Dar es Salaam. Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewasilisha rasmi taarifa ya uchunguzi kuhusu mgogoro wa umiliki wa kiwanja namba 189 kilichopo eneo la Msasani Beach, baina ya mjane Alice Haule na Mohamed Yusufali jijini Dar es Salaam, kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila.
Akizungumza leo Oktoba 20, 2025 kwa niaba ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Kamishna Msaidizi wa Ardhi Mkoa wa Dar es Salaam, Shukurani Kyando, amesema uchunguzi huo umefanyika kufuatia maagizo ya Mkuu wa Mkoa yaliyotolewa wiki mbili zilizopita, ambapo timu maalum iliundwa kupitia nyaraka, kuhoji wahusika na kuchambua mwenendo mzima wa umiliki wa kiwanja hicho.
Kamati pia imebaini kuwa mikataba ya mkopo na mauziano kati ya marehemu Lugaibula na Yusufali haikuwahi kuwasilishwa rasmi wizarani kama taratibu zinavyotaka.
Aidha, shahidi aliyekuwa wakili wa miamala hiyo alikiri mbele ya kamati kuwa marehemu Lugaibula ndiye aliyekuwa anaratibu mchakato wa kupata saini ya mkewe, Alice ingawa baadaye hakurejesha nyaraka hizo kwa ajili ya uthibitisho.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Kamati imehitimisha kuwa umiliki wa kiwanja namba 189 Msasani Beach umekuwa na utata wa kisheria, na inashauri mamlaka husika kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria za ardhi namba 4 na 5 za mwaka 1999, ili kurejesha haki kwa wahusika wote.
“Tumeona umuhimu wa kutoa taarifa hii kwa umma ili kuweka uwazi na kuondoa mkanganyiko kuhusu nani mmiliki halali wa kiwanja hicho. Hatua zaidi zitachukuliwa baada ya uamuzi wa mamlaka husika,” amesema Kyando.
Kutokana na maelezo hayo Kyando alimkabidhi Chalamila hati ya kiwanja ambapo mkuu huyo alimkabidhi mjane Alice.
Endelea kufuatilia Mwananchi.