Dar es Salaam. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), imewakamata watu wanne wanaodaiwa kukutwa wanatengeneza biskuti za bangi wakiwa kwenye sherehe ya kuzaliwa mwenzao, maarufu ‘house party’.
Watuhumiwa hao wanne ambao wote wana umri wa miaka 26 wanadaiwa kuwa wanafunzi wa chuo kikuu na walikusanyika katika nyumba hiyo iliyopo eneo la Mlalakuwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kusherehekea siku ya kuzaliwa ya mwenzao.
Hii si mara ya kwanza kwa biskuti za aina hiyo kukamatwa katika mazingira yanayowahusisha vijana hasa wanafunzi wa vyuo, hali inayoashiria kengele ya hatari kwa kundi hilo.

Akizungumzia hilo Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo amesema vijana hao walikutwa na biskuti 140 za bangi, puli nane, na paketi tisa za bangi zenye jumla ya kilo 2.858.
“Hii inaonesha namna vijana wetu wanavyohatarisha maisha yao kwa kujihusisha na utengenezaji wa bidhaa zenye dawa za kulevya kwa ajili ya starehe,”amesema Lyimo,
Kufuatia hilo amewaonya wanafunzi wa vyuo vikuu kuacha mara moja kujihusisha na dawa za kulevya na badala yake kutumia muda wao katika masomo ili kutimiza ndoto zao.
“Vijana wetu ndio nguvu kazi ya Taifa. Tunataka waishi maisha yenye afya, wasikubali kudanganywa na makundi yanayotumia dawa za kulevya kama sehemu ya starehe. Mamlaka haitasita kuchukua hatua kali kwa yeyote atakayehusishwa na uhalifu huu,” amesisitiza Lyimo.
Katika hatua nyingine mamlaka hiyo imekamata jumla ya kilogramu 10,763.94 za aina mbalimbali za dawa za kulevya pamoja na kilogramu 6,007 na lita 153 za kemikali bashirifu.
Lyimo, amesema mafanikio hayo yametokana na operesheni zilizofanyika katika kipindi cha Septemba na Oktoba 2025 kwenye maeneo mbalimbali nchini.

Katika operesheni iliyofanyika eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, mamlaka ilikamata dawa za kulevya aina ya mirungi zenye uzito wa kilogramu 40.32 zilizokuwa zimekaushwa na kufungwa kama viungo (spices), katika paketi 80 zenye maandishi ya ‘Dry Basil Leaves’.
Dawa hizo zilikuwa zikisafirishwa kwenda nchini Canada na Italia kupitia kampuni za usafirishaji.
Watu wawili wamekamatwa wakihusishwa na dawa hizo na uchunguzi wa awali umebaini dawa hizo ziliingizwa nchini kwa njia za kificho kutoka nchi jirani.
“Uchunguzi wetu umeonesha uwepo wa mtandao wa usafirishaji wa mirungi unaotumia bodaboda na baadhi ya mawakala wa kampuni za usafirishaji, ili kurahisisha kusafirisha dawa hizo bila kutiliwa shaka.
“Mtandao huu unaweza kuathiri taswira ya nchi yetu kimataifa, na sisi hatutalifumbia macho suala hili,”.
Amesema mamlaka hiyo inaendelea na uchunguzi wa matumizi ya bangi kwenye bidhaa mbalimbali ikiwemo vinywaji, vyakula, vipodozi na sigara za kielektroniki (vapes), ambapo baadhi ya bidhaa zimebainika kuwa na viambata vya bangi.
Akizungumzia operesheni zilizofanyika mikoani, Lyimo amesema DCEA kwa kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama imefanikiwa kukamata bangi kilo 9,164.92, mirungi kilo 1,555.46, skanka gramu 367, na heroini gramu 7.498, pamoja na kuteketeza ekari 11.5 za mashamba ya bangi.
Kamisha Lyimo ametumia fursa hiyo kuwaonya bodaboda, wamiliki wa kampuni na mawakala wa usafirishaji kuwa makini na mizigo wanayobeba au kusafirisha ili kuepuka kujikuta kwenye mgogoro wa kisheria.