WALIPOINGIA ndani ya kituo cha polisi, mzee Manyara, mzee Mangushi na Bi Faudhia walitakiwa kuandikisha maelezo na walianza kuhojiwa upya baada ya kila mmoja wao kukabidhiwa kwa askari wa kufanya naye mahojiano.
Kila mmoja alihojiwa jinsi alivyokuwa akimfahamu Muddy na kutoa maelezo yake ya kina, pia kueleza siku ya mwisho kuonana naye.
Kabla ya kumaliza mahojiano hayo, ikatakiwa picha ya Muddy na alitumwa ndugu yake mmoja kwenda kuifuata nyumbani.
Mwisho wa mahojiano kwa kila mmoja wao, waliambiwa mtu mmoja alitakiwa kubaki kwa ajili ya kulisaidia jeshi la polisi kutokana na wizi uliofanywa na Muddy.
Mtu aliyechaguliwa kubaki alikuwa ni mzee Mangushi ambaye gari lake lilitumika kwenye uhalifu.
Mzee Manyara na mkewe walijaribu sana kuwabembeleza polisi wasimshikilie mzee Mangushi huku wakiahidi kumtafuta mtoto wao, lakini ilishindikana na hata dhamana yake ilifungwa.
“Mpaka apatikane dereva aliyekuwa akiliendesha hili gari, ndipo huyu ataachiwa…” alisema Inspekta Haroub.
Kesi ilishakuwa ngumu, mzee Mangushi akaukumbuka ushauri aliopewa na mkewe wa kumtaka kunywa kahawa yake kwa kuwa polisi kulikuwa hakuna jambo dogo.
Ilimbidi mtoto mwingine wa mzee Manyara aende nyumbani kwa mzee Mangushi kumchukulia chakula. Kitendo hicho kilimshtua sana mke wa mzee Mangushi, Bi Swabra na kutaka kujua tatizo lilikuwa nini.
Bi Swabra alipohadithiwa kilichotokea ilimbidi naye kujikongoja hadi kituo cha polisi.
Kuzuiwa kwa mzee Mangushi kuliwachanganya sana watu wengi, jitihada kubwa zikafanyika za kuwasiliana na watu tofauti ili kuweza kumnusuru.
Kwanza walijitahidi kutaka kujua mahali ambako Muddy angeweza kupatikana. Hapo jitihada nyingi zilifanyika kwa kupiga simu kile sehemu ambayo walihisi Muddy angeweza kukimbilia.
Liliposhindikana hilo ikatafutwa njia ya kuwasiliana na watu wengine kwa ajili ya kumuombea dhamana mzee Mangushi. Wakapiwa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa katika jamii na hapo ndipo walipofanikiwa.
Hatimaye saa moja usiku, mzee Mangushi alitolewa kwa dhamana na kutakiwa kuripoti kituoni hapo kila baada ya siku moja.
“Kuripoti kwako kutakoma tu pale huyo dereva wako atakapopatikana…” Inspekta Haroub alimwambia.
***
Kabla ya kulitelekeza gari katika maeneo ya Kongowe, Muddy alihakikisha kila kitu kilikuwa vizuri. Alikuwa akimiliki simu ndogo, akaitoa laini yake na kuitupa.
Kisha alirudi barabara kubwa ya Morogoro na kutafuta usafiri na kufanikiwa kulipata lori lililomfikisha Segera, lori hilo lilikuwa likielekea Tanga mjini. Alitoa kiasi cha pesa na kumlipa dereva wa lori hilo.
Kutoka hapo alipanda gari ndogo iliyomfikisha Arusha mjini ambako alifanikiwa kupata gari nyingine iliyokuwa ikibeba abiria waliokuwa wakienda Namanga.
Saa nne usiku Muddy alifanikiwa kuvuka mpaka wa Tanzania na kuingia upande wa Kenya baada ya kufanya mahojiano mafupi na maofisa wa uhamiaji na kugongewa muhuri kwenye hati yake ya kusafiria.
Baada ya kuvuka mpaka, Muddy alishusha pumzi nzito na nafsi yake ilitulia na kuamini kuwa alikuwa katika mikono salama na mbali kabisa na mkono wa sheria wa Serikali ya Tanzania.
Mara baada ya kuvuka mpaka na akili yake ikatulia, hapo ndipo alipoanza kulisikia tumbo likidai haki yake. Alihisi njaa. Kitu cha ajabu njiani kote hakuhisi kula wala kunywa chochote, hakuhisi hamu ya kula wala kunywa kabisa pamoja na kwamba hakuwa amekula chakula cha mchana.
Muda wote wa safari alikuwa akihisi kama vile alikuwa akiandamwa na jinamizi la Kamba Makambo lililokuwa likimfuata nyuma yake.
Mara baada ya kuvuka mpaka ndipo alipoanza kutuliza akili yake, akatafuta mkahawa uliokuwa upande wa Kenya akanunua chai na mkate baada ya kuchota kiasi cha pesa za Kitanzania kutoka katika briefcase aliyomuibia Kamba na kuzibadilisha kuwa pesa za Kenya.
Chai aliyokunywa ilimsaidia kupunguza ukali wa baridi lililokuwa likiushambulia mwili wake kwa fujo katika maeneo hayo ya mpakani.
Aidha katika kulidhibiti zaidi baridi hilo, Muddy alinunua shuka la Kimasai kutoka kwa wafanyabiashara waliokuwa katika eneo hilo na kumfanya azidi kupata nafuu dhidi ya baridi kali pale alipojifunika.
***
Usiku huohuo, alipanda gari iliyomfikisha Nairobi. Mara baada ya kufika hakutaka kujifanya mjuaji, alibakia ndani ya gari hadi kulipopambazuka.
Alifanya hivyo kwa sababu alishakuwa na taarifa zote kuhusu uharifu uliokuwa umekithiri katika Jiji la Nairobi. Alitambua ingekuwa ni vigumu kwake kutembea usiku mwingi huku kutafuta usafiri wa kumpeleka kwa mwenyeji wake, Fashanu.
Fashanu alikuwa ni rafiki yake ambaye amekuwa naye maeneo ya Gerezani lakini maisha yake yalikuwa Nairobi baada ya kulowea katika nchi hiyo ya Kenya.
Mara kwa mara, Fashanu alipokuwa akirudi Tanzania kwa ajili ya mapumziko na kuwasilimia ndugu na jamaa zake alikuwa akiwapa habari za Nairobi kwamba ukiwa katika jiji hilo hupaswi kumuamini mtu yeyote.
“Hata dereva wa teksi nyakati za usiku usimuamini anaweza kukufanyia kitu mbaya…
“Dereva wa teski anaweza kukuibia kwa kukuzungusha kwa kukupitisha njia za mbali, wakati mnapokwenda ni karibu tu ili umlipe kiasi kikubwa cha pesa,” aliwahi kusisitiza Fashanu wakati alipokuwa akiwaeleza kuhusu maisha ya Nairobi.
“Kule hakuna wema wala ustaarabu, sio kama huku kwetu, mtu anaweza kukuelekeza sehemu bila ya shida yoyote.
“Tena unapokuwa Nairobi mchana unatakiwa utembee kwa ukakamavu…usikimbie lakini usitembee kama uko Gerezani… unatakiwa umwangalie kwa umakini mtu aliyekuwa mbele yako, mtu wa kulia, wa kushoto na nyuma yako… wakati wowote mjini kinaweza kuwaka…” aliongeza Fashanu.
Aidha, Fashanu aliwahi kuwaambia jamaa zake, kwamba Tanzania, mtu akivaa suti na kushika briefcase anaheshimika lakini kwa Nairobi mtu huyo anaweza kukukaba na kukuibia.
“Usishangae hata kwenye hiyo briefcase amejaza mawe,” alisema Fashanu na kuwafanya watu wote waliokuwa wakimsikiliza wacheke.
Muddy aliyakumbuka maneno yote aliyoyasikia kutoka kwa Fashanu na aliyazingatia kwa umakini mkubwa. Alisubiri hadi kulipopambazuka, ndipo alipokodi teksi iliyomfikisha katika kitongoji cha Majengo, karibu kabisa na Msikiti wa Majengo ni hapo sehemu ambayo Fashanu aliwaambia alikuwa akipatikana mara kwa mara.
Baada ya kuwaulizia watu wawili watatu, Muddy alifanikiwa kumpata Mtanzania mwenzake aliyekuwa akiishi Majengo na alikuwa akimfahamu mwenyeji wake.
Muddy aliomba kutaka kupelekwa alipokuwa Fashanu, lakini haikuwa rahisi kama alivyokuwa akitarajia, ilimbidi kujieleza sana kuhusu alivyokuwa akimfahamu mtu huyo. Mwenyeji huyo mwenye asili ya Tanzania aliyempokea Muddy katika maeneo ya Majengo alimuuliza maswali mengi Muddy kwa kuwa alikuwa akimfahamu Fashanu alikuwa ni mtu wa aina gani.
Fashanu alikuwa mtata na hakuwa mtu ambaye angeweza kufikika kwa urahisi na mtu yeyote yule.
“Unamfahamu vipi Fashanu?” yule Mtanzania aliyekuwa akiishi Majengo alimuuliza.
“Ni jamaa yangu, tulikuwa tunaishi naye Karikoo…”
“Mlikuwa mkiishi Kariakoo maeneo gani?”
“Gerezani…”
“Oooh sawa… mimi pia nilikuwa nikiishi Dar es Salaam lakini ni maeneo ya Ilala Shariff Shamba…”
“Napafahamu, nilikuwa nakuja sana kucheza mpira maeneo yale…” Muddy alijieleza.
“Ulicheza na akina nani…?”
Muddy akaanza kuwataja baadhi ya watu ambao hata Mtanzania mwenzake huyo aliyyekutana naye maeneo hayo ya Majengo katika Jiji la Nairobi alikuwa akiwafahamu.
“Ni kweli hao uliowataja ninawafahamu…” alijibu mwenyeji huyo na kukubali kwamba Muddy alikuwa mtu mwema na hakuwa na madhara yoyote kwa Fashanu.
Hata hivyo, Mtanzania huyo, ilimbidi kwanza kufanya mawasiliano na baadhi ya watu ili kuweza kumpata Fashanu na kuzungumza naye.
Kwasababu alimfahamu Fashanu, mtu ambaye alikuwa na matukio mengi ya kumsababishia kesi kutokana na uhalifu aliokuwa akiufanya. Mtu mwenye ukatili na namna yake ya maisha na hasa katika masuala ya utafutaji wa pesa.
Pamoja na kuwa msaada kwa baadhi ya watu, Fashanu alisifika kwa kuwa tayari kufanya jambo lolote lile katika kulinda heshima yake au kutetea udhalimu alikuwa akikusudia kuufanya.
Tangu alipojiingiza katika magenge ya uhalifu alihusishwa katika matukio mengi yaliyofanyika katika Jiji la Nairobi na maeneo mengine katika miji ya Nakuru, Kisumu na Mombasa.
Fashanu Mtanzania aliyelowea katika nchi ya Kenya hususan katika la Jiji la Nairobi, aliingia katika nchi hiyo akiwa mchezaji wa mpira wa miguu.
Hadi alipofikia hatua ya kuachana na mpira hakuna mtu aliyekuwa akilijua jina lake halisi zaidi ya hilo la Fashanu ambalo alilolipata kutokana na kipaji chake kikubwa cha kusakata soka na kulinganishwa na mchezaji wa soka aliyekuwa akilimiliki jina hilo.
Kipaji chake kilimpa jina kubwa katika Jiji la Dar es Salaam na baadaye alipata ushawishi kutoka kwa marafiki zake waliomtaka kwenda kucheza soka katika nchi ya Kenya, kwasababu nyakati hizo soka la Kenya lilikuwa juu na ilikuwa rahisi kupata njia ya kwenda kusakata soka katika nchi za Ulaya.
Fashanu alisafiri hadi Nairobi na kuanza kutafuta maisha yake kwa kutegemea kusakata mchezo wa soka.
Kwa kiasi kikubwa alikubalika katika klabu alizokuwa akicheza na kupata mafanikio makubwa sana lakini sifa zilimlevya na kuanza kuendekeza starehe za kila namna.
Mtoto wa Mjini – 6
