Simba ya meneja yafanya ukatili Eswatini

SIMBA imetanguliza mguu mmoja kwenye hatua ya makundi baada ya kupata ushindi wa kishindo wa mabao 3-0 ugenini Eswatini dhidi ya Nsingizini Hotspurs katika mechi yao ya kwanza ya hatua ya pili ya mtoano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Mambo hayakuwa mabaya sana kwa wawakilishi wengine wa Tanzania, Singida Black Stars ambao walipata sare ya bao 1-1 dhidi ya Flambeou de Centere ya Burundi, shukrani kwa bao la ugenini la Clatous Chama.

“Simba ya meneja,” ndivyo walivyokuwa wakiimba baadhi ya mashabiki wa Wekundu hao katika kujibu mashambulizi ambayo wamekuwa wakiyapokea kutoka kwa watani wao Yanga ambao wamekuwa wakiwakebehi kutokana na kocha wao mpya, Dimitar Pantev kukosa vigezo vya kusimamia benchi la ufundi na hivyo kupewa  madaraka ya umeneja.

Wababe hao wa Msimbazi wameendelea kusimamiwa na kocha mzawa Selemani Matola na ushirikiano wa wawili hao pamoja na kikosi kizima cha Simba wekundu hao wameendeleza kuthibitisha kuwa anga za kimataia ndio anga zao.

Simba ilipata bao la kuongoza kupitia kwa beki wake wa kati, Nangu akiuweka mpira wavuni kwa kichwa akiunganisha kona iliyochongwa na kiungo wa Afrika Kusini, Neo Maema katika dakika ya mwisho kabla ya timu hizo hazijaenda mapumziko.

Mtokea benchini, Kibu Denis aliweka chuma mbili likiwamo moja la dakika za jiooni na kuiweka Simba katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.

MENE 01

Yalikuwa ni matokeo ya kibabe ugenini na kuonyesha dalili zote za Simba kurejea katoka makali yake baada ya kuvuka hatua ya awali ya mtoano kwa ushindi mwembamba kwa mwendo wa mashabiki kushika ‘roho mkononi’. 

Kipindi cha kwanza timu zote zilikuwa zikicheza soka la kushambulia kwa kasi lakini ilikosekana utulivu kwenye kukamilisha mashambulizi yao.

Kwenye mashuti mawili yaliyolenga lango kwa Simba, moja ndio kilikuwa kichwa cha Nangu kilichojaa wavuni huku shuti moja likiwa la mpira wa adhabu ndogo lililopigwa na kiungo Ellie Mpanzu katika dakika ya 17.

Wenyeji Nsingizini Hotspurs kwenye kipindi cha kwanza hawakufanikiwa kupiga shuti hata Moja lililolenga lango, huku mashuti yao saba yakitoka nje.

Simba kwa mara ya kwanza msimu huu ikatoka iliongoza kwa umiliki wa mpira kwenye dakika 45 za kwanza ikimiliki kwa asilimia 52 dhidi ya 48 za Nsingizini.

Nafasi nzuri ambayo Simba iliitengeneza ilikuwa ni dakika ya 36 wakati kiungo wake Neo Maema alipopoteza nafasi ndani ya eneo la hatari shuti lake kali lilitoka nje kidogo chini akipokea pasi ya beki Shomari Kapombe.

Nsingizini nao ikapoteza nafasi dakika ya 39 kupitia kiungo wake Thubelihle Mavuso akiwa karibu na uso wa goli shuti lake linapaa wenyeji wakipoteza nafasi nzuri.

Alikuwa Wilson Nangu aliyetangulia kuipa Simba bao la kuongoza kwa njia ya kichwa akitumia mpira wa kona ya Neo Maema dakika  ya 45+2.

Hilo linakuwa bao la tatu kwa kichwa msimu huu kwa mabeki wa Simba akitanguliwa na Abdulrazack Hamza, Rushine de Reuck, Chamou Karaboue.

MENE 02
MENE 02

Bao hilo likatosha kuifanya mechi hiyo kwenda mapumziko huku Simba ikiongoza kwa bao 1-0 lakini pia ikiutawala vizuri mchezo huo ikicheza soka la kasi.

Kipindi cha pili Simba ilirudi na kasi ileile meneja Dimitar Pantev akirudi na mabadiliko ya kuongeza kasi kwenye kushambulia akimtoa Mwalimu na kuingia Jonathan Sowah.

Simba iliwazima Nsingizini ikimaliza mashambulizi yao kabla ya kufanyika kwa mabadiliko matatu yaliyowaongezea nguvu wekundu hao.

Dakika ya 78 Pantev aliwatoa Maema, Ahoua na Mutale nafasi zao zikichukuliwa na Kibu Denis, Yusuf Kagoma na Morris Abraham.

Mabadiliko hayo yalienda kuwaimarisha Simba katikati ya uwanja Kagoma akiongeza uguvu akicheza sambamba na Camara huku Kibu na Morris wakiongeza kasi kule mbele

Alikuwa Kibu Denis aliipatia Simba bao la pili dakika ya 84 likitengenezwa kwa shambulizi kali mfungaji akigeuka kiufundi na kumalizia kiufundi, akipokea pasi ya kisigino ya Sowah.

Mabadiliko hayo yakaendelea kuibeba Simba dakika ya 90 Kibu tena akaipa Simba bao la tatu likiwa la pili kwake akimalizia kwa ufundi, akipokea pasi ya Morris aliyeingia naye kipindi cha pili.

Ushindi huo wa mabao matatu unaifanya Simba kuendeleza rekodi ya ubabe wakiwa Eswatini kwani mwaka 2018 iliichapa Mbambane Swallows kwa mabao 4-0.

Kipa Moussa Camara hakuwepo kwenye mchezo huo kutokana na majeraha na Pantev alianza na Yakub Seleman ambaye ni mchezo wake wa kwanza wak kimataifa lakini kipa huyo alisimama imara akionyesha ubora mkubwa golini.

Vikosi Simba: Yakub Seleman, Shomari Kapombe, Antony Mligo, Rushine de Reuck, Nelson Nangu/Chamou Karaboue, Naby Camara, Joshua Mutale/Morris Abraham, Neo MaemaKibu Denis, Seleman Mwalimu/Jonathan Sowah, Jean Charles Ahoua/Kibu Denis, Ellie Mpanzu.

Nsingizini Hotspurs: Khanyakweze Shabalala, Vuyo Macina, Shongwe Nkosingphile, Dlamini Neliswa, Adeleke Ade, Ayanda Gadlela/Quality Dlamini, Joel Madondo, Kwakyi Kingsley, Thwala Kwakhe, Mavuso Thubelihle, Sizwe  Khumalo