake ya dakika 25, ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Samia kwa kumwamini kwenda kuwa msaidizi wake huku akisema: “Nitumie nafasi hii kuwahakikishia wazee wetu wa Nyasa na ndugu zangu wenyeji wa Nyasa,” kwamba atafanya kazi vizuri.

“Nitafanya kila jitihada kumsaidia Rais Samia Suluhu Hassan kutekeleza Ilani ya chama chetu. Lakini pia nitafanya kila jitihada kuhakikisha Rais Samia anaona kwamba kuchukua mtu kutoka Ruvuma anaweza kuwa msaada kwake,” amesema Dk Nchimbi.

Katika mkutano huo, Dk Nchimbi ameeleza nia ya kutaka kuwania ubunge Nyasa mwaka 2015, baada ya kustaafu Songea Mjini, lakini akajiweka kando kumpisha Stella Manyanya.

Dk Nchimbi amesema baada ya kutangaza kustaafu ubunge Songea alikoongoza kwa miaka 10, wazee wa Nyasa walikwenda kumwomba akagombea huko.

“Mwaka 2015, nilipotangaza napumzika ubunge wa Songea Mjini, mtakumbuka wengi wenu wazee wawili wawili walitoka kila kata wakaja kuniona Songea. Kwamba kama umeamua kupumzika Songea basi njoo huku na mimi wakati ule baada ya kuwasikiliza nikakubali,” amesema.

Amesema alituma vijana wake kwenda Nyasa kwenye vijiji kutoa salamu kwamba sasa amekubali anakuja… lakini urafiki una gharama.

“Stella Manyanya, rafiki yangu akaja mbio kuniona. Kaka mwenzako nimeshaanza zamani wewe umeombwa juzi tu naomba usije. Nikaambiwa basi dada isiwe taabu napumzika. Bila Stella dada yangu wakati ule mngeniona.

“Lakini mwaka 2020, John akataka kuja tena. Stella akanitumia salamu. John anataka kuja nikampigia simu John nikamwambia, ebu mwache mwenzako apate sehemu ya pili akakubali safari hii John wala hakunitafuta akaja kuchukua fomu bila kuniambia akajua jamaa wataleta ule urafiki wao,” amesema huku watu wakiangua vicheko.

Dk Nchimbi amesema watamsaidia John ambaye ni mdogo wake kuhakikisha mambo yaliyoahidiwa na Ilani ya Chama cha Mapinduzi yanatekelezwa, lakini pia kero ambazo amezitolea zinashughulikiwa.

“Tumesema katika Wilaya ya Nyasa kwanza tutaendelea kuiboresha hospitali yetu ya Wilaya ili iwe na vifaa vingi zaidi, iwe na majengo mengi zaidi, lakini pia iwe na madaktari wengi zaidi,” ameahidi.

Amesema wanakwenda kujenga zahanati mpya 10 Nyasa, vituo vipya vya afya sita ikiwemo kimoja Lituhi.

“Kwenye elimu, tunakwenda kujenga shule za msingi mpya tisa, sekondari mpya sita na kwenye shule za zamani za msingi na sekondari, tunakwenda kuongeza madarasa mapya 210 lakini pia tunakwenda kujenga maabara mpya 14,” amesema.

Ahadi nyingine amesema wanakwenda kujenga stendi ya kisasa na kwenye umeme kwa kuwa vijiji vyote vimekwisha unganishwa watahakikisha vitongoji vyote vinafikiwa.

Eneo la maji, Dk Nchimbi amebainisha miradi mbalimbali ukiwemo wa Luhangarasi, Ruhinda, Malinda, Chiulu Lumemo na mawasiliano. Pia, ukarabati wa mradi wa maji Lundo Nkindo na Ngombo. Kujenga visima virefu kwenye vijiji ambavyo havina maji ya kutosha ili kuhakikisha upatikanaji wa maji safi na salama.

Pia kufunga machujio ya kusafisha maji ili kuhakikisha maji yanatoka safi na salama katika maeneo yote. Lakini pia kuongeza mtandao wa maji maeneo ambayo maji hayajafika ili kuhakikisha maeneo mengi yanapata maji safi na salama.

Eneo la barabara alizozitaja kujengwa ni ya Topol, Liparamba-Mseto, Upoo -Luhangarasi, Kingerikiti-Kikole Matipwili, Mpepo-Lusewa na ujenzi wa daraja la zege lenye urefu wa mita 60 katika barabara ya Kilosa Likwilu Marine.

“Kuanza ujenzi na ukarabati wa daraja la Mitomoni. Ujenzi wa barabara ya Mtua Liparamba kwa kiwango cha changarawe. Ujenzi kwa kiwango cha lami barabara ya Mbamba Bay- Liuli- Lituhi kilomita 112. Ujenzi wa barabara ya Nyoni Maguu kilomita 25,” amesema.

Barabara zingine ni ukamilishaji wa barabara ya Kitahi- Lituhi kilometa 93 ikijumuisha sehemu za Amanimakoro -Ruanda kilomita 35 na Ruanda -Ndumbi kilometa 50. Ujenzi wa barabara ya kiwango cha lami Barabara ya Nangomba Chiwindi kilometa 40 pamoja na ujenzi wa barabara ya Lulindi-Mpepo-Darpori.

Awali, mgombea ubunge wa Nyasa, John Nchimbi amesema miradi mbalimbali imefanyika ikiwamo ya elimu, afya na maji.

“Katika wilaya hii tumeshuhudia shule za msingi mpya sita zikijengwa, kujenga sekondari mpya sita zimejengwa. Tumeshuhudia madarasa katika shule za msingi 116 na madarasa katika shule za sekondari 70 yamejengwa,” amesema.

“Hospitali yetu ya Wilaya imeendelea kuimarishwa na imejengwa zaidi na hivyo inatoa huduma. Tumepata vituo vinne vya afya, zahanati nane. Utufikishie salamu zetu kwa Mama Samia. Tulikuwa tunapata maji kwa asilimia 47 lakini sasa ni asilimia 68,” amesema.

“Ninaamini ulipokuwa ukiandika ilani, kuna mambo mazuri ulikuwa umeyaweka kwa ajili ya Nyasa. Hili nakuachia wewe ili itamke kama lipo Nyasa. Kwa mara ya kwanza toka wamepata uhuru wasikie harufu ya lami ikipita kwao,” amesema John.