Moshi. Mahakama Kuu Kanda ya Moshi imewahukumu kunyongwa hadi kufa wakazi watatu wa mjini Moshi, waliohusika kumuua Khudheifa Chang’a, Ofisa Muuguzi Msaidizi Daraja la Pili katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC.
Muuguzi huyo aliuawa kwa kuchomwa visu saa 9:00 usiku wa kuamkia Julai 2, 2023, katika uchochoro wa Five Star, ilikodaiwa alikwenda kufanya ngono na mshtakiwa wa pili, Fatuma Mdetele maarufu ‘Purity’, ambaye ni kahaba.
Purity ndiye aliyempigia simu mshtakiwa wa kwanza, Aristariki Temu maarufu Arii, akamweleza kuwa mteja aliye naye alikuwa na simu kali (nzuri) na pesa nyingi, wakaenda na mshtakiwa wa tatu, Peter Raymond.
Arii na Peter, ambao ni madereva bodaboda, waliandika maelezo kwa mlinzi wa amani (shahidi wa tano wa Jamhuri, Adinani Kingazi), ambaye ni Hakimu Mkazi Mwandamizi, wakaeleza mwanzo hadi mwisho juu ya mauaji hayo.
Kutokana na uzito wa ushahidi wa mashahidi wa Jamhuri, ambao haukuacha shaka kuwa washtakiwa ndio waliomuua Chang’a, Jaji Safina Semfukwe wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi amewatia hatiani na kuwahukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.
Katika ushahidi huo inaeleza kuwa siku ya tukio, Chang’a alimkodi Purity aliyekuwa kahaba wakaenda uchochoroni, ambako aliwaita mshtakiwa wa kwanza na wa tatu waliomuua Chang’a kwa kumchoma kisu.
Katika hukumu iliyotolewa Oktoba 17, 2025, na kupakiwa kwenye mtandao wa mahakama leo Oktoba 21, 2025, Jaji Simfukwe amesema adhabu ya kuua kwa kukusudia ni moja tu, hivyo washtakiwa hao watatu watanyongwa hadi kufa.
Shahidi wa pili, Happiness Mushi, alieleza kuwa siku ya tukio saa 9:00 usiku alimuona mtu aliyekuwa amekubaliana na Purity kufanya ngono, waliongozana hadi uchochoroni.
Baada ya muda mfupi, aliona pikipiki mbili zikielekea kwenye uchochoro, kila moja ikiwa na watu wawili. Baada ya watu hao kufika uchochoroni, ghafla alisikia sauti ya mtu akiita: “Nisaidieni, nisaidieni!”
Alidai alimuona Purity akitoka uchochoroni akiwa na matone ya damu mikononi, alipomuuliza nini shida, alimjibu kuwa Arii na washirika wake wamempiga mtu aliyekuwa naye kwa kisu.
Shahidi huyo alidai Purity aliondoka, hakujua alikwenda wapi. Ilipofika saa 12:00 asubuhi alimkodi dereva bodaboda (Baraka) ampeleke kwa mpenzi wake Majengo, lakini baadaye alimwambia ampeleke kwenye ule uchochoro.
Alieleza kuwa alifanya hivyo baada ya kusikia kuna mtu ameuawa kwenye uchochoro huo, hivyo alitaka aone sura yake. Alipofika alimkumbuka mtu aliyemuona kwenye klabu ya Redstone usiku huo, hivyo alichukua vitambulisho na kuvipeleka Polisi.
Akiwa Polisi, alikutana na OC-CID aliyemweleza kile alichokifahamu kuhusu tukio hilo. Walikwenda na maofisa wa Polisi kwenye uchochoro huo na kumkuta mtu yule aliyemweleza OC-CID na kile ambacho Purity alimweleza.
Shahidi wa kwanza, Mrakibu wa Polisi Levina Theognance, ambaye ni Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OC-CID) ya Moshi, alieleza namna shahidi wa pili, Happiness, alivyomweleza kile anachokifahamu na akajitolea kuwapeleka eneo la tukio.
Kabla ya kwenda, aliwapa vitambulisho viwili alivyoviokota eneo la tukio ambavyo vilimtambulisha marehemu kuwa ni muuguzi na alikuwa akifanya kazi Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kaskazini ya KCMC ya mjini Moshi.
Shahidi huyo alichukua wataalamu wa uchunguzi wa kisayansi na kwenda nao eneo la tukio, ambako ilibainika mtu huyo ameshafariki dunia.
Ilipofika saa 2:00 asubuhi walikwenda nyumbani kwa Purity, hakuwapo, lakini saa 8:00 mchana alipokea taarifa kuwa madereva bodaboda wako katika harakati za kumhamisha Purity. Walikwenda wakamkuta akipanga vitu vyake.
Shahidi wa nne, Shaban Singano, alieleza namna asubuhi ya siku ya tukio mshtakiwa wa pili alimkodi akimtaka ampeleke Malindi akamchukue mkewe aliyelewa sana. Hawakumkuta, lakini alionekana akiweweseka.
Alidai aliendelea kumsumbua na baadaye akapata taarifa za mtu aliyeuawa uchochoroni, hivyo alikwenda eneo la tukio alikouona mwili.
Aliporudi Malindi ili aondoke, ghafla mshtakiwa alidandia pikipiki. Njiani wakielekea Njoro, mshtakiwa huyo (Titus) alimweleza juu ya mauaji, alipomhoji alijuaje kuna mtu ameuawa, hakumjibu.
Alieleza aliporudi kijiweni walishauriana na madereva bodaboda wenzake wakatoe taarifa Polisi.
Shahidi wa tano, ambaye ni Hakimu Mkazi Mwandamizi na mlinzi wa amani, aliyeandika maelezo ya ungamo ya mshtakiwa wa kwanza na wa tatu, aliwasilisha kortini maelezo ya washtakiwa hao kama kielelezo cha kesi.
Mashahidi wengine, ambao ni maofisa wa Polisi walioshiriki ukamataji, walieleza namna walivyowakamata washtakiwa na walivyoandika maelezo yao ya onyo.
Mshtakiwa wa kwanza, Aristariki Temu, alijitetea akikana shtaka na kuwafahamu washtakiwa wenzake. Pia alikana kuandika maelezo yoyote ya kukiri kosa wala kumtaja mshirika yeyote baina yao.
Mshtakiwa wa pili, Fatuma Mdetele, alikana shtaka, akaeleza namna alivyokamatwa na kuhusishwa na mauaji. Pia alikana kuwafahamu washtakiwa wenzake na kujihusisha na ukahaba.
Alidai Polisi wamembambikia kosa, akieleza awali alikuwa na ugomvi na shahidi wa pili wa upande wa mashtaka (Happiness), akidai alikuwa akimtaka kimapenzi mwanamume waliyezaa naye mtoto.
Mshtakiwa wa tatu, Peter Kulaya, alieleza namna alivyokamatwa, akakana shtaka la mauaji, akieleza amebambikiwa kosa hilo kutokana na ugomvi alionao na afande mmoja aliyechukua Sh800,000 alipokuwa mahabusu Oktoba 2019.
Alikana kuandika maelezo kuwa anakiri kosa hilo na kwamba hakuwahi kuwafahamu washtakiwa wenzake isipokuwa baada ya kukamatwa na Polisi.
Katika hukumu, Jaji Simfukwe alirejea ushahidi wa shahidi wa pili, kwamba siku ya tukio Purity alikubaliana na marehemu (Chang’a) kwenda kufanya ngono uchochoroni, alivyosikia sauti ya kuomba msaada, na alichoelezwa na Purity.
Pia, alirejea ushahidi wa shahidi wa saba aliyeandika maelezo ya mshtakiwa wa kwanza, ambaye alikiri kushiriki mauaji na kumweleza ofisa huyo wa Polisi kuwa waliitwa na mshtakiwa wa pili (Purity) ili wakampore Chang’a.
Alirejea maelezo ya ungamo ya mshtakiwa wa tatu aliyoyaandika kwa mlinzi wa amani, akieleza kuwa yeye ndiye alimchoma kisu marehemu (Chang’a) kwa kutumia kisu cha mshtakiwa wa kwanza, ushahidi ambao unaunganika.
“Mahakama imeridhika kuwa maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa kwanza na maelezo ya ungamo ya mshtakiwa wa kwanza na wa tatu yanaunganika na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa kwanza, wa pili, wa nne, wa saba na wa nane wa Jamhuri,” amesema.
Katika maelezo hayo wanaeleza namna mshtakiwa wa pili alivyowapigia simu na kuwaita eneo la tukio ili wampore Chang’a (marehemu), na kwamba walipofika, alikuwa mbishi akijihami na alimkaba mshtakiwa wa kwanza, Aristariki.
Ili kumnusuru mwenzao, mshtakiwa wa tatu alichukua kisu kutoka kwa mshtakiwa wa kwanza na kumchoma nacho mgongoni, na alipoanza kuwa dhaifu na kupoteza nguvu, ndipo akamwachia mshtakiwa wa kwanza.
Mshtakiwa wa kwanza alipasua chupa na kumshambulia nayo, kisha walichukua pesa za marehemu (Chang’a) na simu zake.
Kuhusu uwepo wa dhamira ovu, Jaji amesema imethibitika bila shaka yoyote kuwa washtakiwa walitenda kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha, jambo ambalo linathibitisha walikuwa na dhamira ovu ya kutenda kosa lililoangukia mauaji.