Dar es Salaam. Upande wa mashtaka (Jamhuri) katika kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Tundu Lissu, umejibu pingamizi la Lissu kuhusu Mahakama kupokea video ya hotuba yake yenye maneno yanayodaiwa ya uhaini ikieleza kuwa, hoja zake hazina mashiko ya kisheria.
Leo Jumatatu Oktoba 20, 2025 Jamhuri imefafanua hoja moja baada ya nyingine na kuhitimisha kwa kuomba Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, ilitupilie mbali pingamizi hilo la Lissu kwa madai halina mashiko ya kisheria.
Katika kesi hiyo, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini akidaiwa kutoa maneno ya kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume na kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu,
Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, alitoa maneno ya kuitishia Serikali na kuonesha nia hiyo kwa kuchapisha meneno hayo katika mitandao ya kijamii kuwa:
“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”
Kesi hiyo inayosikilizwa na na jopo la majaji watatu linaloongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru akishirikiana na majaji, James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde katika hatua ya ushahidi wa Jamhuri, ikiwa ni shahidi wa tatu.
Shahidi huyo wa tatu ni Mkaguzi wa Jeshi la Polisi aliyejitambulisha kwa jina la Samweli Eribariki Kaaya (39), mtaalamu wa picha, kutoka kitengo cha Picha Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam.
Katika ushahidi wake wa msingi, ameeleza kuwa Aprili 8, 2025 alipokea flash disk na memory card zenye video ya Lissu yenye maudhui yanayodaiwa kuwa ya uhaini, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Dar es Salaam kuchunguza uhalisia wake.
Shahidi huyo ameeleza kuwa, baada ya uchunguzi wake, alibaini video hiyo ni halisi, akaandika ripoti ya uchunguzi wake.
Baada ya kuvitambua vielelezo hivyo alivyovipokea na kuvifanyia uchunguzi, aliiomba Mahakama izipokee picha hizo (video) ziwe kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.
Hata hivyo, Lissu alipinga kupokewa kwa vihifadhi data hivyo vyenye video yake kuwa kielelezo akibainisha sababu nne.
Kwanza Lissu alidai kuwa upokewaji wa video hizo kuwa kielelezo umekiuka kifungu cha 263(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), Marejeo ya Mwaka 2023, akidai kuwa, video hazikuwahi kuoneshwa kwenye Mahakama ya Ukabidhi (committal court), Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam Kisutu.
Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga amesema ili kuona kama video hizo zilioneshwa, Mahakama inapaswa kupitia kumbukumbu za wakati wa mwenendo kabidhi, na si maelezo ya mshtakiwa yasiyo chini ya kiapo.
Wakili Katuga amesema mtu anayejitetea wakati mwingine anatumia kila mbinu.
Amedai kuwa, katika ukurasa wa 92 wa kumbukumbu za mwenendo kabidhi, Mahakama ya Ukabidhi (Kisutu) imeeleza wazi kuwa nyaraka hizo sambamba na video zilichezwa na kusomwa kwa mshtakiwa.
“Mwenendo anao na alikuwa na nafasi ya kusoma, lakini hakuna hata siku amewahi kulalamikia kuwa una makosa (ushahidi),” amesema Wakili Katuga.
Amesema katika kuthibitisha hayo, mshtakiwa anakiri kuwa maneno hayo yaliyoko katika vielelezo na kwenye video aliyasema kwenye mkutano na akahoji kama ndio yanatengeneza uhaini na kwamba, ameyasema mara nyingi.
Pia, ameeleza kuwa mshtakiwa amesema vielelezo hivyo hana shida navyo viletwe tu hatavipinga na kwamba, katika kuthibitisha uwongo wake, ndio maana hakuiandika Mahakama katika ukurasa wa 93.
Amesema kumbukumbu za Mahakama ya Ukabidhi imeeleza wazi kuwa kifungu cha 262 kimetekelezwa.
Kuhusu hoja ya pili kuwa video hizo ziliwasilishwa kabla ya ripoti ya uchunguzi wake, Wakili Katuga amedai kuwa, mshtakiwa hajaielekeza Mahakama kuwa ni sharti gani la kisheria, mtaalamu aliyefanya uchunguzi lazima kwanza awasilishe ripoti ya uchunguzi wake kabla ya kielelezo alichokifanyia kazi.
Wakili Katuga amedai kuwa, amefanya utafiti kuona ni wapi sheria inaeleza kuwa ripoti ndio itangulie, lakini hakuna sheria mahsusi inayoelekeza kuwa, pale shahidi mtaalamu amefanya uchunguzi na kuandika taarifa lazima kwanza awasilishe ripoti yake.
Amesema vifungu vya sheria alivyovirejea mshtakiwa vya 216(1), 217(1), 218(1), 219(1) na 220(1) vya CPA, havijasema alichokisema mshtakiwa, ianze kutolewa ripoti ndio vifuate vielelezo.
Amerejea katika shauri moja la rufaa ya Jinai namba 413/20216 katika Mahakama ya Rufani, mkemia alianza kuwasilisha mahakamani dawa alizozifanyia uchunguzi kabla ya ripoti yake.
“Kwa hiyo waheshimiwa majaji, kipi kinaanza inategemea na prosecution plan (mpango wa upande wa mashtaka),” amesema Wakili Katuga.
Hoja ya tatu, kwamba shahidi hana mamlaka kuwasilisha vielelezo mahakamani.
Wakili Katuga amesema mshtakiwa alirejea vifungu 216 mpaka 221 vya CPA, lakini akasema kuwa vinazungumzia mambo mengine.
Wakili Katuga ameeleza vilelezo ambavyo shahidi anaomba kuvitoa ni vile alivyovifanyia kazi na kwamba, amejieleza kuhusu elimu, ujuzi na jinsi alivyovifanyia kazi na ameomba kutoa ripoti ya kazi.
Hivyo, amesisitiza Mahakama ya Rufani katika uamuzi wa mashauri mbalimbali, imetoa sifa ambazo Mahakama inapaswa kuziangalia kabla ya kupokea ushahidi huo, likiwamo la DPP dhidi ya Shaibu Mohamed na wenzake sita rufaa ya Jinai namba 74/2016.
Katika shauri hilo, Mahakama imebainisha sifa tatu kuwa kielelezo na uhusiano na kesi (relevance) materiality (umuhimu) na ustahilifu kisheria (compentency).
“Tunasema shahidi wetu PW3 pamoja na vielelezo hivi anakidhi matakwa ya kanuni kwa kuwa, kielelezo kinachotakiwa kutolewa na shahidi anayehusika anastahili,” amesema Wakili Katuga.
Amesisitiza kuwa, anastahili kwa sababu kwanza, ameieleza Mahakama kuwa ndiye aliyefanyia kazi vielelezo hivyo, pili ameeleza utaalamu akirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika uamuzi wa mashauri mbalimbali.
Amesema kuwa, ustahilifu wa shahidi kutoa kielelezo, ni kuwa na ufahamu wa kitu husika kama vile mmiliki, mtunzajii au aliyekifanyia kazi.
Amesema shahidi katika ushahidi wake ameeleza kuwa, mtaalamu wa picha za mnato na jongefu, ametangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) namba 516 la mwaka 2022 na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Sylvester Mwakitalu kuwa mchunguzi wa picha na mtoa taarifa.
Katika hoja ya nne ya kutokuwa na mnyororo wa utunzaji vielelezo, hasa kwa kutokuwepo nyaraka za makabidhiano, Wakili Katuga amedai kuwa mnyororo wa utunzwaji vielelezo hauthibitishwi na shahidi mmoja tu.
Pia, amedai hiyo si moja ya sifa tatu zilizoainishwa na Mahakama ya Rufani katika upokeaji wa vielelezo.
Katuga pia, amesisitiza suala la mnyororo wa utunzwaji kielelezo ni kwa ajili ya Mahakama, kujiridhisha tu kuwa hakijachezewa bali ni halisi, akisisitiza kuwa, hilo alithibitishwi na shahidi mmoja na kwamba pia ni suala la kiushahidi.
“Kwa hiyo hii hoja hafifu isiyo ya kisheria na ya kupoteza muda wa Mahakama kwa hiyo mlitupe pingamizi hili maana mapingamizi yanaletwa kwa mujibu wa sheria siyo yanaletwaletwa,” amesema Wakili Katuga.
Baada ya majibu ya Jamhuri dhidi ya hoja za Lissu, naye atajibu hoja za Jamhuri na kuiachia Mahakama kuamua.
Endelea kufuatilia kesi hi