PIGENI KURA ZA MAENDELEO- MHE. WANU

Na Yohana Kidaga- Rufiji

Mlezi wa Umoja wa Wanawake wa CCM Tanzania( UWT) Wilaya ya Rufiji, na Mgombea wa Ubunge kwa jimbo la Makunduchi, Mhe. Wanu Hafidh ametoa wito kwa wanarufiji na watanzania kwa ujumla kukipigia kura CCM kwenye uchaguzi mkuu ili kupata maendeleo ya kweli.

Kauli hiyo ameitoa leo akiwa mgeni rasmi kwenye kongamano la UWT la Wilaya ya Rufiji lililofanyika Ikwiriri na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania bara na visiwani.

“Ndugu zangu tusifanye makosa katika uchaguzi huu kwa kuwa sumu hairambwi, CCM tunasema kura yako maendeleo yako”. Amefafanua Mhe.Wanu

Aidha, amesema Serikali kupitia kwa aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo Mhe. Mohamed Mchengerwa imeleta maendeleo makubwa katika kipindi kifupi na kuwaomba wananchi kumpigia kura Mhe. Mchengerwa ili aendelee kuwaletea maendeleo ya kweli.

” Naomba niwe mkweli, mimi nilikuja hapa Rufiji miaka ya nyuma, Rufiji haikuwa hivi ilivyo sasa, sasa hivi kumekuwa na maendeleo ya wazi yanayoonekana hivyo hatuna sababu ya kukinyima kura Chama Cha Mapinduzi”. Ameongeza huku akishangiliwa na wananchi waliohudhuria kongamano hilo.

Katika kikao Mhe. Wanu amewapokea wanachama wapya 153 kutoka vyama vya upinzani na wengine ambao wasio na vyama na kuwaomba kukipigia kura CCM.

“Nimefurahi sana ndugu zangu kwa zawadi mliyonipa ya kuniletea wanachama wapya, naamini siyo rahisi sana kwa wanachama kujiunga na vyama hasa katika kipindi hiki ila hawa ambao leo wamejiunga ni kwa sababu ya kuwa na imani kubwa na CCM”. Amesisitiza Mhe. Wanu

Naye mgombea wa Ubunge wa Jimbo hilo kwa CCM Mhe. Mohamed Mchengerwa amewashukuru wananchi kwa kuendelea kumchagua na kuwaomba safari hii kupiga kura za heshima kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kwake na kwa madiwani wote.

Aidha ameendelea kuwaomba wananchi kujitokeza kesho, Oktoba 20, 2025 kuja kupokea na kumshukuru Mhe Rais Samia Suluhu Hassan wakati anapokuja kwenye kampeni.

Pia ametumia fursa hiyo kuwafundisha wananchi namna ya kupiga kura kwa usahihi hapo Oktoba 29, 2025.

Imeelezwa kuwa Mhe. Mchengerwa ni miongoni mwa wabunge walioliletea maendeleo makubwa katika jimbo hili ambalo limeshakuwa na takriban wabunge kumi.

Baadhi ya maeneo ambayo ameyatendea haki ni pamoja na mapinduzi makubwa kwenye afya, elimu, umeme,maji, miundombinu ya barabara na taa hata masoko.