Kilimanjaro International Marathon 2026 Ilivyozinduliwa Dar – Global Publishers

Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mh. Edward Mpogolo (wa tatu kulia) pamoja na Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania, Khensani Mkhombo (wa tatu kushoto) wakizindua rasmi mbio za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon 2026 Jijini Dar es Salaam. Wengine kutoka kushoto ni mwakilishi kutoka Baraza la Taifa la Michezo, Charles Maguzu, Meneja wa CRDB Kanda ya Dar es Salaam, Muhumuliza Buberwa, Meneja Mawasiliano wa YAS, Christina Murimi na Mkurugenzi wa Michezo Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Boniface Tamba.

Toleo la 24 la Mbio za Kimataifa za Masafa Marefu za Kilimanjaro Premium Lager limezinduliwa rasmi leo Ijumaa wakati wa hafla iliyofanyika katika Hoteli ya Johari Rotana jijini Dar es Salaam, tukio ambalo limekuwa likisubiriwa kwa hamu.

Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania, Khensani Mkhombo alizungumza wakati wa uzinduzi huo.

Akizindua toleo hili la Kili Marathon, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe Albert Chalamila, ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala Mh. Edward Mpogolo, alipongeza kufanyika kwa tukio hili, na kwa hatua iliyokwishapigwa kwa miaka mingi, hasa katika kuinua utalii wa michezo, jambo ambalo ni mada ya wakati huu duniani kote.

Meneja Mawasiliano wa YAS, Christina Murimi akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Alitoa changamoto kwa waandaji wengine kuiga mbio za masafa marefu za Kilimanjaro Premium Lager, ambazo zimedumu kwa miaka 24 sasa na kumekuwa na ushirikiano mzuri na Serikali.

Meneja wa CRDB Kanda ya Dar es Salaam, Muhumuliza Buberwa akizungumza wakati wa uzinduzi huo.

“Nimefahamishwa kwamba ni kupitia Mbio za Kimataifa za Masafa Marefu za Kilimanjaro Premium Lager, ambapo washiriki mahiri kama mshindi wa Mashindano ya Riadha Duniani yaliyofanyika Tokyo mwaka huu, Alphonce Simbu, alipata uzoefu wa kukimbia dhidi ya wanariadha wengine mahiri na kuweza kutambulika kwa kipaji chake cha ajabu, na kupata mafanikio makubwa,” alisema Mhe Chalamila.

Alieleza kwamba hili ni jambo la kusifika “Natunatumai kwamba ushindi wake utawatia moyo wanariadha wengine kushiriki katika mbio za Kimataifa za Masafa Marefu za Kilimanjaro Premium Lager na kusaidia kukuza vipaji vyetu vya ndani na kuendelea kutoa mabingwa zaidi kwa Tanzania.”

Alibainisha kwamba mbio za marathoni zinaonekana kuwa tukio kubwa zaidi la kimichezo nchini, hivyo ni jukwaa zuri la kutangaza utalii.

“Tunajivunia mbio za Kimataifa za Masafa Marefu za Kilimanjaro Premium Lager kwa kuwa zinaonekana kuwa moja ya matukio makubwa ya kimataifa katika ukanda huu kwa kuwakutanisha washiriki zaidi ya 13,200 na idadi sawa ya watazamaji kutoka zaidi ya nchi 60, na wote hawa ni watalii. Hii ni hatua kubwa,” alisema.

Aliongeza kwamba tukio hilo lina mchango mkubwa katika uwezeshaji wa kiuchumi, kwani wafanyabiashara wengi hustawi katika kipindi hiki kutokana na wingi wa watu wanaotembelea Moshi na miji ya jirani wakati wa mbio za masafa marefu.

“Nawapongeza wadhamini wote wakiongozwa na Kilimanjaro Premium Lager (Mdhamini Mkuu wa Mbio za kilomita 42), YAS (Kili Mdhamini wa kilomita 21), Benki ya CRDB (Mdhamini wa Mbio za Burudani za kilomita 5).

Wadhamini Rasmi – Kilimanjaro Water na TPC Sugar. Wabia Rasmi – GardaWorld Security, Toyota Tanzania, Columbia Sportswear, Simba Cement na ALAF Limited. Wasambazaji Rasmi – Salinero Hotel, Kibo Palace Hotel Arusha na Keys Hotel, Moshi. Bila nyinyi isingekuwa rahisi haya yote kufanyika,” alisisitiza.

Mhe Chalamila alitoa wito kwa washiriki na watazamaji kutumia msimu wa mbio za kimataifa za masafa marefu kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii, vikiwemo Mlima Kilimanjaro, Mbuga za Wanyama Serengeti, Ngorongoro, Zanzibar na maeneo mengine, ambayo ni vivutio vya watalii Tanzania.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Masoko wa Kampuni ya Bia Tanzania Bi Khensani Mkhombo alisema wanajivunia kupitia Kilimanjaro Premium Lager, kudhamini tukio hili kwa miaka 24 sasa, na kuifanya kuwa moja ya wadhamini wa muda mrefu nchini Tanzania, na kuongeza kwamba kwa miaka hii wamehamasishwa kusaidia utalii na utamaduni wa Watanzania kwa jumla – ambao tukio hili linasaidia kuukuza.

Alitoa wito kwa washiriki kujiandikisha kwa wakati, kwani usajili utafunguliwa Jumatatu ijayo Oktoba 20 na wanaweza kufanya hivyo kupitia ukurasa rasmi wa tovuti www.kilimanjaromarathon.com, na kupitia Mixx by YAS.

Bi Mkhombo alisema washiriki watarajie wikendi ya shughuli za kufurahisha na kwamba wakimbiaji, wageni na wakazi wa Kilimanjaro katika kipindi hiki, wapange kukaa kwa muda mrefu Moshi, na kufurahia wa Kilimanjaro Premium Lager.

Meneja Mawasiliano wa YAS, Christina Murimi alisema: “Yas inajivunia kurejea kama Mdhamini Rasmi wa Mbio za Kimataifa za Kilomita 21 Sasa katika mwaka wake wa 11, ushirikiano huu unaonyesha dhamira yetu ya kuunganisha na kuwezesha jamii kote Tanzania. Kama mbia katika maendeleo ya kitaifa, tunaendelea kuunga mkono kukuza vipaji, na utalii, kusaidia mipango ya afya na ya uchumi, yote yakiendeshwa na teknolojia ya 4G na 5G yetu.”

Aliongeza: “Nawaalika wote kujumuika nasi, kukimbia, kuungana na kusherehekea ari ya Tanzania na Yas kwenye mbio za Kimataifa za Masafa Marefu Kilimanjaro 2026.”

Waandaaji wa tukio hili walitoa wito kwa wakimbiaji kununua tikiti zao mapema ili kuepuka usumbufu dakika za mwisho, na pia kujipa muda wa kutosha kujiandaa kwa tukio lenyewe litakalofanyika Machi 22, 2026.

Nafasi za ushiriki wa mashindano ni chache na wakimbiaji wanakumbushwa kwamba wa kwanza kufika ndiye atakayehudumiwa kwanza. Idadi inayotakiwa ikijaa, mfumo wa kuingia utafungwa.

Mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager, zitakazofanyika Jumapili Machi 22, 2026 katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU). Zimeandaliwa na Kilimanjaro Marathon Company Limited. Kampuni ya Wild Frontiers Events itahusika na kutangaza shughuli za usafiri wote wa ndani wa tukio hili.