Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Makini, Ameir Hassan Ameir amesema endapo atachaguliwa kuongoza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, ataweka mapendekezo maalumu kwa Baraza la Wawakilishi ili kuingizwa kifungu maalumu kwenye Katiba kitakachotoa kipaumbele kwa makundi maalumu, hususan watoto yatima.
Ameir amesema serikali yake pia itatoa ruzuku maalumu kwa taasisi zinazolea watoto yatima ili ziwahudumie ipasavyo, ikiwemo kuwawezesha kupata huduma muhimu kama elimu, afya, chakula na malazi kama watoto wengine.
Ametoa kauli hiyo leo Jumapili, Oktoba 19, 2025, alipotembelea kituo cha kulelea watoto yatima chz Maftuh Foundation Orphanage, kilichopo Tunguu Kibele, Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni sehemu ya kampeni zake za uchaguzi na mawasiliano na makundi mbalimbali ya kijamii.
“Endapo wananchi watanipa ridhaa, jambo nitakalolipa kipaumbele ni kuhakikisha watoto yatima wanapata huduma bora na kuishi maisha yenye hadhi sawa na wengine,” amesema Ameir.
Ameongeza kuwa katika ilani ya Chama cha Makini, makundi maalumu yametajwa wazi, hivyo serikali yake itahakikisha inatekeleza kwa vitendo matakwa hayo.

Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama cha Makini, Ameir Hassan Ameir Akizungumza na watoto yatima katika kituo cha kulelea watoto cha Maftuh Foundation Ophanange Tunguu Kibele Mkoa wa Kusini Unguja ikiwa ni mwendelezo wa kukutana na makundi mbalilbali katika mchakato wa kampeni za kusaka kura.
Ameir amefafanua kuwa atawasilisha pendekezo la kuongeza kifungu maalumu katika Katiba ili kuhakikisha hata baada ya kumaliza muda wake wa uongozi, serikali zitakazofuata zitaendelea kutekeleza wajibu wa kuyahudumia makundi hayo kikatiba, badala ya kutegemea misaada ya hisani.
Mbali na watoto yatima, Ameir alisema serikali yake itatoa kipaumbele kwa watu wenye ulemavu, wajane, wazee na vijana, akisisitiza kuwa makundi hayo yanahitaji uangalizi wa karibu na huduma stahiki.
“Makundi haya yanapaswa kuishi katika viwango vinavyokubalika, na hili tutalisimamia kwa nguvu zote tukipewa ridhaa na wananchi,” amesema.
Aidha, akiwa kituoni hapo, Ameir ameahidi kuwasomesha bure watoto 10 kutoka kituo hicho kuanzia elimu ya awali hadi kidato cha nne, bila kujali matokeo ya uchaguzi.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi wa kituo hicho, Halima Said Yahya, alisema kituo kina jumla ya watoto yatima 77, akimshukuru Ameir kwa msaada wa vyakula na kwa kutenga muda wa kuwatembelea.
“Tunamshukuru kwa moyo wake wa huruma na tunamuombea dua afanikiwe katika harakati zake,” alisema Halima.
Naye Katibu Mwenezi wa Taifa wa Chama cha Makini, Fahmi Khalfan Abdalla amesema kampeni zao zinaendelea vizuri na zimekuwa zikifanyika kwa amani na usalama, huku wakipata ushirikiano kutoka Tume ya Uchaguzi na vyombo vya dola.
“Mpaka sasa tunaelekea ukingoni mwa kampeni, tunashukuru kwa ushirikiano mzuri tuliopewa. Wananchi wametuelewa na wamepokea sera zetu kwa moyo,” amesema.