Nondo za Maaskofu kuhusu amani

Dar/Moshi. Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Alex Malasusa, na Askofu wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo, Stephano Musomba, wamewataka Watanzania kudumisha amani, utulivu na ustahimilivu, huku wakisisitiza umuhimu wa kupenda kusema ukweli na kujiepusha na uongo.

Viongozi hao wamesema hayo kwa nyakati tofauti leo Jumapili, Oktoba 19, 2025, jijini Dar es Salaam na mkoani Kilimanjaro, na kusisitiza kuwa jamii inayozingatia ukweli hulinda amani na kila Mtanzania ana wajibu wa kuwa balozi wa amani katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, mwaka huu.

Akihubiri katika ibada maalumu ya maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Kanisa la KKKT Dayosisi ya Pare mkoani Kilimanjaro, Askofu Dk Malasusa amewataka Watanzania kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na kwamba kila mmoja aendelee kuliombea Taifa.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Askofu Dk Alex Malasusa

“Kipekee natumia fursa hii kuwasihi kwa unyenyekevu, tuende kwenye uchaguzi tukijua Mungu anatamani tuwe mabalozi wa amani, utulivu na ustahimilivu. Twende kwa amani na tuendelee kuiombea Tanzania yetu ifanye uchaguzi wenye utulivu,” amesema Askofu Malasusa.

Amesema baada ya uchaguzi, ni muhimu Serikali na wadau kufanya tathmini na majadiliano kuhusu namna bora ya kuendelea kulinda amani iliyopo nchini.

“Tumalize uchaguzi wetu vizuri kama ilivyo desturi ya Taifa letu, kisha tuketi tuzungumze. Mungu wetu anasema katika Biblia, ‘njooni tuzungumze.’ Tusiwe na papara, bali tuwe watulivu na tushiriki uchaguzi kwa amani,” ameongeza Askofu huyo.

Kwa upande wake, Askofu wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo, Stephano Musomba, akizungumza wakati wa Misa Takatifu ya Kipaimara katika Parokia ya Tegeta Kibaoni, Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, amewasisitiza waumini na Watanzania kwa ujumla kupenda kusema ukweli na kujiepusha na uongo kama njia ya kulinda amani.

“Tupende kusema ukweli na tujiepushe na uongo, maana tukifanya hivyo, amani ya nchi yetu itaendelea kutawala na kulindwa kwa wivu na kila mmoja wetu,” amesema Askofu Musomba.

Amesema tabia ya kukubali kukosolewa, mara zote humsaidia binadamu kukua kiroho na kimaadili, akibainisha kwamba mtu anapojiona mkamilifu na kukataa ushauri au maonyo, anapotea katika njia ya haki.

Askofu wa Jimbo Katoliki la Bagamoyo, Stephano Musomba

“Anayekataa kukosolewa na kujiona kama malaika, huyo yuko hatarini kupotea. Wapo wanaopenda kusifiwa tu na kuhongwa, wakiamini ndiyo njia bora, lakini si sahihi. Ukamilifu unapatikana pale mtu anapokubali kukosolewa na kuambiwa ukweli,” amesema Askofu Musomba.

Amehitimisha kwa kuwasihi waumini na Watanzania kuishi kwa kusema ukweli, kupendana na kutenda yaliyo mema kama mafundisho ya vitabu vitakatifu yanavyoelekeza, ili Taifa liendelee kuwa na amani na mshikamano.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango, aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho ya Jubilee ya miaka 50 ya Dayosisi Pare, amewataka Watanzania, hususan vijana, kudumisha amani na utulivu katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu, huku akisisitiza umuhimu wa kutumia haki ya kupiga kura kwa kuchagua kiongozi bora na si bora kiongozi.

Dk Mpango amesisitiza kuwa amani na utulivu uliopo nchini ni tunu muhimu inayopaswa kulindwa kabla, wakati na baada ya uchaguzi.

Akizungumzia simulizi ya Askofu Malasusa kuhusu alichoshuhudia nchini Congo, Dk Mpango amesema tukio hilo linaonesha wazi kuwa bila amani hata shughuli za kiroho haziwezi kufanyika kwa utulivu.

“Mmesikia Baba Askofu alichokutana nacho huko Congo. Katika mazingira ya vurugu na mapigano, hata ibada nzuri kama hii haiwezi kufanyika. Hivyo nawasihi sana Watanzania, hasa vijana, tuhakikishe uchaguzi wetu unafanyika kwa amani na utulivu ili nchi yetu iendelee kuwa kisiwa cha amani duniani,” amesema Dk Mpango.

Aidha, ametumia nafasi hiyo kuwasisitiza vijana kutumia teknolojia kwa manufaa, hasa katika kujipatia elimu itakayochangia maendeleo ya nchi kijamii na kiuchumi.

“Ulimwengu wa kidijitali umeleta fursa nyingi, lakini pia changamoto kama unyanyasaji mtandaoni, kusambazwa kwa picha na video zisizofaa, pamoja na ujumbe wa chuki. Napenda kusisitiza tutumie teknolojia kwa njia sahihi yenye tija kwa jamii,” amesema Dk Mpango.

Amesema maadhimisho ya Jubilee hiyo yanapaswa kuwa fursa ya kutafakari upya mwenendo wa dunia ya kidijitali na namna Watanzania wanavyoweza kuitumia kwa maendeleo ya Taifa.

Katika ibada hiyo, Dk Mpango pia amewasilisha mchango wa Rais Samia Suluhu Hassan wa Sh20 milioni kwa ajili ya kusaidia Dayosisi ya Pare katika ujenzi wa kiwanda cha maji ya kunywa.

“Ili kuunga mkono juhudi za Dayosisi hii, Rais Samia amenituma niwakilishe mchango wa Sh20 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha maji. Nimeelekeza wizara za Maji, Viwanda na Biashara, Afya, Tamisemi na Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, kuhakikisha wanatoa ushirikiano ili taratibu zote za vibali zikamilike kwa wakati,” amesema Dk Mpango.

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Pare, Askofu Charles Mjema

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Pare, Askofu Charles Mjema, ameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kutoa ajira za madaktari katika Hospitali ya Kilutheri ya Gonja, sambamba na kusaidia upatikanaji wa gari jipya la wagonjwa.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Askofu Mjema amesema Dayosisi ya Pare inatoa huduma katika eneo lote la Wilaya ya Same, ambalo linachukua takribani asilimia 40 ya Mkoa wa Kilimanjaro.

“Pamoja na suala la madaktari, tunaomba pia msaada wa gari la wagonjwa kwa kuwa lililopo kwa sasa ni chakavu na halikidhi ubora unaohitajika. Dayosisi haina uwezo wa kununua gari jipya,” amesema Askofu Mjema.

Historia ya Dayosisi ya Pare

Wakati wa maadhimisho hayo, ilisomwa historia ya dayosisi hiyo, ikieleza kabla ya kuanzishwa rasmi Juni 13, 1975, injili ilianza kuhubiriwa katika milima ya Upare tangu mwaka 1900 na wamisionari waliotoa mchango mkubwa katika kazi za injili, elimu na huduma za afya.

Miaka 34 baadaye, mwaka 1934, walipatikana wachungaji wa kwanza wazawa. Hata hivyo, kutokana na maandalizi ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia, baadhi ya wamisionari walilazimika kurejea kwao, na wachungaji wazawa waliendeleza kazi ya injili wakisaidiana na wamisionari waliorejea baada ya vita.

Mwaka 1943, idadi ya wachungaji wazawa iliongezeka, na mwaka huo huo Kanisa la Tanganyika ya Kaskazini lilianzishwa, huku eneo la Upare likiwa sehemu ya dayosisi hiyo.

Wazo la kuanzisha Dayosisi ya Pare lilipitishwa mwaka 1967 katika Mkutano Mkuu wa Kanisa uliofanyika Bukoba, na Juni 13, 1975, dayosisi hiyo ilizinduliwa, ikiongozwa na Askofu Dk Eliya Mshana (marehemu), akisaidiwa na Askofu Stephano Msangi.

Baada ya Askofu Mshana kustaafu mwaka 1994, Dayosisi ilipata uongozi mpya hadi mwaka 2008 alipostaafu Askofu aliyemrithi, na mwaka 2010 Askofu Charles Mjema alikabidhiwa uongozi wa dayosisi hiyo, nafasi anayoshikilia hadi sasa.

Imeandikwa na Janeth Joseph na Florah Temba (Moshi), Mariam Mbwana na Imani Makongoro (Dar)