‘Dk Manguruwe’ adai barua 10 alizomuandikia DPP hazijajibiwa, mahakama yamjibu

Dar es Salaam. Mkurugenzi wa Kampuni ya Vanilla International Ltd, Simon Mkondya (40), maarufu Dk Manguruwe anayekabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi, amedai mahakamani kuwa ameshaandika barua 10 kwenda kwa Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ( DPP) akiomba kukiri mashtaka yake, lakini hazijajibiwa.

Mshtakiwa huyo ametoa madai hayo leo Jumanne, Oktoba 21, 2025 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati kesi yake ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.

Mkondya na mwenzake, Rweyemamu John (59), ambaye ni mkaguzi wa fedha wa kampuni hiyo, wanakabiliwa na mashtaka 28 yakiwemo ya kuendesha biashara ya upatu na utakatishaji fedha linalomkabili Mkondya pekee yake.

Hata hivyo, John ambaye ni mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo, yupo nje kwa dhamana baada ya kwenda kuomba dhamana Mahakama Kuu na pia hana mashtaka ya kutakatisha fedha.

“Mheshimiwa hakimu nipo gerezani napata mateso, walalamikaji walionipeleka Polisi nao wanalalamikia kucheleweshwa kwa upelelezi wa kesi hii,” amedai Mkondya mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu,  Anna Magutu, anayesikiliza shauri hilo.

Mshtakiwa huyo aliendelea kudai kuwa, pia ameshamwandikia barua zaidi ya 10 Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ( DPP), akiomba kufanya majadiliano ya kuimaliza kesi hiyo, lakini hadi leo hajajibiwa.

Kutokana na madai hayo, hakimu Magutu alimueleza mshtakiwa huyo tarehe ijayo atapewa majibu na Jamhuri kuhusiana na barua hizo alizoandika.

Awali, wakili wa Serikali, Florida Moses alidai kuwa shauri hilo limeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi wake bado unaendelea hivyo, wanaomba mahakama iwapangie tarehe nyingine.

Hakimu Magutu alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka na kuahirisha kesi hiyo.

Mkondya yeye anaendelea kusalia rumande kutokana na mashtaka yanayomkabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.

Kwa mara ya kwanza washtakiwa hao walifikishwa Mahakamani hapo Novemba 5, 2024 na kusomewa kesi ya uhujumu uchumi.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, kati ya mashtaka hayo 28,  19 ni ya kuendesha biashara ya upatu na mashtaka tisa ni ya kutakatisha viwanja.

Katika moja ya mashtaka hayo kuendesha biashara ya upatu, washtakiwa wanadaiwa  kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi,2023, jijini Dar es Salaam, walitenda makosa hayo

Inadaiwa kuwa Mkondya akiwa kama Mkurugenzi wa kampuni hiyo na John akiwa  Mkaguzi wake waliendesha  biashara ya upatu kwa kuwaahidi watu watapata pesa mara mbili hadi  tatu kama faida zaidi ya waliyotoa.

Washtakiwa hao wanadaiwa kujipatia kiasi cha Sh92.2 milioni kutoka kwa watu 19 tofauti ambao walitoa kiasi tofauti cha fedha kwa kuwaahidi kuwa watapata faida mara mbili hadi tatu ya fedha walizotoa.

Katika mashtaka tisa ambayo ni ya utakatishaji fedha yanayomkabili Mkondya pekee yake, inadaiwa kuwa kati ya Januari Mosi, 2020 na Desemba Mosi, 2023 akiwa katika mkoa wa Dar es salaam na akiwa kama Mkurugenzi wa Kampuni hiyo alijipatia jumla ya viwanja tisa vilivyopo katika kitalu namba AB eneo la Idunda mkoani Njombe.

Pia, Mkondya anadaiwa kujipatia viwanja hivyo huku akijua viwanja hivyo ni mazalia ya makosa tangulizi ya kuendesha biashara ya upatu.