Dar es Salaam. Safari ya kuusaka udiwani kwa makada wanne wa vyama mbalimbali vya siasa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, imeshindwa kufika mwisho, baada ya wagombea hao kupoteza uhai kwa nyakati tofauti kabla ya uchaguzi.
Wagombea udiwani hao waliofariki dunia, wanatoka vyama vya ACT – Wazalendo, Chama cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Wananchi (CUF), katika kata zilizopo mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza na Morogoro.
Wagombea udiwani waliofarikia dunia ni Hamis Msasa wa ACT – Wazalendo Kata ya Mindu, Morogoro Mjini, Feruzi Kamizula wa CCM Kata ya Nyakasungwa, Buchosa mkoani Mwanza, Rajab Mwanga wa CUF Kata ya Mbagala Kuu, Dar es Salaam na Hassan Hassan wa chama hicho Kata ya Chamwino, Morogoro.
Vifo vya wagombea hao vimesababisha Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), kwa nyakati tofauti kusitisha chaguzi katika kata hizo na kupanga tarehe za kufanyika kwa uchaguzi.
Kwa mujibu wa INEC, uchaguzi wa kata za Mbagala Kuu na Chamwino utafanyika Desemba 30, 2025 huku kampeni zake zikitarajiwa kufanyika kwa nyakati tofauti kuanzia Oktoba 22, Novemba hadi Desemba.
Mchakato wa uchaguzi wa kata hizo utakwenda sambamba na ule wa Jimbo la Fuoni Wilaya ya Magharibi, Unguja baada ya mgombea wa jimbo hilo, Abass Mwinyi kufariki dunia Septemba 25 katika Hospitali ya Lumumba Zanzibar, alikokuwa akipatiwa matibabu.
Jana, Jumamosi Oktoba 18,2025 INEC ilitoa taarifa kwa umma ikisema imepokea taarifa kutoka kwa msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Buchosa, ikiwataarifu kuhusu kifo cha Kamizula kilichotokea Oktoba 9, 2025 wilayani humo.
Kutokana na kifo hicho, INEC imeeleza msimamizi huyo wa uchaguzi alisisitisha uchaguzi wa udiwani katika kata hiyo, Oktoba 10, 2025.
“Taarifa ya kusitishwa kwa uchaguzi imetolewa kwa kuzingatia masharti ya kifungu cha 71 (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani na 1 ya mwaka 2024. Baada ya kusitisha kwa uchaguzi wa kata husika shughuli zote ikiwamo kampeni za udiwani kwa wagombea wengine zimesitishwa rasmi.”
Hata hivyo, katika taarifa hiyo, INEC imebainisha kuwa fomu za uteuzi wa mgombea udiwani wa Kata ya Nyakasungwa zimeanza kutolea Oktoba 18 hadi 24.
“Uteuzi wa udiwani Nyakasungwa kupitia CCM utafanyika Oktoba 24, kampeni zitafanyika kuanzia Oktoba 25 hadi 28, wakati Oktoba 29 hadi Oktoba Mosi zitasimama kupisha upigaji kura hadi kutangazwa matokeo.
“Kuanzia Novemba 2 hadi Desemba 29 zitaendelea na Desemba 30 uchaguzi utafanyika,” inaeleza taarifa ya INEC.