LIGI Kuu Bara inaendelea leo Jumatano na kuna mechi tatu za kibabe kuanzia saa 10:00 jioni hadi saa 3:00 usiku.
Katika mechi hizo, zinakutana timu ambazo hazijaachana sana nafasi na pointi, hivyo kufanya kuwa na ushindani mkubwa kwa kila moja kuhitaji ushindi.
Kwenye Uwanja wa Ali Hassan Mwinyi mkoani Tabora, TRA United itakuwa mwenyeji wa Mashujaa katika mechi ya 10:00 jioni.
Unaweza kusema TRA United (zamani Tabora United) haijaanza msimu vyema licha ya kumaliza msimu uliopita nafasi ya tano.
Msimamo wa sasa inashika mkia na pointi mbili baada ya mechi mbili huku ikiwa ndiyo timu pekee ambayo haijaonja ladha ya ushindi, pia ipo kwenye kundi la timu zisizopoteza.
Kwa upande wa wapinzani wake, Mashujaa iliyotoka kufungwa mabao 2-1 na Pamba Jiji, inaingia kwenye mechi hii ikiwa na pointi nne ilizokusanya katika mechi nne.
Timu zote hazipo vizuri kwenye kujilinda kwani TRA United licha ya kufunga mabao mawili, pia imeruhusu mawili wakati Mashujaa imefunga matatu na kuruhusu manne.
Kocha Msaidizi wa TRA United, Kassim Junior, amesema: “Tumejiandaa vizuri kwa mchezo wa kesho (leo), tunaenda kukutana na mpinzani mzuri lakini tunafahamu ubora wake ila tutatumia mapungufu yake ili tupate alama tatu muhimu.
Kocha Mkuu wa Mashujaa, Salum Mayanga, alisema: “Maandalizi ni mazuri sana kwa vijana wangu na mategemeo yangu kupambana ili kupata matokeo mazuri na kufuta makosa.”

Usiku kwenye Uwanja wa Mkwakwani, Tanga, wenyeji Coastal Union inaikaribisha Fountain Gate, timu ambayo imetoka kupata ushindi wake wa kwanza kwenye ligi kwa kuichapa Dodoma Jiji bao 1-0.
Mechi hii inazikutanisha timu ambazo zimepishana pointi moja pekee, Coastal Union inazo nne na Fountain Gate tatu, zote zikishuka dimbani mara nne.
Ushindi wa nyumbani ilioupata Fountain Gate ukiwa ni wa kwanza kwao msimu huu, unaweza kuwapa nguvu katika mechi hii ya ugenini, lakini Coastal Union ina hasira kutokana na tayari imeonja ladha ya kipigo ikiwa nyumbani ilipofungwa 2-1 na JKT Tanzania, huku mechi ya mwisho dhidi ya Mtibwa Sugar, ikitoka 0-0. Kabla ya hapo, ilichapwa 2-0 na Dodoma Jiji, lakini ilianza kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons.
Fountain Gate ilianza kufungwa 1-0 na Mbeya City, ikachapwa 3-0 na Simba, kisha ikalambwa tena 2-0 na Mtibwa, kabla ya kuamkia kwa Dodoma Jiji ikishinda 1-0.
Kocha wa Coastal Union, Mohammed Muya, amesema: “Nawaheshimu sana Fountain Gate ila tumefanya maandalizi mazuri ya kupata alama tatu, makocha waliopo nawafahamu na wao wananifahamu, hivyo hii ni kama Dabi ya Makocha, tumefanya maandalizi ya kuwapa furaha mashabiki wa Coastal.”
Nahodha msaidizi wa Coastal Union, Geofrey Manyasi alisema: “Baada ya mchezo dhidi ya Mtibwa, kocha ametuandaa vizuri kucheza dhidi ya Fountain, tunaamini maandalizi yetu ni mazuri na wachezaji wote tuko tayari kwa mchezo.”
Kocha wa Fountain Gate, Mohamed Ismail ‘Laizer’ amesema anaamini watakutana na ugumu katika mechi dhidi ya Coastal Union kwa sababu wanakwenda kukutana na kocha Mohammed Muya ambaye amewahi kufanya kazi Fountain Gate.

Ni mechi ambayo inafunga siku ya leo ikipangwa kuchezwa Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma kuanzia saa 3:00 usiku. Inazikutanisha timu ambazo zote zina pointi nne na zikitumia uwanja mmoja kwa mechi za nyumbani.
Dodoma Jiji ndio mwenyeji ikiwa imecheza mechi nne, ikionekana kuutumia uwanja wa nyumbani vizuri kwani mechi moja pekee iliyocheza hapo imeshinda, huku ikipoteza mbili za ugenini na sare moja.
Mtibwa Sugar iliyohamia uwanjani hapo baada ya kuachana na Uwanja wa Manungu kutokana na kutokidhi vigezo, yenyewe imeshuka dimbani mara tatu, huku mbili zikiwa nyumbani ikishinda moja na sare moja, ugenini ilikuwa dhidi ya Mashujaa ikipoteza kwa bao 1-0.