Geita. Mgombea ubunge wa Jimbo la Geita Mjini kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), Mhandisi Chacha Mwita, ameahidi kuwa endapo atachaguliwa kuwa mbunge, atahakikisha mkoa wa Geita unakuwa kinara wa ufaulu kitaifa kwa shule zilizopo katika Manispaa ya Geita.
Akizungumza leo Jumanne, Oktoba 21, 2025, katika mkutano wa kampeni uliofanyika Mtaa wa Tambukareli, Kata ya Kalangalala, Mwita amesema uzoefu alioupata kupitia shule binafsi anazozimiliki utamsaidia kuboresha sekta ya elimu katika jimbo hilo.
“Nimeishi Geita kwa miaka 20, ninazifahamu changamoto za wananchi. Nikiwa mbunge wenu, nitahakikisha tunainua kiwango cha elimu, hasa katika shule ya msingi Tambukareli, ili tufanye vizuri kitaifa,” amesema Mwita.
Amesema uzoefu wake katika sekta ya elimu utakuwa nyenzo muhimu katika kupanga mikakati ya kuinua ufaulu na kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.
Kuhusu ukosefu wa ajira kwa vijana, Mwita amesema atashirikiana na Mkurugenzi wa Manispaa ya Geita na Baraza la Madiwani kujenga Chuo cha Ufundi Stadi (VETA), katika eneo la karakana ya Magogo, ili kutoa mafunzo ya ufundi yatakayowawezesha vijana kujiajiri au kuajiriwa.
“Tutajenga chuo pale karakana ya Magogo. Vijana wetu watasoma bure, watafundishwa na kupata ujuzi wa kujiajiri. Tutawatafuta walimu wenye uwezo na kuwalipa sisi wenyewe,” amesema.

Aidha, Mwita ameahidi kupigania kuongezwa kwa bajeti ya Manispaa ya Geita ili kuboresha barabara na mitaro, hasa kipindi cha mvua, akisema hatua hiyo itapunguza kero za miundombinu na kusaidia wajasiriamali kufanya biashara kwa urahisi.
“Tutahakikisha barabara zinapitika na mitaro inajengwa kwa ubora ili kuondoa kero hasa wakati wa masika. Wajasiriamali watapata nafuu kubwa,” amesema Mwita.
Kwa upande wake, mgombea udiwani wa Kata ya Kalangalala, Reuben Sagayika amsema akishinda udiwani atapigania ujenzi wa Kituo cha Afya Kalangalala na Machinga Complex, kwa mujibu wa ahadi zilizomo katika Ilani ya CCM.
“Tutakuwa watu wa vitendo, si maneno. Tutahakikisha soko la Machinga linakamilika ili vijana na akina mama wapate sehemu ya kujiajiri,” amesema Sagayika.
Pia ameahidi kusimamia utoaji wa mikopo ya Halmashauri kwa wajasiriamali, akisema atashirikiana na Afisa Maendeleo ya Jamii kutoa elimu ya matumizi bora ya mikopo hiyo ili iwe na tija kwa walengwa.
“Tutahakikisha mikopo inatolewa kwa wakati na kwa walengwa sahihi. Wajasiriamali watapatiwa elimu ya uwekezaji ili fedha hizo ziwainue kiuchumi,” amesema.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Geita, Robert Nyamaigolo ametumia mkutano huo kutoa elimu kwa wananchi kuhusu matumizi sahihi ya karatasi ya kupigia kura, huku akiwaasa wazazi kuwahamasisha vijana wao kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 29.
“Tuwahimize vijana wetu washiriki kupiga kura kwa amani. Ni wajibu wetu kuchagua viongozi bora watakaoendeleza kazi nzuri iliyofanywa na serikali ya CCM,” amesema Nyamaigolo.