Mtoto wa Mjini – 9

HAMISI alimwambia rafiki yake kwamba, watu walianza kuitilia shaka gari ile baada ya kuiona imeegeshwa pale muda mrefu na kuripoti polisi ambao walifika na kuikagua. Kisha zikapatikana taarifa ya gari lile kutumika katika wizi. 
“Unajua ulikosea sana kuliacha lile gari pale… hukupaswa kulitelekeza lile kule, ungeenda kuliacha kwa mwenyewe… maana ilimbidi akamatwe na polisi…”
Ni hapo Muddy ndipo alipogundua kosa alilokuwa amelifanya baada ya kulitelekeza gari lile katika Mkoa wa Pwani. 
Hamisi alimwambia rafiki yake laiti kama angelirudisha lile gari kwa mwenyewe wala isingejulikana kama ni yeye ndiye aliyeiba zile pesa za Kamba Makambo.
“Ni kweli lakini nilikuwa nahisi kama nilikuwa nachelewa kutoka katikati ya mji baada ya tukio lile, haya ikawaje tena?”
“Ilipotangazwa tu watu wakajua kama ni wewe ndiye uliyemuibia yule Mkongomani…ukatangazwa kwenye TV na magazeti yakaandika habari zako.”
“Daa! Watajuana wenyewe…” alisema Muddy kwa kuamini kama kila kitu kama kingeenda sawa na mipango ya safari yake ingekamilika asingekuwa tena hatiani.
“Hata nilipofika mpakani Namanga niliziona picha zako zimebandikwa kwenye kuta…”  Hamisi aliendelea kumpa habari rafiki yake.
“Kwamba wananitafuta…?”
“Unadhani picha zako zilibandikwa kwa ajili ya kampeni za kugombea ubunge?”
“Aisee…kumbe ile ishu ilikuwa kubwa!” alishangaa Muddy.
“Umeacha gumzo kubwa sana nyumbani… wazazi wako hawakuwa na pa kuweka sura zao…walitawaliwa na sononeko na kila walipopita walionyeshwa vidole kwa kuambiwa walikuwa wakifuga majambazi nyumbani kwao…”
“Daaa! Lakini nikirudi nitawapoza…” Muddy alisema ilhali akiwa ametawaliwa na fadhaa.
“Itabidi uwapoze kwelikweli hadi wakuelewe…maana polisi waliwasumbua,” alisisitiza Hamisi kuhusiana kashfa ambayo wazazi wa Muddy walikuwa wakikumbana nayo.
“Aisee lazima watu wengine waumie ili mmoja anufaike katika familia zetu za Kiafrika…” alijitetea Muddy akidai hakuwa na budi kufanya kile alichokifanya.
“Kuna wakati maneno yalipozidi bi mkubwa wako alikuwa akijifungia ndani na kuangua kilio…” aliendelea kusema Hamisi.
“Najua nimewaumiza kwa kitendo changu, itanibidi nikirudi vizuri nifanye kitu kwa ajili yao.”
Muddy alimwambia Hamisi kwamba maumivu ya watu wote wa familia yake walioumizwa na kitendo chake watayasahau pindi akirudi kutoka Ulaya.
“Nina uhakika nitayabadilisha maisha yao,” alisema.
***
HATIMAYE Fashanu alikamilisha kila kitu na Muddy alitakiwa kusafiri usiku wa siku yake ya sita tangu alipokanyaga katika Jiji la Nairobi.
Kabla ya kuondoka, Muddy aliwachukua rafiki zake hao na wale wa Fashanu kina Omondi, Kimathi, Njuguna, John na kuwapeleka sehemu za starehe ili kuagana.
Muongoza njia alikuwa ni Fashanu na jamaa zake ambao walichagua eneo la Kilimani. Moja kati ya maeneo ya kifahari yaliopo takribani kilometa nne kutoka katikati ya Jiji la Nairobi.
Kilimani ni eneo ambalo linajulikana kwa kuwa na makazi ya hali ya juu, hoteli nzuri, maduka ya kifahari, taasisi za kimataifa na burudani za kisasa.
Eneo hilo linapakana na Yaya Center upande wa Mashariki, Lavington upande wa Kaskazini, Hurlingham upande wa Kusini na Kileleshwa upande wa Magharibi.
Kwa ujumla Kilimani ni kitovu cha burudani, biashara na makazi bora hasa kwa wale wanaopenda maisha ya miji ya kisasa lakini pia utulivu na usalama wa kutosha. 
Fashanu na jamaa zake walihakikisha wanavitembelea viwanja vyote hivyo na walikula na kunywa na kucheza muziki wa kisasa hadi wakatosheka. Waliingia katika klabu ya kifahari ya B-Club ambayo wateja wake walikuwa ni wale wa hadhi ya juu. 
Pia, waliingia Kiza Lounge ambako nako kulikuwa na burudani za Kiafrika, chakula cha kitamaduni na muziki wa kisasa. Hawakutosheka wakaingia Blackyz Lounge, 1824 Kilimani (The Alchemist (karibu na Westlands).
Pia, Muddy alifanya shoping ya nguo za hadhi ya juu katika maduka ya makubwa ya kifahari ya Yaya Center na baada ya kila mmoja kutosheka na starehe, Muddy aliwaachia kiasi cha pesa Fashanu na Hamisi na kuagana nao huku wakitakiana maisha mema.
“Nikifika salama na kuweka mambo sawa, nitawaita mje mshangae Amsterdam,” alisema Muddy wakati Fashanu na Hamisi wakimtakia kila la heri.
“Uzuri hali ya nyumbani unaijua, usitusahau hata kwa vitu vidogovidogo,” Hamisi alimkumbusha swahiba wake na kumwambia asijisahau na kuwaendekeza wanawake wa kizungu bali apige kazi.
“Najua kila kitu, nitajitahidi sana kuwakumbuka…”
Ni baada ya Fashanu, Hamisi na jamaa wengine kurudi kumsindikiza Muddy Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyata (JKIA) ndipo ziliposikika habari za kutafutwa kwa Fashanu na polisi. 
Tayari kulikuwa na taarifa kuhusu uwepo wa mtu anayeitwa Muddy Manyara aliyefanya uhalifu Tanzania na kukimbilia Kenya. 
Hivyo, maaskari wa Kenya walihisi lazima Fashanu angekuwa na taarifa kwa sababu wahalifu wengi kutoka Tanzania walikuwa na desturi ya kukimbilia kwake na yeye amekuwa akiwapa hifadhi.
Nairobi ilikuwa imechafuka, kila kona kulikuwa na askari waliokuwa wakimsaka Fashanu kwa udi na uvumba.
Polisi hao walikuwa na taarifa za Muddy Manyara kuiba pesa nyingi na walifikiria na wao wangeweza kupata mgao wao katika pesa hizo kama wangefanikiwa kumkamata.
Kwa jinsi mpango wao ulivyokuwa walitaka kumfilisi kila kitu Muddy, kisha wamrudishe Tanzania akiwa hana hata senti moja.
Msako ulianzia Majengo, Pumwani hadi wakati polisi walipokuwa wakifika Dandaro, ndege aliyopanda Muddy ilikuwa ikiyapasua mawingu ya Kenya na kuanza safari iliyokuwa imejaa matumaini makubwa kwa abiria huyo.
Fashanu alikuwa ameshamtengenezea kila kitu kuanzia kwa watu wa uwanja wa ndege na baadhi ya maofisa wa uhamiaji wa Kenya, kwa hiyo Muddy safari yake ilianza vizuri. 
Kabla ya kuanza safari hiyo, alipita katika hatua zote za ukaguzi wa Uwanja wa ndege wa JKIA na kwa urahisi na kufanikiwa kuingia ndani ya ndege.
Mara baada ya kufanikiwa kwa hatua hiyo, Muddy alishusha pumzi nzito na kuamini hakukuwa tena na mtu wa kumzuia kuikanyaga Ulaya. Alikuwa ni abiria wa mwanzo kabisa kuingia ndani ya ndege na kuketi kwenye siti yake.
Hakuna mtu aliyebaini kama abiria huyo ilikuwa ni mara yake ya kwanza kupanda ndege.
Muddy alichukua tahadhari zote, abiria huyo mpya kwenye viwanja vya ndege hakutaka kujifanya mjuaji sana wa mambo ndani ya ndege, alikuwa mtulivu na alifuata maelekezo yaliyokuwa yakitangazwa na vitendo vingine ambavyo hakuvijua aliviiga kutoka kwa abiria wengine walivyokuwa wakisafiri nao.
Akiwa ameketi kwenye nafasi yake, aliuona mwangaza mzuri wa maisha yake mbele ya safari yake, aliamini baada ya kufika Ulaya angeweza kupata ajira haraka na kuyabadili maisha yake.
Kubwa alikuwa akifikiria kuwasaidia ndugu zake, hususan wazazi wake, aliumia sana kusikia baba yake na mama yake walifikishwa polisi kutokana na makosa yake.
Alimfikiria pia mzee Mangushi kwa kuwekwa ndani, aliahidi angeweza kumfanyia kitu. 
Baada ya fikra hizo akaifikiria pia safari yake, akilini mwake alitengeneza picha ya majengo mazuri ya kule alikokuwa akienda katika Jiji la Amsterdam.
Polisi wa Kenya walimkamata Fashanu na pia wakamshikilia Hamisi ambaye awali walidhani ndiye Muddy, lakini baada ya kujieleza na kutoa hati yake ya kusafiria aliachiwa.
Hata hivyo, Hamisi hakuachiwa kwa urahisi, ilibidi akate kitu kidogo na ndipo alipoweza kuwa huru.
Utamaduni ulikuwa uleule, unakamatwa na kuingizwa selo bure na hata ukiwa huna hatia unaachiwa kwa kiwango cha pesa.  
***
SAA saba za kukaa angani kutoka Nairobi hadi katika Uwanja wa Ndege wa Stockholm Arlanda (ARN) zilikuwa za faraja kubwa sana kwa Muddy. 
Mara baada ya kufika Sweden abiria wengine walishuka kwa kuashiria kwamba walikuwa wamefika mwisho wa safari zao. 
Waliokuwa wakiendelea na safari walitakiwa kukaa chumba maalumu kusubiri kuunganisha ndege, kwa saa mbili ili kuweza kumalizia safari ya hadi Uwanja wa Ndege wa Amsterdam Schiphol (AMS) katika nchi ya Uholanzi.
Muddy akiwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Arlanda, alikuwa na matumaini makubwa zaidi ya kuendelea na safari yake na kufika hadi katika kituo hicho cha mwisho.
Ni wakati huo ambapo jambo lisilotarajiwa lilipotokea na kumshtua. Sio kumshtua tu, bali lilimchanganya akili yake. 
Muddy alikumbwa na fadhaa na kuhisi kuchanganyikiwa baada ya maafisa wa uhamiaji waliokuwa uwanja wa ndege kumfuata na kumwambia walikuwa wakihitaji kufanya naye mahojiano mafupi.

Hakutaka kubishana nao alijitahidi kujiweka katika hali ya kawaida ingawaje uso wake ulionekana kutawaliwa na hofu kutokana na kitendo hicho.
“Kwa nini mimi…?” alijiuliza huku akiwaangalia abiria wengine waliokuwa pamoja naye katika kusubiri kuunganisha ndege ya kwenda Uholanzi.
Katika muda wote huo, mambo kadhaa yaliusumbua ubongo wake. Kitu cha kwanza kilichoitesa akili yake ni kitendo chake cha kumuibia yule raia Jamhuri ya Congo.
Hata hivyo, akili ya Muddy haikutaka kuamini kama taarifa za uhalifu wake aliokuwa ameufanya Kariakoo zilikuwa zimefika hadi Ulaya.
Maafisa wa uhamiaji walikuwa ni wanaume watupu walionekana kuwa makini sana, walimchukua hadi katika chumba maalumu kwa ajili ya mahojiano wakitaka kujua undani wa safari yake ya Uholanzi.