MAHAKAMA Kuu Masijla Ndogo Dar es Salaam Oktoba 22,2025 inatarajiwa kutoa uamuzi wa pingamizi la juu ya kupokelewa au kutokupolelewa kwa vielelezo vya shahidi wa tatu wa Jamhuri katika kesi ya uhaini inayomkabii Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Tundu Lissu.
Hatua hiyo imefikiwa leo Oktoba 20,2025 na jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Dunstan Ndunguru akisaidiwa na Majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, baada ya jamhuri kumaliza kujibu pingamizi lenye hoja nne lililowasilishwa na Lissu.
Mapema leo Oktoba 20, 2025, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali Nassoro Katuga ulijibu mapingamizi hayo na kuiomba mahakama kuyatupilia mbali kwa kuwa hayana msingi wa kisheria na yanalenga kuchelewesha mwenendo wa kesi.
Akijibu mapingamizi hayo moja baada ya lingine, Wakili Mkuu wa Serikali Nassoro Katuga amedai kuwa vielelezo vinavyolalamikiwa ni flash na memory card zenye video ambazo ni ushahidi wa kielektroniki kwa mujibu wa kifungu cha 3 cha Sheria ya Ushahidi Sura ya 6 iliyofanyiwa marejeo mwaka 2023.
” Kwa mujibu wa sheria hiyo, video hizo zinachukuliwa kama nyaraka, na kwa msingi huo vilisomwa ipasavyo wakati wa hatua ya awali Kisutu….Mahakama inajiridhisha kupitia kumbukumbu zake, si kwa hoja zisizo na kiapo kama anazowasilisha mshtakiwa,”
Amedai nyaraka husika zilipelekwa na zipo katika ukurasa wa 92 hadi wa 93 wa Mwenendo wa kesi katika maelezo ya mashahidi (committal) ya tarehe 18 Machi 2025.
Akijibu pingamizi kuhusu kupokelewa kwa vielelezo vya shahidi wao ambavyo ni flash diski na kadi ya kumbukumbu ‘Memory Card’ Katuga amedai kuwa ni sahihi kwamba kifungu cha 263(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kinataka vielelezo na maelezo ya mashahidi yasomwe katika Mahakama ya Ukabidhi. (Kisutu)
Amedai kuwa, vielelezo vinavyopingwa na mshtakiwa ni vya kielektroniki vinavyotafsiriwa kama nyaraka kwa mujibu wa Kifungu cha 3 cha Sheria ya Ushahidi Sura ya 6, Marejeo ya 2023, kwa maana hiyo nyaraka hizo zinahusiana na flash disk na memory card zenye video zinazohusiana na kesi, ambazo mahakama inaweza kujiridhisha uhalisia wake kupitia kumbukumbu za Kisutu badala ya kutegemea hoja zisizo chini ya kiapo.
Amefafanua kuwa kumbukumbu za Mahakama ya Kisutu zinaonyesha vielelezo hivyo vilitajwa ipasavyo, na kwamba Lissu hana hoja ya kisheria kuzuia upokelewaji wake.
Akijibu hoja ya kwamba vielelezo hivyo vimetolewa kabla ya wakati, Katuga amedai hakuna sheria mahususi inayoelekeza kuwa shahidi mtaalamu ambaye amefanya uchunguzi na kuandaa taarifa ni lazima aanze kutoa taarifa ndipo atoe vielelezo, kwani utoaji wa vielelezo hutegemea mazingira ya kila kesi na namna inavyoendeshwa.
Amedai kuwa shahidi Samwel Kaaya ni mtaalamu aliyesajiliwa kisheria na kutangazwa katika Gazeti la Serikali, hivyo ana sifa zote za kuwasilisha vielelezo hivyo.
“Kwa mujibu wa Kifungu cha 52 na 70(1) cha Sheria ya Ushahidi, ni jukumu la mahakama kuamua kuamini au kutokuamini ushahidi wa mtaalamu baada ya kumskiliza, na si jukumu la mshtakiwa kumvua sifa.” amesema Katuga
Kuhusu hoja ya uvunjaji wa mnyororo wa utunzaji wa vielelezo (chain of custody), Katuga alidai si lazima kuthibitishwa na shahidi mmoja pekee, bali jukumu la mahakama ni kujiridhisha kama uhalisia wa vielelezo umehifadhiwa ipasavyo pasipo kuchezewa. Amedai pingamizi la aina hiyo haliwezi kuzuia vielelezo kupokelewa, hasa pale ambapo hakuna ushahidi unaoonyesha kuwa vielelezo vilichezewa au kubadilishwa.
Awali Mshtakiwa Lissu aliwasilisha hoja nne za pingamizi mahakamani hapo akipinga vielelezo ambayo ni kadi ya kumbukumbu (Memory Card) na Flashi diski visipokelwa akidai kuwa vilipelekwa labla ya wakati na kwamba havikusomwa wala.videp kuonyeshwa katika Mahakama ya kabidhi (Kisutu) wakati wa kusomwa kwa maelezo ya awali kama inavyotakiwa na kifungu cha sheria cha 263(2) cha CPA.
Pia alidai vielelezo hivyo vimetolewa kabla ya wakati, kwani shahidi mtaalamu alipaswa kwanza kutoa taaeifa yake ya kitaalamu kabla ya kuwasilisha vielelezo.
Aidha alidai Mnyororo wa utunzaji wa vielelezo (chain of custody) umevunjika, hivyo uhalali wa vielelezo hivyo unatia shaka.