Watumishi wa umma 34 waliofukuzwa kazi, warudishwa kazini

Dodoma. Tume ya Utumishi wa Umma imewarudisha kazini jumla ya watumishi 34 waliofukuzwa na waajiri wao na wengine tisa mashauri yao yamerudishwa ngazi ya chini ili yakasikilizwe upya.

Aidha, tume hiyo imeridhia watumishi 38 kuendelea na adhabu kama walivyopewa na mamlaka za ajira, 10 kati yao rufaa zao zilikataliwa kwa sababu zilikatwa nje ya muda huku rufaa mbili zikiahirishwa ili zikafanyiwe kazi na sekretarieti.

Takwimu hizo zimetolewa leo Jumatatu Oktoba 20, 2025 na Kaimu Katibu wa tume ya Utumishi wa Umma, John Mbisso aliyesema jumla ya malalamiko 15 yalifikishwa mbele yao na sita yalikubaliwa,  sita yalikataliwa na mengine matatu yametupiliwa mbali kwa sababu maalumu.

Mbisso amesema tume hiyo ilikutana jijini Dodoma kuanzia Septemba 29 hadi Oktoba 17, 2025 chini ya Mwenyekiti wake, Jaji Mstaafu Hamisa Kalombola na kupitia, kujadili na kuamua rufaa na malalamiko ya watumishi wa umma 108 yaliyowasilishwa mbele yake.

Septemba 26, 2025, Mbisso aliitisha mkutano na waandishi wa habari, akaeleza namna tume hiyo inavyokwenda kusikiliza rufaa na malalamiko ya utumishi wa umma, lakini akasisitiza kwenda kutenda haki zaidi kwa watumishi kwa kulenga kutoa ushauri, urekebishi na kusimamia utoaji wa haki.

Ofisa Sheria wa Tume ya Utumishi wa Umma Hussein Mussa

Katibu huyo amesema katika rufaa hizo, serikali za mitaa ziliongoza kuwa na kesi nyingi zilizotoka kwa watendaji wa kata, vijiji na mitaa ambapo tume ililazimika kuwaita warufani 18 na warufaniwa watatu ili kutoa ufafanuzi wa ziada kuhusu hoja zao na majibu.

“Lakini katika rufaa zilizowasilishwa mbele ya tume, makosa yaliyoonekana kutendwa zaidi ni ukiukaji wa maadili ya utumishi wa umma, utoro kazini, kughushi vyeti na kutoa taarifa za uongo, uzembe wa kushindwa kutekeleza majukumu ipasavyo na wizi wa mali za umma,” amesema Mbisso.

Ofisa Sheria wa tume hiyo, Hussein Mussa amesema watumishi walioshinda rufaa zao wanatakiwa kurudishwa kazini mara moja na kulipwa stahiki zao na kama waajiri wao watakuwa na hoja zingine, wanatakiwa kukata rufaa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mussa ametaja haki za watumishi tisa ambao mashauri yao yamerudishwa kuanza upya kuwa wanatakiwa kurudishwa kazini kwa mujibu wa sheria na walipwe mishahara yao ndipo waanze kusikilizwa upya kesi zao.

“Hakuna hasara kwa Serikali kama ambazo watumishi wanapata kwa kupoteza haki za msingi na haki za asili, lakini zisipofuatwa hapo ndipo inakuwa hasara na mfano hawa wanaotakiwa kusikilizwa upya huwa hakuna namna, lazima warudishwe kazini kwanza na kulipwa mishahara yao ndipo waanze kusikiliza mashauri yao kuanzia mwanzo kwani sheria inataka hivyo,” amesema Mussa.

Mwanasheria huyo amesisitiza mamlaka za ajira kuacha kuwafukuza watumishi bila kufuata utaratibu kwani wanawaumiza watu ambao wengi huonekana kama walionewa kutoka kwenye mamlaka za ajira ngazi ya chini.