MGOMBEA Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema Mkoa wa Rukwa umepiga hatua kubwa za kimaendeleo kutokana na mipango ambayo Serikali imeiweka katika kuboresha maisha ya wananchi wa Mkoa huo.
Akizungumza leo Oktoba 19,2025 katika Uwanja wa Shule ya Sekondari Kizwite uliopo Sumbawanga Mjini mkoani Rukwa alipokuwa akihutubia maelfu ya wananchi katika mkutano wa kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29 ,2025 ,Dk.Samia Mkoa huo umepiga hatua katika Nyanja mbalimbali.
Amefafanua kwa mara ya kwanza alifika katika mkoa huo 1997 akiwa anafanyakazi katika shirika lisilokuwa la kiserikali liitwalo Rango ambapo alikaa miezi mitatu akifanya utafiti kuhusu mashirika yasiyokuwa ya kiserikali yaliyokuwepo mkoani Rukwa.
“Wakati huo mkoa huo ulikuwa nyuma kimaendeleo.Nimekuja mara ya pili Rukwa katika kampeni za mwaka 2015 nikiwa mgombea mwenza, nikakuta mambo yamebadilika kidogo lakini siyo hivi. Wakati ule baada ya kampeni nikarudi tena nikamkuta mkuu wa mkoa mama Stella Manyanya.
“Tukawa na ile kauli mbiu Rukwa, ruka kwa maendeleo. Angalau mkoa ukaanza kufunguka na wakati ule ndipo nilipokusanya kero zote za Rukwa nikazibeba kwenda kuzifanyiakazi,” amefafanua mgombea Urais Dk.Samia.
Ameongeza alirejea tena katika huo kwa ziara ya kikazi Julai mwaka 2025 ambapo akafungua na kuweka mawe ya msingi baada ya baadhi ya kero kufanyiwakazi.
“Kila nikifika katika mkoa huu nashuhudia maendeleo makubwa kwani ni tofauti na ilivyokuwa huko nyuma. Hata barabara zilikuwa hazipiti mvua ikinyesha.Sasa hivi unatoka Dar es Salaam asubuhi na Rukwa unaingia kwa wakati wako.
“Kama gari binafsi unafika mapema zaidi. Mambo makubwa yamefanyika.Nilipokuja mwaka Julai mwaka jana kazi nilizozifanya niliweka mawe ya msingi kwenye shule ya wasichana ya sayansi. Shule ile sasa ipo tayari kuchukua wanafunzi.”
Amesema Serikali imejenga shule maalimu za wasichana zenye mchepuo wa sayansi kwa lengo la kuongeza idadi yao katika fani hizo.
Amefafanua Serikali inahitaji madaktari, wahandisi na fani mbalimbali za sayansi .Watoto wa kike ambao walikuwa nyuma kwa muda mrefu wajiunge.
Pia, amesema kwamba Serikali imejenga shule maalum ya wenye vipaji elimu ambazo zinajengwa maeneo mbalimbali nchini.
Akieleza zaidi Dk.Samia amesema shughuli ya pili aliyoifanya katika Mkoa huo alipokuwa katika ziara ya kikazi ni kuzindua chuo cha ualimu Sumbawanga ambacho ni miongoni mwa vyuo vya walimu 35 vya serikali.
“Lengo ni kuongeza idadi ya walimu ambao watasambazwa maeneo mbalimbali nchini hususan mikoa ya pembezoni,”amesema Dk.Samia.
Pia amesema aliweka jiwe la msingi ujenzi wa kampasi ya Rukwa ya Chuo Kikuu cha Sayansi na teknolojia eneo la Kayengesa ambapo ujenzi upo katika hatua za mwisho kukamilika.
Dk.Samia amesema chuo hicho kitatoa fursa kwa vijana kupata ujuzi hatimaye taifa kuzalisha wanasansi wengi katika fani mbalimbali za teknolojia.
“Wakati ule niliweka jiwe la msingi chuo cha VETA Sumbawanga ambacho kitakuwa chuo cha nne ndani ya mkoa huu. Tayari kimeshachukua wanafunzi na kinatoa huduma.
“Nilizindua jengo la huduma za dharura katika Hospitali ya Wilaya Nkasi ikiwa ni sehemu ya uwekezaji katika sekta ya afya mkoani hapa. Nimeona kila mashine inayohitajika zipo na ni mashine za kisasa.”
Pia, amesema aliweka jiwe la msingi katika uwanja wa ndege ambao tayari njia ya kurukia imeshakamilika na hatua inayondelea ni ujenzi wa miundombinu mingine kuukamilisha.
Dk.Samia amesema kwa ujumla katika Mkoa huo Serikali imefanya mambo makubwa ya maendeleo katika miaka mitano iliyopita na imepanga mipango mikubwa zaidi ya kuleta maendeleo makubwa miaka mitano inayokuja kwa kuendelea kusogeza huduma mbalimbali karibu na wananchi.