Malezi ya kielimu yanavyowashinda wengi

Dar es Salaam.Malezi ya mtoto si kazi rahisi. Zamani, familia ilikuwa ikishirikiana kumlea mtoto kwa pamoja. Kila jirani, kila shangazi na mjomba walihusika kuhakikisha mtoto anakua katika nidhamu.

Lakini siku hizi, hali imebadilika. Wazazi wengi wamebaki peke yao katika jukumu hili na bado changamoto ni kubwa zaidi, hasa linapokuja suala la malezi ya kielimu.

Malezi ya kielimu ni pale ambapo mzazi anakuwa mwalimu wa kwanza wa mtoto. Hapa hatuzungumzii tu kumpeleka mtoto shuleni, bali namna mzazi anavyohakikisha elimu inakua sehemu ya maisha ya kila siku nyumbani. 

Mwanafalsafa wa Kihispania,  George Santayana aliwahi kusema: “A child educated only at school is an uneducated child.” Kwa maneno rahisi, mtoto akifundishwa shuleni pekee bila msaada wa nyumbani, anakuwa hajapata elimu kamili.

Kwa mfano, mzazi anapokaa na mtoto wake kusoma hadithi kabla ya kulala, au kumfundisha namna ya kupanga muda wake wa masomo, tayari anakuwa ameanza safari ya malezi ya kielimu. 

Mzazi anapokuwa mfano kwa kusoma vitabu, kujifunza mambo mapya, au kujadili habari za kila siku mezani, mtoto huona kujifunza ni kitu cha kawaida na cha maana.

Hata hivyo, wazazi wengi wa Kitanzania wanashindwa kutekeleza jukumu hili. Kwanza, muda ni changamoto. Wengi hufanya kazi mchana kutwa, wengine wana biashara au shughuli zinazowachosha. 

Baada ya kazi, mzazi anarejea nyumbani akiwa amechoka, hivyo muda wa kukaa na mtoto kuzungumza masuala ya elimu haupatikani.

Pili, wazazi wengi bado wanadhani elimu ni sawa na kupata alama nzuri darasani. Watoto wakipata “division one” au wakionekana wakizungumza Kiingereza vizuri, mzazi husema kazi imekamilika.

Lakini malezi ya kielimu yanazidi matokeo  ya darasani. Yanahusu kujenga utu, kujitegemea, maadili na kufikiri kwa kina.

Changamoto nyingine ni mgawanyo wa majukumu ndani ya familia. Mara nyingi, jukumu la kumsaidia mtoto kimasomo huachwa mikononi mwa mama pekee, huku baba akijikita kwenye kutafuta kipato. 

Wakati mwingine, wazazi wote wawili wanakosa nafasi hiyo na mtoto hubaki akijilea mwenyewe. Matokeo yake, watoto wanakuwa na nidhamu dhaifu na maadili yanayoyumba.

Licha ya changamoto hizi, suluhu ipo. Kwanza kabisa, wazazi wanapaswa kujitahidi kutumia muda wao wa nyumbani vizuri.

 Hata dakika 30 za kusoma na mtoto au kujadili mada moja shuleni ni msaada mkubwa. Pili, wazazi wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa. 

Mtoto anapomuona mzazi akisoma gazeti, kitabu au hata kuandika mawazo yake, naye hutamani kufanya hivyo.

Hii ndiyo maana mtaalamu wa elimu, Robert J. Havighurst aliandika kwamba: “The two basic principle processes of education are knowing and valuing”  yaani elimu ni kujua na kuthamini.

Ni muhimu pia kuwapa watoto nafasi ya kuuliza maswali na kujadili mawazo yao. Badala ya kumkemea mtoto anapokosea, mzazi anaweza kumuuliza: “Kwa nini umefikiria hivi? Unaonaje tukijaribu kwa njia nyingine?” Njia hii humfundisha mtoto kufikiri kwa kina na kuchukua uamuzi.

Zaidi ya hapo, wazazi wanapaswa kushirikiana na walimu. Kila mzazi akihudhuria vikao vya shule, kufuatilia maendeleo ya mtoto wake na kushirikiana na mwalimu, mtoto hujifunza kuwa elimu si jukumu lake peke yake, bali la familia nzima na jamii.

Umuhimu wa malezi ya kielimu ni mkubwa. Kwanza, hujenga tabia ya kujifunza maisha yote. Mtoto anayesaidiwa nyumbani hachukulii elimu kama adhabu, bali kama fursa ya kujitengeneza. Pili, huweka msingi wa mafanikio shuleni. Santayana aliongeza: “Mtoto anaposaidiwa nyumbani, matokeo yake darasani huwa bora zaidi.”

Zaidi ya yote, malezi haya hujenga utu na maadili. Mwandishi, Simon Soloveychik alisisitiza katika kitabu chake Parenting for Everyone kwamba: “We raise not a child but a man.” Yaani, lengo la malezi si kufundisha tu hesabu na kusoma, bali kumtengeneza binadamu mwenye utu, heshima na huruma.

Kazi za kitafiti za Nancy E. Hill zinaonyesha kuwa matarajio ya wazazi kuhusu elimu huathiri hata maisha ya watoto wanapokuwa watu wazima. Ikiwa mzazi atamjengea mtoto imani kuwa elimu ni nguzo ya maisha, mtoto huyo atakua akiamini hivyo na kufanikisha maisha yake.

Kwa hiyo, malezi ya kielimu si jambo la hiari bali ni jukumu la msingi kwa kila mzazi. Ni kweli maisha ya sasa yamejaa msongo na kazi nyingi, lakini bila muda wa kukaa na watoto na kuwasaidia kielimu, tutakuwa tunawafundisha nusu tu ya maisha. 

Taifa lenye wazazi wanaojituma katika malezi ya kielimu ndilo taifa litakaloandaa kizazi chenye maarifa, nidhamu na maadili kwa ajili ya kesho bora.