Mara yajitosa kampeni ya nishati safi

Musoma. Wakala wa Nishati Vijijini (REA), umeanza kusambaza mitungi ya gesi 19,530 yenye thamani ya zaidi ya Sh390 milioni mkoani Mara ikiwa ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, huku wananchi mkoani humo wakiiomba Serikali kusogeza vituo vya kujaza gesi karibu na makazi yao.

Mitungi hiyo yenye ujazo wa kilo sita kila moja itauzwa kwa bei ya ruzuku ili kuwezesha wananchi wa maeneo hayo ya vijijini kuanza matumizi ya nishati hiyo na kuachana na matumizi ya kuni na mkaa, ambayo yameelezwa
kuwa na athari nyingi ikiwemo za kiafya na kimazingira.

Rais Samia Suluhu Hassan tayari alitangaza mkakati wa Serikali wa kuongeza matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini hadi kufika asilimia 80 mwaka 2034.

Akitoa taarifa ya mradi huo katika kijiji cha Etaro wilayani Musoma leo Oktoba 21,2025,Mhandisi wa miradi kutoka REA, Geofrey Gedo amesema kuwa kwa mujibu wa utafiti waathirika wengi wa matumizi ya nishati isiyokuwa salama ni wanawake na watoto, jambo ambalo Serikali imeona ipo haja ya kulitafutia ufumbuzi wa kudumu.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi wa usambazaji wa mitungi ya gesi mkoani Mara ikiwa ni sehemu ya uhamasishaji wa hamii kuhusu matumizi ya nishati safi ya kupikia.  Picha na Beldina Nyakeke

“Utafiti uliofanywa mwaka 2016 ulibainisha kuwa watu 33,024 hufariki nchini kila mwaka kabla ya wakati hii ni sawa na asilimia 8.49 ya vifo vyote nchini na vifo hivi hutokana na magonjwa ambayo yanachangiwa na uchafuzi wa hewa ndani ya nyumba, huku waathirika wengi wakiwa ni wanawake na watoto,” amesema

Amesema takwimu zinaonyesha kuwa matumizi ya kuni kama chanzo kikuu cha nishati ya kupikia nchini bado ni makubwa ambapo asilimia 63.5 ya kaya nchini zinatumia kuni kama chanzo cha nishati.

Amefafanua takwimu hizo pia zinaonyesha kuwa matumizi ya mkaa ni asilimia 26.2 huku matumizi ya gesi iliyojazwa kwenye mitungi (LGP) ikiwa ni asilimia 5.1 pekee, na umeme ukiwa unatumiwa kwa asilimia 3 huku vyanzo vingine vikiwa ni asilimia 2.2.

Amesema kupitia mradi huo wa uuzwaji wa mitungi hiyo kwa bei ya ruzuku utasaidia kupandisha kiwango cha watu wanaotumia nishati ya gesi nchini hivyo kuondokana na athari zinazotokana na matumizi ya nishati chafu ya kupikia.

“Mitungi hii itauzwa kwa bei ya ruzuku ya asilimia 50 ambapo kila mtungi pamoja na vifaa vyake utauzwa kwa Sh20,000 hii bei ni rafiki na tunaamini hata zile familia zenye kipato cha chini kitamudu,” amesema.

Wakizungumza kwenye uzinduzi huo baadhi ya wakazi wa kijiji cha Eyaro wameiomba Serikali kuhakikisha nishati hiyo ya gesi inapatikana kwa ukaribu ili kuepuka gharama za ziada.

“Hapa kwetu angalau kuna sehemu gesi ikiisha unaweza kwenda kujaza kwa sababu hapa senta kuna wafanyabiashara wanaojihusisha na biashara hii lakini kuna maeneo mengi hakuna gesi, hivyo ukihitaji inakubidi usafiri umbali mrefu,” amesema Nyangeta Chimwejo.

Eva William amesema kutokana na mabadiliko ya tabia nchi wananchi hasa wa vijijini hawana budi kuanza kutumia nishati ya gesi katika mapishi yao kwa maelezo kuwa upatikanaji wa miti na mkaa hivi sasa umekuwa wa shida.

Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka akikabidhi mtungi wa gesi kwa mkazi wa Kijiji cha Etaro wilayani humo ikiwa ni uzinduzi wa usambazaji wa mitungi zaidi ya 19,000 mkoani Mara kwaajili ya kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia

“Zamani kuni zilikuwa zinapatikana kwa ukaribu zaidi lakini sasa hivi misitu yote imeteketezwa na matumizi ya binadamu, tunashukuru Serikali kutuletea mitungi hii kwani itakuwa ni hamasa kwa wengi kuachana na matumizi ya kuni na mkaa na kuhamia kwenye gesi,” amesema.

Akizindua mradi huo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Juma Chikoka amesema Serikali imeweka ruzuku kupunguza gharama ili wananchi wajaribu matumizi ya nishati hiyo na kuona faida yake ikilinganishwa na matumizi ya kuni na mkaa.

Chikoka amesema mitungi hiyo inatarajiwa kusambazwa katika wilaya zote sita za Mkoa wa Mara na kueleza kuwa Serikali inatambua athari zinazowakumba wananchi hasa wanawake kutokana na matumizi ya kuni na mkaa.