TBL yaibuka kidedea kortini sakata la bia ya Basembi, Balimi

Mwanza. Mahakama Kuu imeipiga marufuku kampuni ya East African Spirits (T) Limited, kuzalisha bia aina ya Basembi Extra Lager kwa kuwa inaingilia alama ya biashara ya bia ya Balimi inayozalishwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL PLC).

Kutokana na ukiukwaji huo wa alama ya biashara (trade mark), Mahakama pia imeiamuru kampuni hiyo kuilipa TBL PLC fidia maalumu ya Sh200 milioni kwa kukiuka haki zake kati ya Juni 2024 hadi Desemba 2024 iliposambaza bia hiyo.

Mahakama Kuu Divisheni ya Biashara kanda ya Mwanza imetamka kuwa kampuni ya East African Spirits (T) Limited imekiuka alama ya biashara ya TBL PLC na itawajibika pia kuilipa kampuni hiyo Sh50 milioni kama fidia ya uharibifu wa jumla.

Hukumu hiyo imetolewa Oktoba 17, 2025 na Jaji Mwajuma Kadilu na kuwekwa katika mtandao wa mahakama leo Oktoba 20, 2025 ambapo mbali na kuamuru kulipwa kwa fidia, Jaji huyo ameiamuru kampuni hiyo kulipa gharama za kesi hiyo.

Kulingana na hati ya madai, TBL PLC ililalamika kuwa kitendo cha kampuni hiyo kusambaza bia yenye jina la Basembi pamoja na ufungaji wake, ishara, muundo wa maneno na muktadha, uliingilia alama ya biashara ya bia ya Balimi Extra Lager.

TBL PLC ilieleza kuwa yenyewe ndio mmiliki wa alama ya biashara ya Balimi Extra Lager tangu mwaka 1999 na kwamba soko lake kubwa liko kanda ya ziwa.

Kulingana na kampuni hiyo, neno Balimi inahusu wakulima katika ukanda wa ziwa wakati Basembi ina maana ya wachimbaji hususan wachimbaji wa madini na ni Julai 2024, ndio waligundua kuwa kuna bia inafanana na Balimi kwenye soko.

TBL PLC ililalamika kuwa mdaiwa amekuwa akipitisha bidhaa hizi kana kwamba ni za mlalamikaji, ingawa sio za TBL PLC na hatua hiyo zilikusudiwa kuwapotosha na kuwachanganya wateja waamini bidhaa hizo zinatoka kwa mzalishaji mmoja.

Utetezi wa East African Spirit

Katika utetezi wake wa maandishi, kampuni ya East African Spirit (T) Limited ilikanusha madai hayo na kueleza kwa kuwa bidhaa hizo zinatofautiana kwenye chupa, ladha na ujazo, mnywaji yeyote wa bia anaweza kuzitofautisha.

Kampuni hiyo ilisema bidhaa yao ya Basembi inajitambulisha kwa maneno; “Madini Fahari Yetu” wakati Balimi inatumia “Fahari ya Mavuno Yetu” na kusisitiza kuwa muundo wa maneno hayo ni tofauti na yana maana mbili tofauti.

Katika hukumu yake, Jaji alisema kulingana na ushahidi, bia zote mbili yaani Balimi na Basembi ni alama za biashara zilizosajiliwa kisheria na zote zinatumia neno “Extra Larger”, ikimaanisha hakuna mwenye haki pekee kutumia maneno hayo.

Jaji alisema mdai katika shauri hilo analalamika kuwa alama ya biashara ya Basembi ambayo inatumika katika kuuza bia katika soko lilelile ambalo Balimi inazalishwa, kusambazwa na kuuzwa na TBL PLC inawachanganya wateja.

Akinukuu ushahidi wa shahidi wa kwanza wa mdai alisema mauzo yao yameshuka katika Mkoa wa Shinyanga kutokana na mdaiwa kuingilia haki za alama ya biashara ya Balimi na kwamba Basembi inawachanganya wateja kwa kuwa zinafanana.

Shahidi huyo alisema alama zilizotumika katika Basembi zinafanana na zile za Balimi, ushahidi ulioungwa mkono na shahidi wa pili ambaye ni muuzaji wa rejareja wa vinywaji katika mji wa Kahama akisema hilo linachanganya wateja.

Wakati akiulizwa maswali ya dodoso, Mkurugenzi wa East African Spirit, alisema mdai katika shauri hilo hajawahi kulalamikia ukubwa wa chupa ya Basembi wala kulalamikia ubunifu wala ujazo wa bia hiyo ya Basembi wanayoizalisha.

Alieleza Juni 26, 2024 ndio waliingiza Basembi sokoni na wakati huo Balimi tayari ilikuwa katika soko muda mrefu na baada ya kuizindua, walikamata soko na kufikia Desemba 30, 2024 waliuza Basembi zenye thamani ya Sh2 bilioni nchi nzima.

Kwa Shinyanga pekee ambako bia hiyo ilizinduliwa, waliuza bia zenye thamani ya Sh530 milioni katika kipindi hicho cha Juni 26,2024 hadi Desemba 30,2024.

Shahidi wa tatu wa utetezi, aliieleza mahakama kuwa wateja huwa hawaangalii utambuzi wa rangi, bali wanategemea uaminifu wa chapa ingawa walitegemea kujua mpangilio wa rangi kama vile nyekundu, bluu na kadhalika.

Kulingana na shahidi huyo, mpangilio wa rangi kati ya Basembi na Balimi unatofautiana, akisema Basembi ina rangi nyekundu, njano, bluu na nyeupe wakati Balimi ina rangi mbili za ‘maroon’ na fedha tofauti na Basembi.

Katika Basembi, shahidi huyo alisema kiwango cha kilevi inaonyeshwa chini kabisa upande wa kushoto wa nembo na kuna miale ya jua na kwamba kwa Balimi vipengele hivi ni sawa au vinakaribiana na jinsi Basembi anavyoonekana.

Jaji Kadilu katika hukumu yake hiyo baada ya kupima ushahidi alisema kesi kati ya Liverpool Gin Distillery dhidi ya Sazerac Brands iliweka vigezo vya kuzingatiwa wakati wa kupima uwepo wa mkanganyiko katika alama za biashara.

“Katika kesi hii ilielezwa kwa pamoja kuwa alama lazima ichunguzwe kupitia macho ya mtumiaji wa wastani wa bidhaa au huduma inayobishaniwa,” alisema.

Jaji alisema shahidi wa pili wa utetezi alieleza kuwa hakuna kinachochanganya wateja kwa vile chupa ya Basembi ni ndogo kulinganisha na ile ya Balimi ingawa Basembi ina maneno “Madini Fahari Yetu” na Balimi ina “Fahari ya Mavuno Yetu.”

Kwa mujibu wa Jaji Kadilu, umakini wa mteja unatofautiana kulingana na aina ya bidhaa lakini katika kesi iliyopo mbele yake inahusu pombe, hivyo wateja hawatarajiwi kuwa makini kwenye lebo na maneno yanayoitambulisha.

“Zote Balimi na Basembi ziko katika kundi la 32 katika makundi ya alama za biashara Tanzania, na huwa zinawekwa kwenye ‘shelf’ madukani hivyo kufanya uwepo wa uwezekano wa kuzichanganya,”alisema Jaji Kadilu na kuongeza:

“Ushahidi pia umeonyesha kuwa wateja wa Shinyanga ambako zinauzwa bia hizo mbili hawana elimu ya kutosha na wamekuwa wakimchukulia Basembi kuwa ni Balimi ndogo au Balimi kwenye maboksi,” alieleza Jaji katika hukumu hiyo.

“Kwa maoni yangu, hii ni dalili tosha ya mkanganyiko unaosababishwa na matumizi ya alama hizo mbili kwenye daraja moja la bidhaa.”

Ni kwa msingi huo, mahakama hiyo imethibitisha kuwa kampuni ya East African Spirits (T) Limited imekiuka haki za TBL PLC kwa kutumia alama ya biashara kwenye bia ya Basembi inayofanana na ya Balimi inayozalishwa na TBL.

Hivyo mahakama inatamka kuwa mdaiwa alikiuka haki za TBL katika bia yake ya Balimi, na anatoa zuio la kudumu kwa kampuni hiyo kuzalisha, kuuza, kuifanyia promosheni au kuitangaza bia ya Basembi au nyingine inayofanana na Balimi.

Mbali na hilo, lakini mahakama inamwamuru mdaiwa kuilipa TBL PLC fidia maalum (specific damages) ya Sh200 milioni, Sh50 milioni kama fidia ya uharibifu walioufanya kwa kukiuka haki za TBL PLC na pia kulipa gharama za kesi.