Namelok Sokoine: CCM itatokomeza migogoro ya wakulima na wafugaji

Arusha. Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Namelok Sokoine, amewataka wananchi wa Ngorongoro kujitokeza kwa wingi kukipa kura chama chake katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025.

Namelok amesema kuwa chama hicho ndicho chenye dhamira na uwezo wa kutokomeza kabisa migogoro ya muda mrefu, baina ya wakulima na wafugaji nchini.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika kata ya Ngaresero, wilayani Ngorongoro, Namelok amesema migogoro hiyo imekuwa ikirudisha nyuma maendeleo ya wananchi, hususan katika nyanja za kiuchumi na kijamii, hivyo kuiamini CCM ni kuendeleza hatua za kuhakikisha migogoro hiyo inabaki historia.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Namelok Sokoine,

“Mpeni kura Rais Samia ambaye ameonyesha uongozi wa mfano unaojali watu wa pembezoni, wenye dhamira ya kutatua changamoto za ardhi.”

“Ndio maana imepima maeneo ya malisho na kilimo, kuweka mipaka na kuimarisha miundombinu ya kijamii ili wananchi wa Ngorongoro na maeneo mengine wafuge na kulima kwa utulivu.”

Amesema kuwa chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, Serikali imeendelea kuwekeza katika upangaji na upimaji wa matumizi bora ya ardhi ili kuhakikisha wakulima na wafugaji wanaishi kwa amani bila migongano.

Namelok amesema juhudi za CCM kwa sasa zimejikita katika kusimamia utatuzi wa migogoro kwa njia za kisasa, ikiwemo upangaji wa ardhi, utoaji wa elimu kwa jamii na usuluhishi endelevu, hatua ambazo zinaimarisha umoja na ushirikiano kati ya wakulima na wafugaji.

Kwa upande wake, Yannick Ndoinyo, mgombea ubunge wa Jimbo la Ngorongoro kupitia CCM, amewataka wananchi wake kutumia kura zao kama silaha ya maendeleo kwa kuhakikisha wanashiriki kwa wingi uchaguzi mkuu wa baadaye mwaka huu.

“Kura ni silaha ya maendeleo, tukimpa Rais Samia na wagombea wa CCM ushindi, tunaihakikishia jamii yetu mwendelezo wa amani na maendeleo tuliyoanza kuyaona,” amesema Ndoinyo.

Waziri Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, amewataka viongozi wa serikali za mitaa kusaidia wananchi wa maeneo ya mbali kufika vituoni siku ya kupiga kura, akisisitiza kuwa kila Mtanzania anapaswa kushiriki katika maamuzi ya mustakabali wa nchi yake.

“Ni wajibu wetu kuhakikisha kila mwananchi, hasa wa vijijini, anapata fursa sawa ya kupiga kura kwa amani na utulivu. Hiyo ndiyo njia ya kuendeleza demokrasia na maendeleo ya kweli,” amesema Sumaye.