BINGWA mtetezi wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), Mlandege, imeonekana kuteseka katika ligi hiyo baada ya kucheza mechi nne bila ya ushindi wala kufunga bao msimu huu wa 2025-2026.
Mlandege ambayo msimu uliopita ilitwaa ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar kwa tofauti ya mabao mbele ya KVZ zote zikimaliza na pointi 62, msimu huu katika mechi nne za kwanza, imeambulia sare tatu na kupoteza moja.
Licha ya timu hiyo kufanya maboresho makubwa ya kusajili wachezaji kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Brazil, Ufaransa, Comoro, Ghana na Nigeria, lakini imeshindwa kufanya kile kilichotarajiwa kama bingwa mtetezi.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha msaidizi wa timu hiyo, Sabri China amesema wachezaji wanatengeneza nafasi, lakini kinachoshindikana ni kufunga kwani hawana utulivu mzuri wa kufanya uamuzi.

“Tatizo kubwa kwa wachezaji waliosajiliwa kutoka nje ni kutoendana na kiwango cha wachezaji wazawa na mifumo inayotumika kutokana na ligi yetu kutokuwa bora zaidi kama za kwao,” amesema na akuongeza, wakati mwingine changamoto ni wachezaji kutoelewa mfumo unaotumiwa na timu na kutumia mifumo yao binafsi.
Hata hivyo, Sabri amesema ligi tayari imeanza na wanaanda mikakati mizuri kwa kikosi hicho ili ubingwa huo kuendelea kubaki mikononi mwao.
Wakati mabingwa hao wakijiandaa na michuano ya CECAFA Kagame Cup 2025 iliyoanza Septemba 2 hadi 15, mwaka huu, kikosi hicho kilitambulisha wachezaji 13 ambao ni Enzo Claude (Ufaransa), Vitor De Souza (Brazil), Ishmael Robono (Ghana), Davi Nasciimento (Brazil), Fortune Chidera (Nigeria), Alfonsi Ahmed (Comoro), Hamis M’sa (Comoro), Berry Iziegbuwa (Nigeria) na Patrick Henry (Nigeria).

Wachezaji wengine kwa upande wa wazawa ni Abubakar Hussein, Omar Ramadhan, Yazidu Idd na Mudathir Juma.
Hadi sasa, Mlandege imeshacheza mechi 10 za mashindano yote msimu huu, imepoteza tano, imeshinda mbili na sare tatu. Pia imefunga mabao 11 na kuruhusu 14.
Mara ya mwisho ilipata ushindi Septemba 27, 2025 kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar dhidi ya Ethiopian Insurance wa mabao 3-2 ikiwa ni mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hata hivyo, matokeo hayo hayakuwasaidia zaidi kutolewa mashindanoni kwa jumla ya mabao 4-2 baada ya awali kufungwa 2-0.