KOCHA Mkuu wa Azam FC, Florent Ibenge amesema licha ya mshambuliaji wa timu hiyo, Jephte Kitambala kutajwa kwa ubora kutokana na kufunga mabao na kuisaidia timu hiyo kwenye malengo ya kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, bado ana kazi ya kufanya na kuweka wazi timu hiyo haimtegemei mtu mmoja.
Azam FC tayari imekaa mguu mmoja sawa kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kushinda mabao 2-0 ugenini dhidi ya KMKM na Ijumaa Oktoba 24, 2025 itakuwa nyumbani kurudiana na timu hiyo na mshindi wa jumla anafuzu makundi.
Kitambala aliyetua Azam msimu huu akitokea AS Maniema ya kwao DR Congo, amefunga mabao mawili katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, akianza kupachika kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya Al Merreikh Bentiu na lingine juzi dhidi ya KMKM.

Ibenge amesema timu hiyo ilivyo sasa haimtegemei mchezaji mmoja kuamua matokeo na timu nyingi zenye mafanikio mazuri michuano ya kimataifa zina sifa kama iliyonayo Azam kwa sasa ambayo ameitaja inahitajika kufanyia kazi nafasi nyingi wanazotengeneza kuamua kuwa mabao.
“Ukiiangalia Azam FC ukiondoa Kitambala ambaye amegeuka gumzo kuwa ndiye mchezaji bora eneo la mwisho, timu yangu haimtegemei mchezaji mmoja, pia ukiondoa sifa hizo timu inatengeneza nafasi nyingi tofauti na uwiano wa mabao tunayofunga,” amesema na kuongeza;

“Tunatengeneza nafasi nyingi lakini matumizi ya nafasi ni madogo, nawapongeza wachezaji wangu wanapambana lakini nimeona shida hii, nitaifanyia kazi kabla ya mchezo wa Ijumaa ili kutengeneza mazingira mazuri kutinga makundi kwa ubora.”
Ibenge amesema wachezaji wake wote wapo kwenye nafasi nzuri ya kuamua matokeo, kwani kila mmoja ana uchu wa kuitetea nembo ya Azam FC na kufikia malengo yao ya kutinga makundi wakiwa na dakika nyingine ngumu nyumbani dhidi ya KMKM.

“Tumepata matokeo mazuri ugenini, hii haitufanyi tukashindwa kuwaheshimu wapinzani wetu, kama sisi tulishinda ugenini na wao wanaweza kupata matokeo hayo ugenini, tutawaheshimu wapinzani wetu na tutaingia kupambania nembo na kufikia malengo,” amesema.