Dar City yaweka historia, yafuzu 16 bora Basketball Africa League

Mwakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Basketball Africa League (BAL), Dar City, imefuzu  hatua ya 16 bora ya mashindano hayo ya bara la Afrika, ambayo yanatarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu jijini Nairobi, Kenya.

Dar City ilijihakikishia nafasi hiyo baada ya kuonyesha kiwango cha juu katika mashindano ya Road to BAL yaliyofanyika katika Shule ya Kimataifa ya Tanganyika (IST), jijini Dar es Salaam.

Mabingwa hao wa Tanzania walitawala hatua ya mchujo kwa kushinda mechi zao zote mbili, na kuongoza kundi lao na kufuzu kwa hatua inayofuata.
Katika mchezo wao wa ufunguzi, Dar City ilitoa burudani kwa kuichapa timu ya Djabal Basket Iconi ya Comoro kwa ushindi wa pointi 102–50.

Timu hiyo ilionyesha ushirikiano mzuri na uwezo mkubwa wa kumalizia mashambulizi, na kuwafurahisha mashabiki wengi waliojitokeza kwa wingi kuwaunga mkono.

Katika mchezo wao wa pili, Dar City iliendeleza ubabe wao kwa kuifunga timu ya Namuwongo Blazers ya Uganda kwa pointi 83–70, na hivyo kufuzu rasmi kwa hatua inayofuata ya mashindano hayo ya bara.

Akizungumza na gazeti la Mwanaspoti baada ya ushindi huo, kocha mkuu wa Dar City, Mohamed Mbwana, amewapongeza wachezaji wake kwa nidhamu, mshikamano, na kujituma kwao katika kipindi chote cha mashindano. Amesema mafanikio hayo ni matokeo ya maandalizi mazuri pamoja na uwekezaji unaoendelea wa klabu katika vipaji vya ndani ya nchi.

“Tunafurahia kufuzu kwa hatua ya 16 Bora. Wachezaji wamefanya kazi kwa bidii na matokeo yao yameiletea Tanzania heshima kubwa,” alisema Mbwana.

“Mipango mizuri na uwekezaji wa uongozi wetu imechangia sana mafanikio haya na kutufanya kuwa timu yenye nguvu katika mashindano ya ndani.”

Dar City ndio mabingwa watetezi wa Ligi ya Mpira wa Kikapu ya Dar es Salaam (BDL), na mafanikio haya ya hivi karibuni ni hatua nyingine muhimu katika kuimarisha nafasi yao kwenye medani ya kikapu ya kanda hii.

Mbwana aliongeza kuwa ni muhimu kikosi chake kubaki makini na kujiandaa vizuri kwa hatua inayofuata huko Nairobi, ambako wanatarajiwa kukutana na timu kali zaidi kutoka mataifa mbalimbali barani Afrika.

“Tunajua changamoto zinazotukabili ni kubwa. Wachezaji watapumzika kwa wiki mbili ili kupata muda wa kuwa na familia zao kabla hatujaanza tena mazoezi ya kujiandaa na mashindano ya Nairobi,” aliongeza.

Mashindano ya BAL, yanayoandaliwa kwa pamoja na NBA na FIBA Africa, yanaendelea kukua na kuwa jukwaa kuu la mpira wa kikapu barani Afrika, yakitoa fursa kwa vilabu vya Kiafrika kuonyesha vipaji vyao katika ngazi ya kimataifa.

Dar City kufuzu kwao ni fahari kwa Tanzania na ni hatua nzuri kuelekea kutambulika zaidi katika ramani ya mpira wa kikapu barani Afrika.