UDSM Yaimarisha Miundombinu ya TEHAMA Kupitia Mradi wa HEET


NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV

Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimeboresha kwa kiwango kikubwa miundombinu yake ya TEHAMA kupitia Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Uchumi (HEET), hatua itakayoongeza ufanisi katika ufundishaji, ujifunzaji na utoaji wa huduma za kimtandao chuoni hapo.

Akizungumza mbele ya wahariri wa vyombo vya habari waliotembelea chuo hicho leo Oktoba 21, 2025 kuona maendeleo ya utekelezaji wa mradi, Makamu Mkuu wa Chuo, Prof. William Anangisye, amesema UDSM sasa ina uwezo wa kupokea na kusambaza mtandao wa 10Mbps kutoka uwezo wa awali wa 1.5Mbps, jambo litakalorahisisha upatikanaji wa taarifa na maudhui ya masomo kwa njia ya kidijitali.


Prof. Anangisye amesema chuo kinaendelea kuziunganisha kampasi zake zote kwa mtandao wa ndani ili kuwezesha matumizi ya teknolojia katika ufundishaji na kujisomea, sambamba na ujenzi na ufungaji wa vifaa vya kisasa vitakavyowezesha maandalizi na uendeshaji wa masomo pamoja na mitihani kwa njia ya mtandao.

Aidha, kumbi za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua jumla ya wanafunzi 8,000 kwa wakati mmoja zimewekewa vifaa vya kisasa vya kufundishia, ikiwa ni sehemu ya maboresho ya mazingira ya kusomea.


Prof. Anangisye pia amebainisha kuwa mradi huo umewezesha uundaji wa mifumo ya kisasa ya masomo ambayo inatambulika kimataifa na inaweza kutumiwa pia na wanafunzi wenye mahitaji maalum. Hadi sasa, masomo 1,000 yamekwishaingizwa katika mfumo huo.

“Kwa sasa wanafunzi 39,000 wakiwemo 165 wenye mahitaji maalum pamoja na walimu 600 wameshaingizwa kwenye mfumo huu,” amesema Prof. Anangisye .

Aidha, kupitia Kituo cha Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (CVL), jumla ya wahadhiri 377 wamepatiwa mafunzo ya matumizi ya mifumo hiyo, na mafunzo kwa wahadhiri wengine yanaendelea. Utekelezaji huo, amesema, unaiweka UDSM katika nafasi ya kuwa kinara wa mageuzi ya kidijitali katika elimu ya juu nchini.

Kuhusu maboresho ya taaluma, Prof. Anangisye amesema jumla ya mitaala 250 imefanyiwa mapitio ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira na uchumi wa kisasa.

 
“Mitaala hii imeandaliwa kwa kuzingatia ushauri wa wadau, hususan waajiri. Tumeongeza msisitizo kwenye mafunzo kwa vitendo ili mhitimu wa UDSM awe na maarifa, ujuzi na amali kulingana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050,” ameongeza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile, alipongeza Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa usimamizi mzuri wa mradi huo, akisema majengo yanayojengwa yanaonyesha kiwango kikubwa cha utaalamu na ubunifu. 

“Leo tumeshuhudia majengo makubwa na mazuri yanayojengwa hapa UDSM kupitia mradi wa HEET. Nawapongeza kwa uhandisi mzuri na usimamizi bora. Vyombo vya habari tutaendeleza ajenda ya ubunifu wa chuo hiki na kuujulisha umma,” amesema Balile.
Balile pia amewataka Watanzania kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa amani wakati wa uchaguzi ujao kwa kusema, “Wiki ijayo tunapiga kura, chagueni viongozi mnaowataka, kura yako ndiyo itakayohesabika siyo vurugu.”

Profesa Anangisye alihitimisha kwa kusema kuwa Mradi wa HEET ni ukurasa mpya katika historia ya elimu ya juu nchini Tanzania, na kwamba Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kitaendelea kuzalisha wahitimu wabunifu, waadilifu, na wenye uwezo wa kuongoza nchi kuelekea uchumi wa kati na wa ngazi ya juu.