Mahakama ya Hakimu Mkazi Kivukoni, Kinondoni imewahukumu vijana wanne, akiwemo askari mmoja na mabondia wawili, kifungo cha miaka saba jela kila mmoja baada ya kupatikana na hatia ya kujaribu kumteka mfanyabiashara Deogratus Tarimo.
Hata hivyo, mahakama hiyo imewaachia huru washitakiwa wawili Nelson Msela (24), dereva wa teksi, na Anitha Temba (27) baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha ushiriki wao katika tukio hilo.
Waliohukumiwa ni Fredrick Nsato (21), askari na mkazi wa Kibamba; Isaack Mwaifuani (29), bondia mkazi wa Kimara; Benki Mwakalebela (40), wakala wa mabasi katika Stendi ya Magufuli; na Bato Twelve (32), bondia mkazi wa Kimara Bonyokwa.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu Ramadhani Rugemalira alisema mahakama imejiridhisha bila kuacha shaka kwamba washitakiwa hao wanne walihusika katika jaribio la utekaji, ingawa walishindwa kutekeleza mpango wao hadi mwisho.
“Washtakiwa wote wanne mnahukumiwa kifungo cha miaka saba jela kwa kosa la kujaribu kumteka mfanyabiashara Deogratus Tarimo, kwa kuwa ushahidi umeonyesha walikuwa katika harakati ambazo hazikufanikiwa,” alisema Hakimu Rugemalira.
Awali, washitakiwa walikuwa wakikabiliwa na kosa la utekaji, lakini mahakama ilibadilisha shtaka hilo na kuwa kujaribu kuteka, baada ya kubainika kuwa Tarimo aliachwa eneo la tukio bila kupelekwa sehemu nyingine.
Katika utetezi wao, washitakiwa waliomba kupunguziwa adhabu wakidai kwamba Askari Nsato aliwadanganya kuwa wanakwenda kumkamata mtuhumiwa wa uhalifu, hivyo walishiriki tukio hilo bila kujua ukweli.