Siha. Wagonjwa wa Kifua Kikuu na wenye changamoto ya kupumua silikosesi, waliopo hospitali maalumu ya magonjwa ambukizi Kibong’oto wilayani Siha, mkoani Kilimanjaro, wamepatiwa msaada baada ya kutembelewa na viongozi wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Manyara (Marema).
Msaada uliokabidhiwa kwa wagonjwa hao na viongozi wa Marema ni pamoja na sabuni za kuogea na kufulia, miswaki, mafuta ya kujipaka, dawa za meno, sukari na fedha taslimu.
Mwenyekiti wa Marema, Elisha Mnyawi akizungumza wakati wa kukabidhi misaada hiyo leo Oktoba 19, 2025, amesema wametembelea wagonjwa hao ili kuwatia moyo na kuona maendeleo yao.
Mnyawi ameeleza japokuwa wachimbaji madini wagonjwa wapo kwenye hospitali hiyo ya Kibong’oto, pia wamebaini wagonjwa wengine ambao siyo wachimbaji wa madini.
Amesema ujio wao umewasaidia kujifunza vitu vipya ikiwemo namna ya kuepuka magonjwa ambukizi ya kifua kikuu na changamoto ya upumuaji wa mapafu silikosesi.
“Kipekee nimshukuru Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga ambaye hivi karibuni alifanya ziara Mirerani na kutuagiza kufuatilia wagonjwa wa T.B na Silikosesi na sasa tumetekeleza hilo,” amesema Mnyawi.
Makamu Mwenyekiti wa Marema, Money Yusuf amesema wamekuwa wakijitahidi kufuatilia miongozo ya afya ili kufanya shughuli za uchimbaji wa madini kwa manufaa ya wachimbaji.
Katibu wa Marema, Tariq Kibwe ameeleza kwamba wagonjwa wanaopatiwa huduma ya matibabu kwenye hospitali hiyo ni 22 wa Kifua Kikuu, na 19 wa changamoto ya kupumua silikosesi.
Kibwe ameeleza kwamba miongoni mwa wagonjwa hao wapo ambao siyo wachimbaji madini ya Tanzanite yupo kijana wa gereji, na mfanyakazi kiwanda cha saruji.
Mmoja wa wauguzi wa hospitali hiyo Bahati Laizer, amewashukuru viongozi hao kwa kufika kuwajulia hali wagonjwa hao na kuwapatia mahitaji hayo.
“Kwa niaba ya uongozi wa Hospitali ya Kibong’oto tunawashukuru viongozi wa wachimbaji kwa kututembelea na kuwaona wagonjwa,” amesema Laizer.
Mmoja kati ya wagonjwa hao, Lerumbuki Saigurani amewaomba wamiliki wa migodi kuwapatia fedha ili waweze kupata huduma stahiki katika hospitali hiyo.
“Serikali imetumia gharama kubwa kutuhudumia, kuajiri wauguzi, madaktari, dawa na mitungi ya kutusaidia kupumua, hivyo wamiliki wa migodi tuliyokuwa tunafanyia kazi watusaidie rasilimali fedha za kuchangia matibabu,” amesema Saigurani.