TUJITOKEZE KWA WINGI KUMPONGEZA RAIS SAMIA DAR

:::::::::::

Mkurugenzi wa Msama Production na mwanachama wa CCM, Alex Msama, amewaomba wakazi wa Jiji la Dar es Salaam kujitokeza kwa wingi kumpokea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atakapowasili kwa ajili ya kampeni za uchaguzi mkuu wa Oktoba 29.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Msama amesema ujio wa Rais Samia ni tukio kubwa kwa wakazi wa jiji hilo na unatoa nafasi kwa wananchi kusikiliza moja kwa moja sera na maono ya mgombea huyo wa CCM.

Amesema kuwa Rais Samia amekuwa akipokelewa kwa hamasa na shangwe kubwa katika kila mkoa aliopita, jambo linalothibitisha mapenzi ya dhati kutoka kwa wananchi wa Tanzania.

Msama amewataka wakazi wa wilaya za Ilala, Temeke na Kinondoni kujitokeza kwa wingi siku ya ziara hiyo, akisisitiza kuwa ni fursa ya kipekee kuonesha mshikamano wao na kumuunga mkono Rais wao.

Aidha, amewahimiza wananchi wa kada zote kushiriki kwa amani bila kujali tofauti za kisiasa, kidini au kijamii, kwa kuwa uchaguzi ni sehemu ya demokrasia na unapaswa kufanyika katika mazingira ya utulivu.

Msama pia amewataka Watanzania kupuuza kauli na propaganda kutoka kwa watu wanaoishi nje ya nchi ambao, kwa mujibu wake, wanajaribu kuchochea taharuki bila sababu ya msingi.

Amesisitiza kuwa vyombo vya dola vimehakikisha kuwa uchaguzi huu utakuwa wa amani na kwamba wananchi waendelee kuwa na imani na taifa lao, huku wakilinda amani iliyopo kwa vitendo.